Na Hafidh Kido
Mwenyekiti wa bodi ya
wakurugenzi gazeti la Raia Mwema Jenerali Ulimwengu, ametambuliwa rasmi kuwa
wakili nchini Tanzania
katika sherehe za 47 za kuwakubali na kuwasajili mawakili wapya.
Jenerali ambae kwa vipindi
tofauti amewahi kuwa mkuu wa wilaya, mbunge na mwandishi wa habari amekuwa
miongoni mwa mawakili wapya 618 waliokula kiapo mbele ya jaji mkuu Othman
Chande katika viwanja vya Law School of Tanzania jijini Dare s salaam jana.
Akizungumza katika ghafla
hiyo Jaji Chande, alisema kwa mwaka 2012 Tanzania imepata mawakili wapya 901
ingawa alieleza kwa viwango vya kimataifa ni idadi ndogo sana kwa nchi kubwa
kama Tanzania.
“Mwezi July tulipata mawakili
283, na leo tumepata wengine 618 hivyo kufanya jumla ya mawakili 901 kwa mwaka
huu wa 2012 kwa viwango vya kimataifa hii ni idadi ndogo sana hasa kwa nchi
kubwa kama hii, tunahitaji mawakili wengi zaidi kuweza kumaliza matatizo ya
kisheria yanayowakumba wananchi hasa mikoani,” alisema.
Hata hivyo jaji Chande
aliongeza mbali ya idadi kubwa ya mawakili wanaopatikana kila mwaka lakini
asilimia sabini (70%) ya mawakili wanaishia jijini Dar es alaam na kuacha idadi
ndogo sana
kuenda vijijini.
“Tanzania ina idadi ya watu
wanaokaribia milioni 50, asilimia 70 ya mawakili wote wamejazana hapa Dar es
Salaam, huko mikoani kuna uhaba mkubwa wa mawakili, kwa mfano Lindi kuna wakili
mmoja, Kigoma wapo wawili, Sumbawanga wapo wawili, Mara wapo wanne, Njombe wapo
watano, Tabora wapo sita, Tanga na Kagera wapo tisa na mikoa mipya ya Geita,
Simiyu na Katavi hakuna hata wakili mmoja,” Jaji Chande.
Miongoni mwa mawakili
waliosajiliwa siku hiyo ya jumatatu ni aliekuwa mwenyekiti wa umoja wa vijana
CCM mkoa wa Arusha Ole Milya ambae kwa sasa amehamia chama cha demokrasia na
maendeleo (chadema) amesema ataitumia elimu yake kukabiliana na migogoro ya
ardhi mkoani mwake.
Sherehe hizo za kuwakubali na
kuwasajili mawakili wapya zinafanyika mara mbili kwa mwaka ambapo tangu
zilipoanzishwa mwaka 1986 zimefanikiwa kuzalisha mawakili wengi nchini ambao
hata hivyo wameonekana kusongamana mijini na kusahau wananchi wa vijijini ambao
kwa hali halisi ndiwo wanaohitaji msaada wao mkubwa hasa kutatua migogoro ya
ardhi.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
18/12/2012
No comments:
Post a Comment