Tuesday, December 18, 2012

Zanzibar na historia inayokanganya...

 Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere alipotembelea kituo cha TVZ mwaka 1974 ambapo ilikuwa ni siku ya kumbukumbu ya miaka kumi ya mapinduzi. Zanzibar ndiyo ilikuwa nchi ya pili afrika kuwa na kituo cha TV ya rangi Afrika baada ya Afrika kusini.

Viongozi wa Zanzibar wakati wa uhuru mwaka 1963.

JE WAJUA? 

JANA ZANZIBAR ILIFANIKIWA KUWA MWANACHAMA WA UMOJA WA MATAIFA

Siku (Tarehe 16 Mwezi wa 12) miaka 49 iliyopita (mwaka 1963) Bendera ya lililokuwa Taifa la Zanzibar (sasa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania) na Bendera ya Jamhuri ya Kenya zilipandishwa Hewani katika Viwanja vya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani ikiwa ni ishara ya kutambulika Rasmi kwa Mataif
a hayo kama Wanachama wapya wa Umoja wa Mataifa.

Zanzibar ilipata Uhuru wake Disemba 10, mwaka 1963 chini ya Utawala wa Sultan kama Mkuu wa Nchi na Uongozi wa Shughuli za Serikali wa Waziri Mkuu Sheikh Mohammed Hamad Shamte wa Ushirikiano wa Vyama vya Zanzibar & Pemba Peoples Party (ZPPP) na Zanzibar Natiolist Party (ZNP) au "Hizbu" cha aliyekuwa Waziri wa Kwanza Mambo ya Nje wa Zanzibar Sheikh Ali Muhsin Barwany.

Balozi Hilal Mohammed Hilal Al-barwan aliteuliwa kuwa Balozi wa Kwanza wa Zanzibar katika Umoja wa Mataifa ambapo Disemba 16, 1993 Waziri Mkuu Mohammed Hamad Shamte alilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika Hotuba yake ya kuitambulisha Zanzibar kama Mwanachama Mpya wa Umoja wa Mataifa. 

Tarehe 17 Disemba, 1963 Balozi Hilal Mohammed Hilal Al-Barwan aliwasilisha Hati zake za Utambulisho kama Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana U Thant.

Serikali husika (iliyokabidhiwa Uhuru) ilidumu kukaa Madarakani kwa muda Mchache tu kabla ya kufanyika Mapinduzi yaliyoongozwa na Makomredi wa ASP na wale wa Chama cha Ummah Party kwa Msaada Mkubwa wa Serikali ya Chama cha Tanu ya iliyokuwa Nchi ya Tanganyika (sasa Tanzania Bara, ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania). 

Mapinduzi hayo yalimleta Madarakani Sheikh Abedi Amani Karume kama Rais Mpya wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika Serikali iliyoundwa kwa ubia wa Wanachama wa Chama cha ASP na wale wa Ummah Party cha Komredi Abdulrahman Mohammed Babu.

MCHAKATO ULIPOANZIA.

Mchakato wa Zanzibar kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa ulianza Mwaka 1960 ambapo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Dag Hamaskold aliitembelea Zanzibar Tarehe 6, Januari, mwaka 1960 wakati akielekea katika Ziara yake Maalum ya Kikazi Nchini Zaire (Sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo).

Pichani ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Dag Hamaskold akiwa pamoja na Viongozi Mbalimbali pamoja na Wajumbe wa Baraza la kutunga Sheria la Zanzibar (Legco) katika Viwanja vya Bustani ya Victoria huko Zanzibar wakati wa Ziara yake hiyo, ambapo Picha hii hutajwa kama Picha ya Mwisho ya Bwana Darg na jopo lake kabla ya Ndege yake kuanguka huko Rhodesia ya Kusini (sasa Zambia) wakati akielekea Zaire.

Wengine kwenye Picha waliosimama kutoka kushoto kwenda kulia ni Sheikh Dahman (Mjumbe Baraza la kutunga sheria, LEGCO kupitia chama cha ZNP), Sheikh Ali Sharif (Mjumbe Baraza la kutunga sheria, LEGCO kupitia Chama cha ASP), Bwana N.V.Patel (Mjumbe Baraza la kutunga sheria, LEGCO kupitia ASP), Bwana Master (Mjumbe katika Msafara wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa), Sheikh Rashid Al-Ghaithy (Mjumbe Baraza la kutunga sheria, LEGCO kupitia ZNP) na Sheikh Juma S. Al-Mugheiry (Karani wa Baraza la kutunga sheria, LEGCO).

