Friday, December 21, 2012

Lulu aweka wazi uhusiano wake na marehemu Kanumba...


UHUSIANO wa kimapenzi baina ya msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael 'Lulu' anayedaiwa kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba, umewekwa wazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya msanii huyo kukiri kuwa alikuwa na uhusiano na Kanumba.

Upande wa serikali jana Ijumaa ulisoma maelezo ya mashahidi tisa wanaotarajia kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo pamoja na maelezo ya Lulu aliyoyatoa Kituo cha Polisi Oysterbay, ambayo ni moja ya vielelezo vitakavyowasilishwa mahakamani wakati kesi itakapoanza kusikilizwa rasmi.

Akisoma maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando, Wakili wa serikali, Shadrack Kimaro, alidai kuwa Lulu alitoa maelezo hayo Aprili 7 mwaka huu katika kituo cha polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam mbele ya askari wa kituo hicho, Sajenti Renatus.

Alidai kuwa Lulu alizaliwa mwaka 1994 na kwamba ana elimu ya Kidato cha Nne aliyoihitimu katika Shule ya Sekondari ya Midway, baada ya hapo aliendelea na shughuli za sanaa ambazo alizianza tangu mwaka 2000.

Alidai kuwa Lulu alifahamiana na Kanumba kwa muda wa miaka 10 wakifanya kazi za sanaa na Januari mwaka huu ndipo walipoanza rasmi uhusiano ya kimapenzi.

Alidai kuwa katika uhusiano huo hawakuwahi kuishi pamoja isipokuwa alikuwa akienda kwa Kanumba anapojisikia na mara kadhaa aliwahi kulala huko.

Wakili huyo alidai kuwa katika kipindi cha miezi minne ya uhusiano wao, walikuwa wakigombana mara chache lakini sababu kubwa ilikuwa ni wivu wa mapenzi kwa sababu wote walikuwa hawaaminiani.

Pia Wakili huyo alidai kuwa Aprili 5, mwaka huu Kanumba na Lulu walitumiana ujumbe mfupi wa simu.

Alidai kuwa jioni ya siku hiyo Lulu alimpigia simu Kanumba na baada ya muda mfupi alikwenda nyumbani kwake Sinza Vatican.

Alidai kuwa alipofika kwa Kanumba, alimkuta akiwa chumbani kwake akinywa pombe ambayo ilikuwa imechanganywa na soda na ghafla simu yake iliita na alipotoka nje kutaka kwenda kuisikiliza Kanumba alimfukuza hadi barabarani.

Alidai kuwa baada ya kumfukuza alimkamata na kuanza kumpiga vibao na mateke huku akilalamika kwamba anamdharau na alimpeleka hadi chumbani ambapo alichukua panga lililokuwa chini ya kitanda na kuanza kumpiga kwa ubapa.

Alidai kuwa baada ya kumpiga kwa ubapa ghafla alitupa panga chini huku akiwa amesimama alianza kupumua kwa taabu na baada ya muda mfupi aliyumba na kujigonga ukutani na kuanguka chini.

Alidai baada ya kuanguka, Lulu alikimbia na kwenda kujifungia chooni kwa hofu na baada ya muda alitoka na maji na kwenda kummwagia Kanumba lakini hakuamka.

"Siyo mimi niliyemuua nilimkuta amekunywa pombe na alikasirika sana kupita kiasi...siwezi kumsukuma ila yeye anaweza kunifanya atakavyo,"alidai Lulu.

Alidai kuwa baada ya kuona hali hiyo alishikwa na hofu na kuamua kukimbia kwenye ufukwe wa Coco Beach. Alidai kuwa akiwa huko alipewa taarifa kuwa Kanumba amefariki na ndipo alipompigia simu rafiki yake ili aende kumsaidia kuendesha gari waelekee kwenye msiba.

Uchunguzi wa awali wa polisi ulionyesha kuwa hakukuwa na jeraha lolote kuanzia kichwani hadi mwilini kwa Kanumba.

Inadaiwa kuwa uchunguzi wa kifo hicho ulifanywa na jopo la madaktari watatu na daktari mmoja wa familia kutoka hospitali ya Amana ambapo ulibaini kuwa ubongo wa Kanumba ulikuwa umevimba na damu imevilia.

Baada ya uchunguzi huo sampuli kadhaa kama kucha za mikono yote miwili, majimaji ya machoni, ini, figo, damu vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Baada ya kusomwa maelezo hayo Hakimu Mmbando alimuhoji Lulu kama ana lolote la kuongea na baada ya kujadiliana na Wakili wake, Lulu alijibu kuwa hana cha kuongea.

"Kesi yenu kwa hapa Kisutu imefikia mwisho kwa hiyo jalada litapelekwa Mahakama Kuu tayari kwa kuanza kusikilizwa...utaendelea kukaa mahabusu hadi utakapoletewa wito wa kufika Mahakama Kuu,"alisema Hakimu Mmbando na kuahirisha kesi hiyo.
Chanzo: Gazeti MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment