Sunday, December 30, 2012

TCRA kuanza kuzima mitambo ya Dar es Salaam kwanza.... Analogia kuenda Dijitali


WAKATI zimebakia saa 24 Tanzania kuungana na nchi nyingine duniani kuanza kurusha matangazo ya televisheni kwa mfumo wa Dijitali zikiachana na ule wa Analojia, imebainika kuwa mpango huo utaanzia Mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Habari za ndani kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zilizolifikia Mwananchi Jumapili, zinaeleza kuwa Jiji la Dar es Salaam pekee, ndiyo litakuwa la kwanza kuingia kwenye mfumo huo kuanzia Januari mosi, 2013 na siyo mikoa mingine nchini.
TCRA, imeshatangaza kuwa itaufunga mfumo wa analojia ifikapo Desemba 31 mwaka huu yaani kesho.
Habari hizo zimeeleza kuwa mamlaka hiyo imeamua kuchukua hatua za tahadhari katika utekelezaji wa mpango huo muhimu, kwa kuanza na mji mmoja baada ya mwingine, ambapo  mwezi mmoja baada ya Dar es Salaam kuanza kutumia mfumo wa dijitali, utafuatia Mkoa wa Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma alipoulizwa aliliambia gazeti hili jana kwamba mamlaka yake itatoa ufafanuzi kuhusu suala hilo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.
“Hatuwezi kukurupuka katika suala hili, tuko makini, lakini kesho (leo), tutakuwa na mkutano wa wanahabari kwa ajili ya kueleza mikakati mbalimbali na jinsi tulivyojipanga katika jambo hili,” alisema Profesa Nkoma.
Tayari TCRA imetaja miji mingine mbali ya Dar es Salaam ambayo imeshaunganishwa katika mfumo wa dijitali kuwa ni pamoja na Arusha, Mwanza, Tanga, Mbeya, Moshi na kwa sasa mji wa Morogoro unajengewa miundombinu husika.
Habari zaidi zilieleza kuwa kwa utaratibu uliopo sasa itachukua miezi kadhaa kabla ya kuzimwa kwa mfumo wa analojia katika miji minane ya awali, ambapo pia itachukua muda mrefu zaidi kuzimwa mfumo huo nchi nzima.
Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU), limezitaka nchi zote duniani kuhamia kwenye mfumo huo wa kurusha matangazo ya televisheni wa dijitali kutoka mfumo wa analojia ifikapo Julai 2015.
Ikiwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Tanzania imeanza kutekeleza azimio la nchi hizo ilizozitaka kufanya hivyo mwaka huu wa 2012, badala ya kusubiri hadi tarehe ya mwisho iliyowekwa na ITU.  
Wakati Tanzania ikiwa mstari wa mbele kuhamia kwenye mfumo huo wa dijitali, ingawa kwa mtindo wa awamu, nchi nyingine wanachama wa EAC hasa Kenya na Uganda bado hazijaingia katika mfumo huo.
TCRA imezikabidhi kampuni tatu kufanya kazi ya usambazaji wa mfumo huo wa dijitali, ambazo ni Basic Transmissions  inayoundwa na Kampuni za IPP Media na Sahara
Communications, Kampuni ya Ting ya Agape Associates na Star Media Tanzania Limited (Startimes) ambayo ina ubia na  Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Star Communications and Technology ya China.
TCRA imekuwa ikielezea kuwa Tanzania ipo tayari kujiunga na mfumo huo kwa kuwa asilimia kati ya 22 kati ya 24 ya nchi ambayo inatumia analojia, tayari imefikiwa na mtandao wa mfumo wa dijitali, ikijumuisha miji minane ambayo kwa kiasi kikubwa kampuni ya Startimes imeifikia.
Hata hivyo, baadhi ya watu wameshindwa kuzielewa takwimu hizo kwa kuwa mitambo ya analojia ipo katika mikoa kadhaa nchini, ambayo bado haijapata mfumo wa dijitali. Mikoa hiyo ni pamoja na Lindi, Tabora, Bukoba, Musoma, Kigoma na Singida.
Kampuni ya Startimes ndiyo inayoongoza kwa kuwa na wateja wengi ambapo hadi sasa inakadiriwa kufikisha wateja 350,000,  Kampuni ya Ting ikiwa na wateja 10,000, huku Kampuni ya Basic Transmissions ikitangaza kuanza shughuli zake hivi karibuni.
Bei ya king’amuzi ni Sh39,000 ingawa mnunuzi anapaswa kulipia fedha za ziada kwa ajili ya kifurushi atakachochagua.
Hata hivyo, utata bado unagubika urushaji huo wa chaneli za bure ambazo ni ITV, Star TV, TBC1, Channel Ten na Eat Africa TV ikielezwa kuwa wamiliki wa vituo hivyo hawataki zionyeshwe bure kwenye kila king’amuzi bali ving’amuzi vyao pekee.
TCRA imeeleza kuwa kwa sasa imefanikiwa kupata ufumbuzi wa muda, ambapo chaneli zote zinaweza kuonekana bure kwenye kila king’amuzi.
Wananchi wachangamkia ving’amuzi
Katika hatua nyingine, gazeti hili lilifika katika ofisi za makao makuu ya Startimes jijini Dar es Salaam na kukuta mamia ya wananchi wakiwa katika foleni ya kununua ving’amuzi hivyo.
Baadhi ya wananchi hao walionyesha masikitiko yao baada ya kufutwa kwa malipo ya mwezi ya Sh9,000, badala yake kubaki malipo ya Sh23,000 na 36,000 kwa mwezi.“Kwa sasa wametoa ofa, ukinunua king’amuzi kwa Sh39,000 utalipia malipo ya mwezi ya kati ya Sh13,000 au Sh23,000, kile kifurushi cha bei nafuu wamekifuta na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa,” alisema Hadji Jumanne mkazi wa Kijitonyama.
Naye Happy Lazaro alisema Serikali inatakiwa kuongeza muda ili kuwapa fursa wananchi kununua ving’amuzi hivyo kwa kuwa hivi sasa imekuwa vurugu na huenda mitambo ya analojia ikazimwa huku wengi wakiwa hawajapata ving’amuzi hivyo.
Hata hivyo, watendaji wa kampuni hiyo waligoma kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazotolewa na wateja wao ikiwa ni pamoja na ubovu wa baadhi ya ving’amuzi, mabadiliko ya bei ya vufurushi kwa maelezo kuwa siyo wasemaji.
Chanzo: Mwananchi.com

No comments:

Post a Comment