Na: Raymond Kaminyoge Dar na Joseph
Lyimo, Simanjiro
WAKATI
Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), likihaha kumtafuta aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema akiwa amevaa sare za jeshi hilo ,
mtu huyo ameibuka na kusema yuko tayari kufukuzwa kazi kuliko kuacha
kuishabikia Chadema.
Kauli hiyo ya JWTZ imekuja baada ya jana, gazeti hili
kuchapisha picha ya mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa JWTZ akiwa
amepiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari,
huku akiwa amenyoosha vidole viwili alama inayotumiwa na Chadema.
Baada ya taarifa hiyo, JWTZ lilitoa taarifa likieleza
kushtushwa na tukio hilo na kusema kwamba
linamtafuta mtu huyo kwa udi na uvumba ili kujiridhisha kama
kweli ni askari wake.
‘‘Kimsingi Jeshi linafanya uchunguzi wa kumtambua mtu huyo
kama kweli ni askari,’’ ilisema sehemu ya taarifa ya Kurugenzi ya Habari na
Uhusiano ya jeshi hilo ambayo iliyatilia shaka
mavazi aliyokuwa amevaa mtu huyo kama ndiyo yanayotumiwa na jeshi hilo sasa.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema ingekuwa rahisi kumtambua mtu
huyo kwa kuangalia paji la uso lakini alilifunika ili asitambulike.
‘‘Pamoja na hayo, jeshi linamtafuta ili kumchukulia hatua za
kinidhamu kutokana Kanuni za Majeshi ya Ulinzi likisema Sheria namba Nne ya
Mabadiliko ya Nane katika Katiba ya Nchi ya mwaka 1992, Ibara ya 147(3),
mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa,’’ ilisema taarifa
hiyo.
Mbali ya taarifa hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala
Mgawe alisema endapo itabainika kuwa aliyevaa sare hizo ni mwanajeshi, moja ya
hatua dhidi yake ni kufukuzwa kazi mara moja.
Mbali na hatua hiyo, Kanali Mgawe alisema kuanzia sasa, Jeshi
limepiga marufuku mtu yeyote kuvaa sare zake katika mikutano yote ya siasa na
atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Kuhusu kitendo cha askari huyo kupiga picha na Lema, Kanali
Mgawe alisema moja ya masharti muhimu ya askari anapiojiunga na jeshi ni
kutambua na kutii sheria inayomzuia kujihusisha na masuala ya siasa na kwamba
kitendo cha mtu huyo kimemshangaza na kumfanya amtilie shaka kama kweli ni
askari aliyekamilika.
Msimamo wa mtuhumiwa
Kwa upande wake, mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa
Kikosi cha Chuo cha Mafunzo Monduli (TMA), mkoani Arusha, alisema ni bora
afukuzwe kazi kuliko kunyimwa kujiunga na Chadema.
Akizungumza jana kwa sharti la kutotajwa jina akiwa Mirerani,
Simanjiro mtu huyo alisema Chadema ni chama makini chenye uwezo wa kuongoza
nchi kwani kinatetea wanyonge na kujali masilahi ya jamii.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment