Release No. 203
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 28, 2012
KLABU ZASUBIRI FEDHA ZAO
TRA ZICHEZE LIGI KUU
Klabu 14 ambazo timu zao
zinashiriki Ligi Kuu ya Vodacom zimesema hazitacheza hatua ya pili ya Ligi hiyo
inayotarajiwa kuanza Januari 26 mwakani hadi zitakaporejeshewa fedha zao
zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka kwenye moja ya akaunti
za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
Novemba 23 mwaka huu,
TRA kwa uwezo ilionao kisheria iliielekeza benki ya NMB kuilipa fedha hizo (sh.
157,407,968) kutoka kwenye moja ya akaunti za TFF ikiwa ni Kodi ya Lipa Kama
Unavyopata (PAYE) kutoka kwenye mishahara ya waliokuwa makocha wa timu za
Taifa.
Serikali ndiyo inayolipa
mishahara ya makocha hao moja kwa moja kwenye akaunti zao, lakini ilikuwa
haikati PAYE kutoka kwenye mishahara hiyo, hivyo malimbikizo kufikia sh.
157,407,968.
TFF bado inaendelea na
mazungumzo na pande husika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa
upande mmoja na TRA kwa upande mwingine) ili fedha hizo zirejeshwe kwani
zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu (kampuni ya Vodacom) kwa ajili ya maandalizi
ya timu hizo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.
OFISA WA CAF KUTUA
MWAKANI KUKAGUA VIWANJA
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) litamtuma nchini ofisa wake Abbas Sendyowa kukagua viwanja
na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa klabu kupata leseni
zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho hilo .
Ofisa huyo kutoka Uganda
atawasili nchini Januari 7 mwakani ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo
Januari 14 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.
Utekelezaji wa kazi yake
nchini utahusisha mwakilishi kutoka TFF, mwakilishi kutoka Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, mameneja wa viwanja husika na Ofisa Usalama wa
TFF.
NAZARIUS KILUNGEJA
AONDOLEWA UCHAGUZI RUREFA
Kamati ya Uchaguzi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kumuondoa Nazarius
Kilungeja kugombea uenyekiti katika uchaguzi wa chama hicho.
Kutokana na uamuzi huo,
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA kuendelea na
mchakato wa uchaguzi huo kama ilivyopangwa
awali.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment