JESHI la
Polisi limetoa siku saba kwa baadhi ya askari kuzisalimisha fedha
zipatazo sh milioni 150 wanazodaiwa kuiba, ambazo zilizoporwa na majambazi Mtaa
wa Mahiwa na Livingston jijini Dar es
Salaam juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini, Kamanda wa Polisi
wa Kanda Maalum, Suleiman Kova, alisema kutokana na tuhuma hizo jeshi hilo limeunda Jopo la
wapelelezi ili kujua ukweli wa madai hayo.
Alisema Jopo hilo
litaundwa na watu watano, likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum, Ahmed
Msangi, atakayehakikisha kwamba muda mfupi inavyowezekana, ukweli upatikane ili
wananchi wajulishwe matokeo.
Kamanda Kova alisema jeshi hilo lina mfumo wake wa kuchunguza askari
wake inapotokea amejihusisha katika matukio yanayokwenda kinyume na maadili ya
kazi yake.
Alisema tukio hilo
halikubaliki hivyo kila aliyepewa jukumu la kulifuatilia ni lazima ahakikishe
kuwa anafanya kazi kwa ufasaha ili majibu yapatikane haraka kuondoa shaka shaka
kwa wanachi.
Kova alimtahadharisha Msangi kuwa, endapo atashindwa kutoa
majibu ya kuridhisha basi atambue hata yeye itabidi awajibike ambapo alisema
vitu kama hivi vikiachwa viendelee vinaliletea jeshi hilo sifa mbaya na kupoteza imani kwa
wananchi.
“Pamoja na kumkabidhi kazi hiyo Msangi lakini hata mimi
sitakaa kimya bali nitalifuatilia kwa karibu ili mradi tuwapatie wananchi
ukweli”alisema Kova.
Alibainisha kuwa hawezi kupinga kama askari wanaweza
kushiriki katika vitendo hivyo viovu bali suala hilo bado linahitaji ushahidi zaidi hivyo, ni
vema wananchi wenye ushahidi wakatoa ushirikiano utakaosaidia kupatikana fedha
hizo.
Aidha, Kova alilitaka jeshi la polisi kufanya kazi zake kwa
nidhamu, uaminifu na ueledi kwani endapo ofisa au askari atakiuka maadili ya
kazi yake, basi hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi yake bila kuchelewa.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza jopo hilo linaundwa na polisi wenyewe bila
kushirikisha wadau wengine kwa madai kuwa, eti lifanya kazi kwa kutii sheria
zote bila kwenda kinyume.
Chanzo:
Mjengwa blog
No comments:
Post a Comment