JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
|
|
|
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 14/12/2012
KWA NINI LAMBALAMBA WANAPIGWA VITA DODOMA
Hili ni
kundi la watu ambalo wameliunda kwa lengo la kujihusisha na vitendo vya
kitapeli na ulaghai kwa wananchi hususani wa vijijini, ili kujipatia mali
zikiwemo fedha na mifugo ya aina mbalimbali toka kwa wanavijiji katika mkoa
wetu wa Dodoma.
Kundi hili
ni mkusanyiko wa watu wa jamii tofauti ambao wanatoka maeneo ya Rufiji , Pwani, Tanga na Morogoro ambao
wamekuja kuivamia jamii ya watu Dodoma
ambayo nayo ina mila na desturi zake katika mambo ya jadi.
Wamekuwa
wakitumia mtindo wa kujifanya kuwa wao ni waganga wa tiba za jadi kwamba wana
uwezo wa kutoa vitu vya kichawi katika
majumba ya watu, sehemu za biashara na
pia kufichua wachawi, vitu
ambavyo kwa hakika hawana uwezo navyo.
Ili mtu
akubalike kuwa ni mganga wa tiba za jadi ni lazima afahamike katika eneo
analofanyia shughuli zake hizo kuanzia uongozi wa ngazi ya chini hadi wa juu wa serikali na
awe na kibali cha kuendesha tiba hizo kisheria kitu ambacho kundi la lamba
lamba hawakidhi matakwa hayo.
Pia Mganga
wa jadi kwa asili yake hatakiwi kufanya kazi zake kwa kuita baadhi ya watu ni
wachawi. Hutakiwa kutoa tiba na kinga kwa kutumia miti shamba kulingana na
uwezo wake, na sio wanachofanya hao wanaojiita lambalamba hii ni tofauti na
sheria zinavyoelekeza.
Kwanza
wanavijiji huchangishwa na
ndipo huitwa kundi hilo kuja kufanya kazi
wanayodai ni ya kufichua wachawi au washirikina, ambao wanadai wanavuta mali za watu
wengine kwao na kuwa matajiri.
Uchunguzi
wetu umebaini kwamba wanachofanya kundi la lambalamba kwa kushirikiana na washirika
wao, huwa wanapandikiza vitu kwenye nyumba, mashamba au sehemu za biashara za
mlengwa nyakati za usiku.
Baada ya
kufanya hivyo ndipo wanaondoka na kundi la watu na kwenda kutoa vitu ambavyo
walishavipandikiza kabla, kisha kinachotokea kwa anayefanyiwa hivyo ni kudhalilika
yeye na familia yake kuwa ni
mchawi na kibaya zaidi hulazimishwa kutoa kiasi cha fedha na mifugo kama adhabu
na kutishiwa wasithubutu
kwenda kutoa taarifa Polisi.
Hili ni
kosa la jinai na ukiukwaji mkubwa wa haki za Binadamu, hatuwezi kuvumilia na
kuwaacha wananchi wenzetu kuendelea kupoteza fedha na mali zao kwa
kuwanufaisha hao matapeli.
Zipo
taarifa kuwa lambalamba hao wanapofika vijijini hutafutiwa wanawake wa kuwapikia
na kuwastarehesha. Huu ni unyanyasaji wa kijinsia na jambo la hatari ambalo
litachangia kuenea kwa magonjwa ukiwemo UKIMWI.
Haya
yanayofanyika ni utapeli mkubwa uliobuniwa na watu hao wa kujipatia fedha. Ni
jambo linalodhalilisha, linalojenga chuki, na uchochezi ndani ya jamii. Pia
linahatarisha usalama na amani
pamoja na afya za wanawake na jamii kwa ujumla.
Hili ni
jambo la kukemea kuanzia ngazi ya Familia, Kitongoji, Mtaa, Kata hadi Taifa.
Wote kwa pamoja tunaona athari zake tukemee kwa nguvu zote na wale wanaoendesha
na kushabikia kundi hilo
watolewe taarifa ili wakamatwe.
Watu
wasiogope kutoa ushahidi dhidi ya kundi la lamba lamba na washirika wake hao
wanaovuruga amani, utulivu, usalama na kurudisha maendeleo nyuma.
Tupo kwenye
karne ya Sayansi na Teknolojia tusijiaibishe kwa kukumbatia mambo ya zama za
kiza kwa kupumbazwa akili zetu na matapeli waliobuni mradi wa kujipatia fedha
na mali kwa ujanja wa kupandikiza vitu kwenye nyumba, sehemu za biashara na
mashamba, kisha baadaye wanakuja kuvitoa na kudai wamefanya hivyo kwa uwezo wao
wa kubaini wachawi na kuifanya jamii yetu iishi kwa chuki na kukosa amani na
kushindwa kufanya shughuli za kujiletea maendeleo
Mwisho
napenda kutoa wito kwa wananchi kwa ujumla kupitia
dhana ya utii wa sheria kwa hiari kushirikiana kwa pamoja na Jeshi la
Polisi kwa kutoa taarifa za watu hao
ili kuutokomeza uhalifu huu ili jamii yetu iendelee kubaki salama na yenye amani na utulivu.
[D. A. MISIME – ACP]
KAMANDA WA POLISI [M] DODOMA
CONTACT:
POLISI
MKOA WA DODOMA
DAWATI
LA HABARI, ELIMU NA MAHUSIANO,
Phone: 0715 006523, Luppy Kung’alo – Mrakibu
msaidizi wa Polisi (ASP)
Phone: 0712 360203, Silyvester Onesmo –
Police Konstebo (PC)
No comments:
Post a Comment