Waliokaa kutoka Kushoto kwenda kulia ni Sheikh Juma Aley (Waziri kupitia Chama cha ZNP), Sheikh Abeid Amani Karume (Waziri kupitia ASP) Bwana Dag Hamaskold (Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa), Bwana Smithson (Waziri katika Serikali ya Uingereza), Bwana Kirk Madan (Katibu Mkuu Kiongozi), Bwana Hilal Mohammed Hilal Al-Barwani (Waziri, ZNP na Pia Balozi wa Kwanza wa Zanzibar Umoja wa Mataifa) na Sheikh Ameir Tajo (Waziri, ASP).

ZANZIBAR NA TANGANYIKA ZAPOTEZA UANACHAMA WAKE KATIKA UMOJA WA MATAIFA.

Tanganyika imekuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa tokea Disemba 14, mwaka 1961 mara baada ya kupata Uhuru wake tarehe 9 Disemba, mwaka 1961 kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza ambapo Dr. Vedastus Kyaruzi alikuwa Balozi wa Kwanza wa Tanganyika katika Umoja wa Mataifa akifuatiwa na Balozi A. Z. Nsilo Swai na kisha Chifu Erasto A. M. Mang'enya kuwa Balozi wa Mwisho wa Tanganyika katika Umoja wa Mataifa.

Mara baada ya Muungano wa Nchi za Tanganyika na Zanzibar Mwaka 1964 na kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nchi ya Zanzibar pamoja na Nchi ya Tanganyika zilipoteza Viti vyake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo kilitengwa kiti kipya kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiti ambacho kimeendelea kuwepo mpaka leo kikiiwakilisha Tanzania huko Umoja wa Mataifa.

Tarehe 19 Mwezi Novemba Mwaka 1964 Bwana John Samuel Cigwensisi Malecela aliteuliwa Kuwa Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Tanzania. Mabalozi wengine waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Mataifa ni Balozi Akil B.C. Daniel, Balozi Salim Ahmed Salim, Balozi Paul M. Rupia, Balozi Mohamed Ali Foum, Balozi Dr.Wilbert K. Chagula, Balozi Anthony B. Nyaki, Balozi Daudi N. Mwakawago, Balozi Dr.Augustine P. Mahiga, Balozi Ombeni Y. Sefue na huyu Mpya Balozi Tuvako Manongi.

CHANGAMOTO ZA MUUNGANO.

Miongoni mwa mambo ambaye yamekuwa yakiibuliwa kama moja ya malalamiko ya baadhi ya Wazanibari juu ya kero za Muungano ni ukweli kuwa Ushirikiano wa Kimataifa halikuwa katika moja ya Mambo yaliyokubalianwa katika Mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar (Kimsingi Mambo ya Nje ndio moja ya yaliyokubalianwa katika Mkataba wa Muungano).

Hivyo basi kuingizwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa katika Mambo ya Muungano kinyume na Makubaliano ya Muungano huonekana kama ni batili na sehemu ya kuiminya Zanzibar katika Muundo wa Muungano (ukitolewa Mfano kuwa katika Mabalozi wote waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Mataifa tokea Muungano Wawili tu ndo Wazanzibari na waliobaki wote ni Watanganyika).

Kwa kiasi flani hali hii (ya kuingizwa kinyemela kwa Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Mambo ya Muungano na kutokuwepo kwa uwiano wa kuridhisha wa Uteuzi wa Mabalozi wa Kudumu katika Chombo hiki kikuu cha Ushirikiano wa Kimataifa Duniani) inatumika kama moja ya sababu kuu za Msingi za wanaodai Zanzibar huru na kuvunja Muungano, lakini pia imekuwa Moja ya madai makuu ya wanaotaka kuendelea kwa Mashirikiano na Muungano wenye Utu na Heshima kati ya Tanganyika na Zanzibar kwa Kuboresha Muundo na kuondoa zile ambazo zinaonekana kuwa ni kero za Muungano.

Jambo hili ni zito na lina Mantiki makubwa katika mustakabali wetu kama Nchi, Kwa nafasi yetu kila mmoja ana wajibu wa kulitafakari hili na kuja na majibu ya msingi kulingana na uelewa wake, mifano kuntu na uzoefu juu ya hali hii kutoka katika Mataifa mbalimbali yenye Mashirikiano kama yetu.

Naamini Tutafanikiwa, Mungu Ibariki Tanzania.

Picha ni kwa Hisani kubwa ya Bwana Shafiq Sanya na Maelezo ni Kwa Hisani Kubwa ya Seif Abalhassan wa Watanzania Mashuhuri.

No comments:

Post a Comment