Rais jakaya Kikwete, amewataka watanzania kufanya kazi kwa
nguvu ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanaenda sawa na
ongezeko la watu nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa matokeo ya sensa ya idadi ya
watu na makazi katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam leo asubuhi,
Kikwete amesema idadi ya watu Tanzania
inaongezeka kwa asilimia 2.9 kutoka mwaka 2002 ilipofanyika sensa ya mwisho na
kutoa matokeo ya watu milioni 34.4 ambapo alitabiri itakapofika mwaka 2016
idadi ya watu nchini itafikia milioni 51.
Aidha matokeo ya sensa kwa mwaka huu wa 2012 yanaonyesha Tanzania
ina jumla ya watu Milioni 44,929,002 ambapo Tanzania Bara ni Milioni 43,625,434
na Tanzania Visiwani ni Milioni 1,303,568.
“Idadi hii inaonyesha dalili mbaya ambapo nchi itakuwa na
mzigo mkubwa katika masuala ya kijamii na kiuchumi, idadi kubwa ya watu inamaanisha
Serikali iongeze mikakati ya kimaendeleo ili kukabiliana na ongezeko hili la
watu,” alisema Kikwete na kuongeza;
“Umuhimu wa kupanga uzazi uanze sasa, maana ushindani wa
rasilimali chache tulizonazo utakuwa mkubwa sana miaka ya usoni, hivyo ni vema wananchi
wakajulishwa umuhimu wa kupanga uzazi.”
Tangu Tanzania
iundwe mwaka 1964 baada ya kuunganishwa Tanganyika
na Zanzibar ,
hii ni sensa ya tano kufanyika ambapo sensa ya kwanza ya mwaka 1967 idadi ya
watanzania ilikuwa ni milioni 12,313,54 (milioni 12.3). Tanzania bara ilikuwa na watu milioni 11,958,654
(milioni 11.9) na Tanzania
visiwani kulikuwa na watu laki 3,544,00 (laki 3.5).
Hata hivyo sensa ya mwaka 2002 ilionyesha ongezeko kubwa la
watu waliofikia milioni 43.625,434 (milioni 43.6) Zanzibar peke yake ilikuwa na wakaazi milioni
1.335,68 (milioni 1.3).
Katika hatua nyingine Rais Kikwete amesema haya ni matokeo ya
awali ambayo yameonyesha idadi ya watu kwa ujumla. Lakini ikifika mwezi
februari 2013 yatatolewa matokeo mengine yatakayoonyesha idadi ya watu kwa
jinsia yaani wanawake wapo wangapi na wanaume wapo wangapi.
Mwezi Aprili 2013 yatatolewa matokeo mengine yatakayoonyesha
idadi ya watu kwa umri kuanzia kata, wilaya na mikoa. Na ikifika mwezi June 2013
zitatolewa takwimu nyingine zitakazoonyesha watu wenye ajira, idadi ya kaya na
masuala mingine ya kitakwimu.
Awali waziri mkuu Mizengo Pinda ambae ndie mwenyekiti wa
kamati kuu ya sensa taifa amesema Serikali kwa mwaka huu imeendesha sensa kwa
asilimia tisini (90%) na asilimia 10 (10%) ni wahisani, tofauti na mwaka 2002
ambapo serikali iligharamia zoezi la sensa kwa asilimia 70 (70%).
Aidha Pinda aliongeza kuwa kwa mwaka huu wataalamu wa ndani
katika zoezi zima walitumika sana
tofauti na mwaka 2002, ambapo kwa mwaka huu wataalamu wa kutenga maeneo ya
sensa walikuwa 150, makarani 20,000 na wataalamu wengine wa takwimu 400 wote
watanzania.
Pesa zilizotumika kuwalipa posho za kuendesha sensa ni
milioni 90, ambapo waliweza kutoa zabuni 29 za kuendesha zoezi zima kwa kampuni
za kizalendo zipatazo 29 na kuwalipa kiasi cha bilioni 11.7.
Mpaka matokeo ya awali ya sensa yanatangazwa leo serikali
imetumia kiasi cha Sh bilioni 120 na kwa mujibu wa rais Kikwete ifikapo mwezi
June 2013 yatakapotangazwa matokeo ya mwisho serikali itakuwa imetumia kiasi
cha Sh bilioni 140 kwa zoezi zima.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM ,
TANZANIA
kidojembe@gmail.com
+255 752 593894/ +255 713 593894
No comments:
Post a Comment