Sunday, December 30, 2012

Tanzania nchi inayoongoza kwa kuomba misaada....

Na Zitto Kabwe
Tanzania imekuwa moja ya nchi kipenzi kwa mataifa ya nje yaliyoendelea. Mapenzi haya yameonyeshwa kwa sura nyingi, ikiwamo kumiminiwa misaada ya kifedha na hata uwekezaji mkubwa kupitia kampuni za kutoka nchi hizo.
Takwimu za misaada ambayo Tanzania imekuwa ikipata zimekuwa za kukanganya na wakati mwingine zinazotiwa chumvi kulingana na malengo ya mtoa takwimu.
Kuna kijitabu kinachoeleza kuhusu misaada hii na mambo mengine, kinaitwa Pocket World in Figures huchapishwa na jarida la The Economist. Tangu mwaka 2006 nimekuwa msomaji asiyekosa kusoma kijitabu hiki.
Mwaka huu pia kijitabu hiki, 2012 Edition, kimetoa takwimu za ‘wapokea misaada’ na ‘watoa misaada’ duniani.
Tanzania nchi ya kwanza Afrika Mashariki, ya tatu Afrika na ya sita duniani kwa kupokea misaada.Mwaka 2010 Tanzania ilipokea misaada ya jumla ya dola za Marekani bilioni 2.9.
Misaada hii ilikuwa chini ya nchi kama Afghanistan (dola bilioni 6.3), Ethiopia (dola bilioni 3.5), CongoKinshasa (dola 3.4bn), Haiti (dola 3bn) na Pakistan (dola 3bn). Hivyo katika nchi za Afrika, Tanzania ni taifa la tatu kwa kupokea misaada mingi zaidi na ni la kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki.
Hata hivyo, inabidi kusoma takwimu hizi kwa mapana yake kidogo kwa kuangalia, kwa mfano, katika mwaka huo kila Mtanzania alipata msaada wa dola ngapi.
Kijitabu hicho kinatoa takwimu hizo pia na msaada kwa kila kichwa (aid per head) kwa kila Mtanzania ilikuwa ni dola 64.
Hapa Tanzania ilizidiwa na nchi kadhaa za Afrika ikiwamo Congo – Brazzavile (dola 325), Namibia (dola 113.5), Msumbiji (dola 84), Mauritius (dola 98), Botswana (dola 78) na Burundi (dola75).
Hata kwenye kipimo hiki bado Tanzania imeshika nafasi ya pili katika nchi za Afrika Mashariki katika kupokea misaada kulingana na idadi ya watu kwa kuishinda Burundi tu.
Ufisadi na misaada
Ni vema kuongeza kuwa nchi za Afrika Mashariki zinazoongoza kwa misaada, Tanzania na Uganda, ndizo pia zinaoongoza kwa ufisadi. Kwa mujibu wa taasisi ya Transparency International,Uganda inaongoza kwa ufisadi ikifuatiwa kwa karibu na Tanzania katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Je, kuna uhusiano wa kisayansi kati ya ufisadi na misaada kutoka nje?
Inawezekana inahitajika utafiti kuonyesha uhusiano huo. Nchi zenye kupokea misaada mingi hufanya serikali zao kuwajibika kwa watoa misaada zaidi kuliko wananchi wake na hivyo kupuuza vita dhidi ya ufisadi inayoendeshwa na raia wa nchi husika.
Laana ya rasilimali (resources curse)
Asilimia 45 ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi inatokana na madini, na hasa dhahabu. Tanzania ni nchi ya nne Afrika, baada ya Afrika Kusini, Ghana na Mali, kwa uzalishaji wa dhahabu, mwaka 2011 iliuza nje dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.3.
Tangu uzalishaji mkubwa wa dhahabu uanze nchini mwaka 1998, Tanzania imekwishauza nje dhahabu ya thamani ya dola za Marekani bilioni 11.3.
Katika kipindi hicho mapato ya serikali kutokana na vyanzo vyote vya mapato kwenye sekta ya madini ni dola za Marekani milioni 455 tu.
Licha ya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya madini na kukua kwa uchumi kwa kasi ya zaidi ya asilimia sita kwa mwaka, bado umasikini wa Tanzania umeendelea kuwa mkubwa zaidi.
Utajiri wa madini na misaada kutoka nje vimeshindwa kupunguza umasikini na badala yake zaidi ya Watanzania milioni wameingia katika dimbwi la umasikini katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 na 2010.
Laana ya misaada?
Nchi ambayo takribani theluthi ya bajeti yake inategemea misaada kutoka nje lakini ikiwa na ufisadi na umasikini mkubwa inakuwa imeathirika kwa laana ya misaada (aid curse).
Ingawa watafiti wengi wameandika kuhusu ‘laana ya rasilimali’, kuna haja ya kufanya tafiti kuona kama kuna uhusiano kati ya wingi wa misaada kwa nchi na kushindwa kuendelea kwa nchi husika. Licha ya misaada ambayo Tanzania imekuwa ikipokea bado ni miongoni mwa nchi 18 duniani zenye pato dogo zaidi kwa mtu (GDP per head).
Hata hivyo kwa kipimo cha maendeleo ya watu (human development index), Tanzania imejichomoa kutoka kwenye nchi 25 masikini zaidi duniani. Asilimia 35 ya Watanzania wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa kwa mujibu wa taarifa za serikali (PHDR 2011).
Uzoefu wa Tanzania unaonyesha kuwa misaada mingi kutoka nje sio suluhisho la maendeleo ya watu.
Tanzania bilamisaada
Tanzania iache kupokea misaada ili kujikita kwenye kuongeza mapato ya ndani na kujitegemea? Tanzania bila misaada inawezekana? Jawabu ni uwajibikaji tu. Tukijenga misingi ya uwajibikaji na kuwajibishana tutaweza kuendesha nchi yetu bila kutegemea misaada, kwa kuondoa matumizi ya hovyo kama posho, magari na safari za nje, kukuza mapato ya ndani kwa kupanua wigo wa kodi na kukusanya zaidi kama tunavyostahili kutoka sekta ya madini na kasha mafuta na gesi asilia na kuwekeza vya kutosha kwenye kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Nchi tajiri ziache kutoa misaada kwa Tanzania kuanzia bajeti ijayo ya mwaka 2013/14. Hatutakufa.Tutajitegemea!
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment