Thursday, December 6, 2012

Leo ndiyo leo Tanzania na Uganda uwanja wa Namboole Nusu fainali...

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
TANZANIA Bara, Kilimanjaro Stars leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa kumenyana na wenyeji, Uganda, The Cranes katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kuanzia saa 12:00 jioni.
Mchezo huo, utatanguliwa na mechi nyingine ya hatua hiyo kati ya Zanzibar na Kenya, ambayo, itaanza saa 10:00 jioni.     
Hii inakuwa mara ya pili mfululizo, Bara kukutana na Uganda katika Nusu Fainali ya michuano hii, kwani hata mwaka jana pia mjini Dar es Salaam, zilikutana katika hatua hiyo, Desemba 8, Uwanja wa Taifa.
Katika mchezo huo, wenyeji wakiwa chini ya makocha wazalendo, walichapwa mabao 3-1 ndani ya dakika 120, Stars ikitangulia kupata bao mapema tu dakika ya 18, mfungaji Mrisho Khalfan Ngassa, lakini Nahodha wa The Cranes  Andy Mwesigwa akasawazisha dakika ya 56.
Mchezo ulipohamia katika dakika za nyongeza, Uganda walipata mabao mawili na kuwamaliza wenyeji, wafungaji Emmanuel Okwi dakika ya 102 na Isaac Isinde dakika ya  111 kwa penalti.
Kocha wa Stars, Mdenmark Kim Poulsen ametahadharisha wanataka uchezeshaji wa haki kutoka kwa refa Mohamed El Fadil wa Sudan, ambaye pia aliwachezesha katika mechi dhidi ya Rwanda Robo Fainali.
“Vijana wamejiandaa vizuri kabisa na wote wako katika hali nzuri ya kucheza ila tunachoomba ni uchezeshaji wa haki kutoka kwa refa, maana tunacheza na wenyeji ambao wana watazamaji wengi,” alisema.
Poulsen alisema timu zote mbili ni nzuri na iwapo muamuzi atachezesha vizuri basi utakuwa ni mchuano mkali. “Vijana wana ari na mchezo huu na tukipewa haki tutacheza vizuri kama tulivyofanya katika michezo dhidi ya Rwanda,” alisema Poulsen.
Kuhusu hali ya timu, Mdenmark huyo alisema hana majeruhi hata mmoja na pia aliwasifu wachezaji wake kwa kuonyesha umoja na nidahmmu ya hali ya juu. “Hawa wanakaa kama familia, si unawaona walivyo pamoja?” alisema Poulsen na kuongeza kuwa hilo ni muhimu sana kwa mchezaji.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Stars, Sylvester Marsh amesema kama Uganda waliwafunga Tanzania Dar es Salaam mwaka jana, basi na wao watawafunga Kampala mwaka huu.
Kocha wa Uganda, The Cranes, Msoctland, Bobby Williamson alisema kwamba Stars ni timu nzuri, lakini haina uwezo wa kuifunga timu yake.
“Wana wachezaji wazuri, wenye vipaji, lakini bado timu yangu ni nzuri katika mashindano haya, tutawafunga,”alisema.
Safu ya ushambuliaji ya Stars leo inatarajiwa kuongozwa na Mrisho Khalfan Ngassa na John Raphael Bocco ‘Adebayor’ ambao wanaongoza kwa mabao katika mashindano haya, kila mmoja akiwa na mabao matano.
Uimara zaidi wa Stars upo katika safu ya kiungo, ambako kuna watu mahiri kama Frank Domayo, Amri Kiemba, Salum Abubakar na Mwinyi Kazimoto.
Stars pia inajivunia safu imara ya ulinzi, chini ya Nahodha, kipa Juma Kaseja, mabeki Erasto Nyoni, Amir Maftah, Kevin Yondan na Shomary Kapombe ambao wameruhusu bao moja tu katika mechi nne zilizopita, tena la penalti, dhidi ya Burundi.
Bocco, aliyeimarika zaidi kiuchezaji, mwenye nguvu, anayeenda hewani na kuambaa vema na mpira, atasimama mbele ya mdomo wa goli la Korongo wa Kampala, wakati Ngassa atakuwa akishambulia kutokea pembeni.
Domayo, Kiemba na Sure Boy watakuwa wote wakikaba kwa bidii, wakati Kazimoto atakuwa akiiendesha timu, zaidi ya kuwatengenezea nafasi za kufunga Bocco na Ngassa.
Kiemba amekuwa akitumia mwanya wa timu kufanya mashambulizi ya kushitukiza kupanda kusaidia na ndiyo maana aliwafunga Rwanda, jambo ambalo linatarajiwa na leo pia.
Kazimoto mwenye mashuti makali hajafunga hata bao moja katika mechi nne zilizopita, lakini matarajio ya wengi atatikisa nyavu kuanzia leo baada ya kuizoea zaidi hali ya Kampala.
Uganda nao wana ukuta sugu, ambao haujaruhusu hata bao moja hadi sasa, ikiongozwa na kipa Hamza Muwonge, mabeki Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi na Isaac isinde, wakati safu ya kiungo ya kiungo inatarajiwa kuongozwa na Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito na Moses Oloya.
Safu ya ushambuliaji leo bila shaka dhamana watapewa, Robert Ssentongo, Hamisi Kiiza na Brian Umony, wakati Emmanuel Okwi anaweza kuanzia benchi tena. Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mkali, Uganda wakicheza mbele ya malefu ya mashabiki wao na Bara wakijaribu kulipa cha Dar es Salaam  mwaka jana. 
Timu hizi zimekutana mara 12 katika Challenge tangu mwaka 1975, kila timu ikishinda mechi tano, sare mbili na Bara imefunga mabao 16, wakati imefungwa mabao 17.
Uganda; Hamza Muwonge, Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi, Henry Kalungi, Isaac Isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito, Moses Oloya, Robert Ssentongo, Hamisi Kiiza na Brian Umony.
Tanzania; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Franko Domayo, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto, John Bocco na Mrisho Ngassa.  
Mungu zibariki timu zetu, Bara na Zanziabr leo, ibariki Tanzania. Amin.

