Wachezaji wa Azam FC wakikaguliwa pasi zao za kusafiria mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Kinshansa...
Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
WAWAKILISHI wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Soka
Afrika, (CAF), Azam FC wamewasili salama mjini Kinshasa ,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) majira ya saa 5:58 usiku wa jana kwa saa
za huku na saa 7:58 kwa saa nyumbani Tanzania , tayari kucheza mashindano
ya Kombe la Hisani mjini hapa.
Hata hivyo, Azam
wamewasili pungufu ya watu watano katika msafara wao wa watu 27, kufuatia
maofisa na wachezaji wa kigeni kuzuiliwa mjini Nairobi , Kenya
kwa kutokuwa na viza za kuingia DRC.
Wenyeji wa Azam, waandaaji
wa mashindano waliwahakikishia wageni wao hakutakuwa na tatizo la kuingia DRC
bila viza, kwa kuwa wamekwishaandaa utaratibu mzima na msafara mzima utapatiwa
viza mara utakapowasili Kinshasa .
Hata hivyo, kwa ujumla
hali ilikuwa tofauti, Kocha Mkuu Stewart Hall, Msaidizi wake, Kali Ongala, wote
raia wa Uingereza, Daktari Paulo Gomez, raia wa Ujerumani na wachezaji Kipre
Tcheche na Kipre Balou raia wa Ivory Coast walizuiwa mjini Nairobi.
Mkuu wa msafara,
Katibu wa Azam, Nassor Idrisa alitumia busara kwa kuwapatia fedha za malazi na
kujikimu watu hao watano ili wabaki Nairobi
kushughulikia viza na wataungana na timu leo baadaye.
Aidha, baada ya kufika
Uwanja wa Ndege wa Njili mjini hapa, msafara wa Azam pia ulipata misukosuko
mingine, kuanzia uwanjani hapo, wakati Maofisa wa Idara ya Uhamiaji walipokataa
kuupokea kwa sababu ya viza.
Ilifikia hatua Maofisa
hao wakaagiza msafara urejeshwe kwenye ndege ili kurejea Tanzania , kwa
kuwa haukuwa na viza, hata hivyo wenyeji wa mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi,
wakafanya jitihada na kufanikiwa kumalizana na Maofisa hao wa Idara ya Uhamiaji.
Kufika katika hoteli
ya Florida
walipopangiwa kufikia, lilikuwa ni tatizo lingine, kwanza chakula kilikuwa
kichache na baadhi ya wachezaji walilala bila kula kabisa. Lakini kwa ujumla
mazingira ya hoteli hayakuwa yenye kuridhisha.
Hata hivyo, kwa mara
nyingine Katibu, Nassor akatumia busara kwa kukubali timu ilale hadi asubuhi na
kupatiwa na hoteli nyingine yenye hadhi, jambo ambalo wenyeji wao waliafiki na
kuomba radhi kwa usumbufu wote uliojitokeza.
Katika michuano hiyo,
Azam inatarajiwa kufungua dimba leo kwa kumenyana na Dragons kwenye Uwanja wa
Martyrs, saa 9:30 za huku, yaani saa 11:30 za nyumbani Tanzania .
Azam ambao ni washindi
wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na Ligi Kuu,
wamepangwa katika Kundi B pamoja na Dragons na Shark FC, ambayo watacheza nayo
Desemba 17.
Ikifuzu kwenye kundi
lake, Azam itaingia Nusu Fainali moja kwa moja, ambazo zitachezwa Desemba 25 na
Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu.
Kundi B, lina timu za DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na Real De
Kinshasa. Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa amesema wamekuja kushiriki
mashindano haya kwa lengo la kuwapa mazoezi na uzoefu wachezaji wake kabla ya
kuingia kwenye Kombe la Shirikisho mwakani.
Alisema Azam pia,
itatumia mashindano hayo kama fursa ya
kuwapima wachezaji wake kabla ya kuanza kwa Kombe la Shirikisho mwakani, ambako
wamepangwa kuanza na Al Nasr Juba ya Sudan Kusini.
Kikosi cha Azam
kilichowasili jana hapa, ukiondoa waliozuiwa Nairobi ni; Mwadini Ally, Jackson
Wandwi, Gaudence Mwaikimba, Himidi Mao, Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz, Luckson
Kakolaki, Samir Hajji Nuhu, Zahoro Pazi, Seif Abdallah, Malika Ndeule, Omar
Mtaki, Abdi Kassim, Uhuru Suleiman, Brian Umony na David Mwantika.
Wachezaji wengine
ambao hawahusiki katika safari hiyo, ni wale waliopo kwenye kikosi cha timu ya
taifa, Khamis Mcha ‘Vialli’, John Bocco ‘Adebayor’ na Salum Abubakar. Wachezaji
wapya, Joseph Mieno na Joackins Atudo kutoka wanaweza kujiunga na timu baadaye
mjini hapa.
Katika mchezo wa leo,
timu itaongozwa na kocha wa makipa, Iddi Abubakar Mwinchumu ambaye ni ‘Azam
Damu’, aliyeipandisha timu kutoka Daraja la Tatu hadi Ligi Kuu kwa kulinda
lango vema, huku John Bocco ‘Adebayor’ akitupia nyavuni.
No comments:
Post a Comment