Sunday, December 30, 2012

Mwili wa mwanamke aliedhalilishwa na kufariki wawasili India...


NEW DELHI, India
MWILI wa mwanamke wa India ambaye amefariki hospitalini nchini Singapore baada ya kubakwa kinyama mjini New Delhi umerejeshwa nchini humo kwa ndege maalumu ya kukodi.
Balozi  wa  India  nchini  Singapore, T.C.A Raghavan  aliwaambia waandishi wa habari jana, saa  kadhaa baada  ya  mwanamke  huyo kufariki kutokana  na  viungo  vyake  kushindwa kufanya  kazi katika hospitali nchini Singapore  ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Mwanamke huyo na ndugu wa marehemu walisafirishwa kwenda India katika ndege maalumu ya  kukodi  mchana wa  jana Jumamosi, kwa mujibu wa Raghavan.
Waziri  Mkuu wa India,  Manmohan Singh alisema kuwa amesikitishwa sana na kifo cha mwanamke  huyo  ambaye alifanyiwa  vitendo  vya  kinyama  kwa kubakwa  na kundi  la  vijana na kwamba  maandamano  yaliyozuka  kutokana na kitendo  hicho “yanaeleweka”.
“Nimesikitishwa  mno  kufahamu  kuwa mwathirika huyo wa mashambulizi ya kinyama yaliyofanyika  Desemba 16 mjini New Delhi ameshindwa kunusurika kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata baada ya shambulio dhidi yake, “ aliandika waziri  huyo mkuu katika tovuti yake.
“Tumeshaona hisia na nguvu ambazo tukio hili limesababisha. Hii ni hali ambayo inaeleweka kutoka  kwa vijana wa India  ambao wanataka mabadiliko ya kweli.
“Nataka  kuwaambia, familia yake na taifa  kwa jumla kuwa amepoteza maisha, ni juu yetu wote kuhakikisha kuwa kifo chake hakitakuwa cha bure.”
India imetikiswa na maandamano makubwa tangu msichana huyo mwenye umri wa miaka 23 aliposhambuliwa kinyama  katika basi mjini New Delhi na kundi la watu sita.
Serikali imekuwa ikijaribu kulituliza wimbi  la hasira kwa  kuahidi adhabu kali kwa uhalifu mkubwa unaohusiana na  ngono pamoja na kuunda tume maalumu ya uchunguzi kuhusiana  na jinsi ya kushughulikia kesi za ubakaji.
Wakati maofisa wakijitayarisha kwa ghasia zaidi mitaani, polisi waliongezwa katika eneo la kati la mji mkuu wa India kabla ya mwili wa msichana huyo kurejeshwa  nchini  humo jana.
Ofisa wa polisi wa mjini New Delhi, alihimiza watu kuomboleza  kifo cha  mwanamke  huyo kwa  amani  wakati  maeneo  kadha  ya  mji  huo mkuu  yamefungwa.
Singh, ambaye  hapo  kabla  alitoa  wito wa  utulivu , alisema kuwa  itakuwa, “Heshima  kubwa  kwa  kumbukumbu  yake  iwapo tutaweza  kuelekeza  hisia zetu hizi  na  nguvu  katika  kuchukua hatua  sahihi. Kwa muda huu tunahitaji mjadala wa maana na uchunguzi kuhusiana na mabadiliko ya lazima  na haraka ambayo yanahitajika katika mtazamo wa jamii.
“Ni  matumaini  yangu  kuwa  tabaka  lote  la  kisiasa  pamoja  na jamii yote  itatenga maslahi yao  finyu ya binafsi na ajenda  ili kutusaidia  kufikia hatima  ambayo tunaikusudia, na kuifanya  India kuwa mahali bora na salama  kwa wanawake kuweza  kuishi.

No comments:

Post a Comment