MATOKEO YA JUMLA STARS NA CRANES TANGU 1975:
                     P    W  D   L    GF GA      Pts
Uganda         12 5    2    5    17 16       17
Tanzania       12 5    2    5    16 17       17

REKODI YA STARS NA CRANES CHALLENGE TANGU 1974:
Desemba 8, 2011; Nusu Fainali, Dar es Salaam
Uganda 3–1 Tanzania (dakika 120)
Januari 9, 2009; Kundi A Uganda
Tanzania 1-2 Uganda
Desemba 11, 2001; Kundi B Rwanda
Tanzania 1-0 Uganda
Desemba 1, 1995; Kundi B Uganda
Tanzania 2-1 Uganda B
Desemba 10, 1994; Fainali Kenya
Tanzania 2-2 Uganda: (Tanzania ilishinda kwa penalti 4-3)
Desemba 10, 1992; Fainali Mwanza
Tanzania B(Kakakuona) 0-1 Uganda
Desemba 17, 1990; Nusu Fainali Zanzibar
Tanzania 1-1 Uganda (dakika 120, Uganda ilishinda penalti 6-5)
Desemba 1, 1984; Kundi A Uganda
Tanzania 1-1 Uganda
Novemba 20, 1983; Kundi A Kenya
Tanzania 1-1 Uganda
Novemba 17, 1982; Kundi A Uganda
Tanzania 0-1 Uganda
Novemba 9, 1979; Kundi A Kenya
Tanzania 5-3 Uganda
Desemba 10, 1974; Fainali Dar es Salaam                                    
Tanzania 1-1 Uganda (Tanzania ilishinda kwa penalti 5-3)
Chanzo: Bin Zubeir blog...

No comments:

Post a Comment