Tuesday, December 18, 2012

Sita wafungiwa kucheza soka Zanzibar yumo Cannavaro wa Yanga na Solembe wa Coastal...


Na Salum Vuai, Maelezo CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimewafungia kucheza mpira ndani na nje ya nchi kwa muda wa mwaka mmoja wachezaji sita wa timu ya Taifa Zanzibar Heroes, kuhusiana na kugawana mgao wa dola elfu kumi walizopata katika mashindano ya Chalenji hivi karibuni. Awali, Kamati Tendaji ya chama hicho ilitangaza kuwasimamisha kwa muda usiojulikana wachezaji wa timu hiyo waliokaidi kurejesha dola mia tano kila mmoja, walizopata kutokana na mgao huo wa dola elfu kumi walizopata kwa kushika nafasi ya tatu kwenye michuano hiyo iliyofanyika Uganda. Hatua ya kuwafungia wanasoka hao, imekuja kufuatia nahodha wa timu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na msaidizi wake Aggrey Morris, kushindwa kufika ofisi za ZFA Ijumaa iliyopita, walikoitwa kwenda kutoa maelezo kuhusiana na sakata hilo. Barua ya ZFA iliyoandikwa Disemba 15, 2012 ikiwa na nambari ya kumbukumbu ZFA/2/2012 kwenda kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imewataja wanasoka hao waliofungiwa kwa kile kilichodaiwa utovu wa nidhamu, kuwa ni, Aggrey Moris, Khamis Mcha, (Azam FC), Nassor Masoud (Simba SC), Nadir Haroub (Young Africans SC). Twaha Mohamed (Mtibwa Sugar) na Suleiman Kassim (Coastal Union). Hata hivyo, katika orodha hiyo yumo pia mchezaji Seif Abdallah aliyesajiliwa na Azam hivi karibuni akitokea Ruvu Shooting, ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wamerejesha fedha hizo awali. Zanzibar Leo, iliwasiliana na aliyekuwa Meneja Fedha wa Zanzibar Heroes Said Omar Kwimbi kujua juu ya mchezaji huyo, ambaye alikiri kuwa Seif alikwisharejesha fedha hizo. Aidha, uongozi wa ZFA umefahamisha kuwa, baba mdogo wa mlinda mlango Mwadini Ali ambaye kwa sasa yuko ziarani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na klabu yake ya Azam, alifika katika ofisi za chama hicho akiwa na salamu za familia, kwamba inabeba jukumu la kuzirejesha fedha hizo. Taarifa ya Kamati Tendaji ya ZFA iliyokutana Novemba 14, mwaka huu kujadili kitendo cha utovu wa nidhamu kilichofanywa na wachezaji wa timu hiyo kupora fedha hizo dola elfu kumi kiliamua kuchukua hatua zifuatazo: ZFA imewapongeza na kuwasamehe wachezaji wote waliotanabahi na kujutia kitendo hicho na kuamua kuzirejesha fedha walizochukua. Aidha pamoja na kukilaani kitendo hicho, ZFA imesema wachezaji wote ambao wanaendeleza kiburi kwa kukaidi kurejesha fedha hizo wanafukuzwa mara moja kutoka katika timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), na hivyo kuzufungiwa kushiriki mashindano yoyote yatakayoandaliwa na ZFA au kwa kushirikiana na taasisi nyengine kwa muda wa mwaka mmoja. Aidha, imewazuia kuwemo, kushiriki au kuwa na haki ya kushiriki katika timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kipindi kama hicho, na kwa hatua hiyo inawaondoa mara moja katika orodha ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania. Taarifa hiyo imesema, kwa kuzingatia kuwa hakuna TFF bila Zanzibar, na kwamba kuikosea Zanzibar na ZFA ni sawa na kuikosea TFF na Tanzania, hivyo wachezaji hao wanafungiwa kucheza mpira nje na ndani ya Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja. Imeelezwa kuwa, utekelezaji wa adhabu hizo unaanza mara moja kuanzia tarehe ya barua hiyo (Disemba 15, 2012), ambapo TFF imeombwa kutoa ushirikiano na kuhakikisha kuwa wachezaji wote waliotajwa ambao wameteuliwa katika Taifa Stars wanaondoshwa mara moja kwenye timu hiyo. Habari zaidi kutoka ndani ya ZFA zimeeleza kuwa, kufuatia hatua hizo, kwa sasa hakuna tena nafasi wala mchezaji yeyote aliyekwishafungiwa, kurejesha fedha hizo, na kwamba hazitapokelewa, wala hakuna msamaha utakaosikilizwa. Mbali ya barua hiyo kunakiliwa kwa uongozi wa juu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo na BTMZ, pia nakala zimepelekwa kwa klabu za Azam, Simba, Yanga, JKT Oljoro, African Lyon na Coastal Union.

No comments:

Post a Comment