Saturday, December 22, 2012

Hivi ndivyo Lema alivyoshinda rufaa yake.. jana mahakama ya rufani jijini.

Mbunge wa Ubungo John Mnyika katikati akifurahia jambo na Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema kulia jana wakati wa maandamano ya kuelekea makao makuu ya chadema Kinondoni wakitokea mahakama ya rufani mjini.



MAHAKAMA ya Rufani imemrejesha bungeni Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ikiwa ni miezi tisa tangu alipovuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Mahakama hiyo ilimrejesha Lema bungeni, baada ya kushinda rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Arusha iliyotolewa Aprili 5, mwaka huu.
Hukumu hiyo iliyosomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu imemtambua Lema kuwa mbunge halali wa Arusha Mjini na kuwaamuru wajibu rufaa kumlipa gharama za rufaa hiyo.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Bernard Luanda kwa niaba ya wenzake wawili waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa wajibu rufani hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi.
“Rufaa imefanikiwa na tunatengua hukumu, tuzo na amri  ya Mahakama Kuu. Tunamtangaza mrufani kuwa Mbunge wa Arusha Mjini,” ilisema Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo.
Uamuzi huo uliwafanya wanachama na wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika ndani ya ukumbi wa Mahakama hiyo, kulipuka kwa furaha huku wakiimba kibwagizo cha “People’s Power!” na wengine wakiongeza kwa kuimba “Lema! Lema! Lema!”
Wanachama na wafuasi hao wa Chadema walianza kusukumana kwenda kumkumbatia Lema, huku wengine wakipanda kwenye viti (mabenchi) ya mahakamani.
Tukio hilo lilisababisha taharuki kutokana na kusukumana, huku wengine wakianguka kwenye mabenchi, hali ambayo pia iliwapa wakati mgumu viongozi wa Chadema akiwamo, Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kutoka nje ya ukumbi huo.

Hoja mpya
Katika rufaa yake, Lema kupitia kwa mawakili wake, aliwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, lakini katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani iliibua na kutolea uamuzi hoja mpya ambayo haikuwa imetolewa na upande wowote mahakamani hapo.
Hoja hiyo ambayo iliibuka kwa mara ya kwanza kabisa siku ya kusikiliza rufaa hiyo ni kama warufani walikuwa ni wapiga kura waliojiandikisha.  
Katika uamuzi wake kuhusu hoja hiyo, Mahakama ilisema kuwa wajibu rufaa hao, hawakuwa wapiga kura kwa kuwa katika kumbukumbu za Mahakama hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa ni wapiga kura waliosajiliwa.
Mahakama ilipoibua hoja hiyo, Wakili wa warufani, Mughway alijibu kuwa wajibu rufaa hao ni wapiga kura halali waliosajiliwa na kwamba hata Mahakama ilijiridhisha kwa kuangalia kadi zao za kupigia kura.
Wakili Mughaway alidai kuwa suala hilo lilijitokeza Mahakama Kuu na wajibu rufaa hao wakawasilisha kadi zao mahakamani ambazo ilinakili majina na namba zao na kisha kuzirejesha kwa wenyewe.
Lakini Wakili wa Lema alidai kuwa hata kama kadi hizo ziliwasilishwa mahakamani, utaratibu ambao ulitumika haukuwa wa kisheria, akidai kwamba zilipaswa ziwasilishwe kama vielelezo vya ushahidi na si jaji kuziangalia na kisha kuzirejesha kwa wahusika.
Katika hukumu yake jana, Mahakama ya Rufani ilikubaliana na hoja za mawakili wa warufani, ikisema kumbukumbu za Mahakama hazionyeshi mahali ambako kadi hizo zimepokewa mahakamani kama vielelezo vya ushahidi.
Mahakama ilisema kwamba kinachoonekana katika kumbukumbu za Mahakama ni kiambatisho na maelezo tu kuwa wajibu rufani ni wapiga kura waliosajiliwa na kwamba badala yake wakili wao ndiye aliyejaribu kuthibitisha hilo kwa maelezo, badala ya vielelezo.
“Katika kesi hii, Wakili Alute (Mghway) aliwasilisha kadi za wajibu rufaa kwa Jaji (Aloyce Mujuluzi) kuthibitisha kuwa wajibu rufaa walikuwa wapiga kura halali,” ilisema Mahakama katika hukumu yake hiyo.
Mahakama hiyo ilisema utaratibu huo ni kinyume cha sheria kwa kuwa ushahidi kama huo ulipaswa uwasilishwe moja kwa moja mahakamani na utolewe na mmiliki wa nyaraka hizo.
Pia Mahakama hiyo ilisema kumbukumbu hizo hazionyeshi kama mrufani alipewa fursa ya kuzungumza lolote kuhusiana na utaratibu huo wa kuwasilisha hati hizo.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilisema kuwa hata kama ingethibitika kuwa wajibu rufani walikuwa wapiga kura waliosajiliwa, bado hawakuwa na haki kisheria kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi kwa madai ya mrufani kutumia lugha za matusi kwenye kampeni zake.
Ilisema kwa kuwa kisheria hayo ni maslahi ya umma kufikishwa mahakamani chini ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba, kanuni ya haki ya kisheria kufungua kesi ni kwamba mlalamikaji anapaswa kuonyesha haki zake au maslahi ambayo yameingiliwa na athari alizozipata.
“Hivyo mpiga kura hana haki ya kisheria kufungua kesi kuhoji matokeo ya uchaguzi pale ambako haki zake hazikukiukwa,” ilisema Mahakama ya Rufani.
Ilisema kwa mujibu wa Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya Tanzania, raia anakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi kwa maslahi ya jamii, kama ilivyotokea katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 1995.
Mahakama ilisema kuwa shauri hilo halikufunguliwa chini ya Ibara ya 26 (2) ambayo inampa fursa na haki raia yeyote kufungua shauri mahakamani lenye maslahi ya umma, huku ikisisitiza kuwa madai ya wajibu rufani katika kesi hiyo hayagusi maslahi ya jamii yote.
Katika hoja hiyo, Wakili wa wajibu rufani, Mughway alitumia kesi ya William Bakari na mwenzake dhidi ya  Chediel Mgonja na AG, namba 84 ya mwaka 1980.
Katika kesi hiyo Mahakama Kuu iliamua kuwa inapothibitika kuwa mpiga kura amejiandikisha ana haki ya kufungua kesi kupinga matokeo.
Mahakama ya Rufaa ilisema kwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu katika kesi hiyo ina maana kuwa mpiga kura ana haki zisizo na mpaka kufungua kesi hata kama haki zake hazijakiukwa kwa namna yoyote.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa Mahakama Kuu katika kesi hiyo iliamua kwa makosa na kwamba haidhani kuwa sheria haikukusudia kusema kuwa mtu yeyote bila kujali mahali alipojiandikisha na kupiga kura anaweza kupinga matokeo katika jimbo lolote nchini.
Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake ilisisitiza kuwa katika kesi kama hiyo ilikuwa ni wajibu wa yule tu ambaye anaona haki zake zilikiukwa.
Kutokana na kuamua hoja ya kwamba mpiga kura hana haki ya kufungua kesi, mahakama haikushughulika na hoja nyingine zilizowasilishwa na warufani, wala rufaa iliyofunguliwa na wajibu rufaa.
Chanzo: Mwananchi
</

No comments:

Post a Comment