Ndugu
Wananchi,
Mtakumbuka kuwa hapo tarehe 23
Februari 2012 tuliwatangazia kupitia vyombo vya habari juu ya usitishwaji wa
matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia kwenda katika mfumo
mpya unaotumia teknolojia ya dijitali.
Napenda kuwaleleza kuwa, maandalizi ya
kuzima mitambo ya analojia kuanzia tarehe 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa
mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, napenda sasa kutoa taarifa
kuwa uzimaji wa mitambo ya analojia utafanyika kwa awamu kama
ifuatavyo:-
(1) Dar Es Salaam-31 Desemba, 2012;
(2) Dodoma & Tanga- 31 Januari, 2013;
(3) Mwanza-28 Februari, 2013;
(4) Moshi & Arusha-31 Machi, 2013;
(5) Mbeya-30 Aprili, 2013.
Tumeamua kuanza kuzima mitambo
hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa makampuni yenye
leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa mingine.
Makampuni haya yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo katika mikoa
minane katika miezi minane ijayo.
Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho
ni ile iliyopo Kisarawe na Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari
2013, vitapaswa kuanza kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV,
EATV, Channel 10, StarTV, DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN,
CloudsTV na Efatha.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
inafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za
kusambaza ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa
ili kukidhi mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora
unaokubalika.
Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa
wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa
wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi
watakuwa na matatizo na ving’amuzi.
Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya
nchi yetu. Tutakapokuwa tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na
utangazaji zitapanuka na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia
televisheni kupitia simu zetu za mikononi. Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu
kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na kutangaza
vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka, na
tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo
nchi yetu haiwezi kubaki nyuma.
Ndugu Wananchi,
Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania
itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu. Serikali inatarajia
kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na
wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa
televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya
teknolojia ya analojia.
Uhamaji huu hautahusu televisheni za
wananchi zinazopata matangazo kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya
(cables). Hivyo, wananchi wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo
wataendelea kupata matangazo yao kama kawaida.
Ndugu Wananchi
Ndugu Wananchi,
Nawashukuru kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment