Thursday, December 13, 2012

Tafsiri yangu tukio la Ray C na kikwete....


Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa pamoja na Ray C wa kwanza kushoto ni Mama yake mzazi Ray C Bibi Margareth Mtweve (kushoto) na kulia ni Sarah Mtweve Dada yake Ray C. Picha na mdau Freddy Maro wa Ikulu.

wiki iliyopita vyombo vya habari hasa mitandao ya kijamii vilijaa picha za mwanamuziki Rehema Chalamila maarufu Ray C, akiwa amepeana mkono na Rais Jakaya Kikwete akimshukuru kwa kuamua kusimamia matibabu yake.

Siku ya jana nikaona picha nyingine Rais Kikwete akiwa amepeana mkono na waandishi wa habari, namna inavyoonekana ni kuwa walipanga msitari ili kupata picha na Rais wakiwa wamepeana nae mkono. Ni baada ya mkutano na waharirir katika ukumbi wa mkutano ndipo likafuata zoezi hili la kupiga picha na rais wakiwa wamepena mkono.

Ni utamaduni wa waafrika kupeana mkono kwa lengo la salamu ama kushukuru, sijakuwepo na ndiyo maana nikaiita ni dhana maana niliona picha za waandishi wawili wakiwa wamepiga picha zinazofanana, ikimaanisha walikuwepo wengine wakisubiri zamu yao ya kupeana mkono na Rais. Lakini mpaka sasa sijapata kuona habari yoyote kuhusu picha zile kuhusu aina ya shukurani waandishi wale walikuwa wakitoa kwa Rais, ama ni Rais ndie aliekuwa akiwashukuru.

Hii kitaalamu katika masuala ya mawasiliano na mahusiana tunaita kujenga mahusiana ama waingereza wanaita 'rapport'. nchi inayotimiza miaka zaidi ya 50 bila kuwashinda maadui watatu maradhi, ujinga na umaskini, hatuna muda wa kushikana mkono na Rais ili tupige picha. tunataka matendo yatakayotufanya tumpe mkono wenyewe tena mkono wa shukurani kama alivyofanya Ray C. 

leo asubuhi wakati nikielekea ofisini, katika daladala nilikutana na vijana wenzangu wawili ambao kwa muonekano tu ni watumiaji wa dawa za kulevya, alikuwa dada na kaka mmoja. afya zao zinaonekana kuanza kuimarika nadhani wapo katika mchakato wa kuacha dawa hizo. Maana niliona wakizungumzia kuhusu dawa ya Methadon ambayo huwasaidia kuacha kutumia dawa za kulevya.

Vipo vituo vingi hapa nchini vina uhaba wa dawa hiyo ya Methadon, sijui Serikali inatilia nguvu vipi upatikanaji wa dawa hii na kuwatembelea wagonjwa ambao wapo katika vituo maalum 'rehab' ambao wanakutana na changamoto za lishe duni na ukosefu wa ajira zitakazowawezesha kuenda mbio siku nzima ili wasipate muda wa kukaa na magenge hatarishi.

Natamani siku moja wajitokeze kina Ray C 1000 (elf moja) wapige picha na Rais wakiwa wanatabasamu kwa msaada waliopatiwa juu ya namna ya kuachana na dawa za kulevya.

Naomba leo niishie hapa...

Hafidh Kido
Dar es Salaam, Tanzania 

No comments:

Post a Comment