Thursday, December 20, 2012

Kiwanja cha mil 70 chauzwa kwa mil 9 na mbunge wa Tanga Omar Nundu

 Hapa nikiwa na mkaazi wa Mwakidila akinionyesha kiwanja chenyewe kilichouzwa badala ya kujengwa Hospitali.

 Kwa wakaazi wa Tanga kama hawaamini wanaweza kuenda kuuliza wakaazi wa eneo hilo. Huu ni msikiti wa mwakidila, kiwanja kipo nyuma ya msikiti huu.

                  Hapa sasa ni masiwani shamba, ndipo panapojengwa hospitali hii ya wilaya Tanga mjini.

                                                           Kiwanja cha masiwani shamba.

Ujenzi ukiendelea masiwani shamba, nadhani kwa sasa watakuwa wamepiga hatua maana tangu mwezi wa sita mwaka huu nilipopiga picha hii sijajaaliwa kupitia tena maeneo haya.
Na Hafidh Kido

Jinamizi linazidi kumwandama aliekuwa waziri wa uchukuzi ambae pia ni mbunge wa Tanga mjini Omar Nundu, mbali ya kutimuliwa uwaziri, miezi kadha iliyopita kushutumiwa na waziri mpya wa uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe kwa kumrudisha kazini kaimu mkurugenzi mtendaji wa ATCL Paul Chizi bila ya kufuata taratibu sasa anakabiliwa na tuhuma mpya za kuhusika na uuzwaji wa kiwanja cha ekari 17 mali ya jiji la Tanga kwa bei chee.

Akizungumza na kidojembe mkazi wa Tanga ambae hakutaka jina lake litajwe humu alisema eneo hilo linalopatikana sehemu za Mwakidili njia ya kwenda Pangani lilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya Wilaya lakini baada ya kutokea mivutano baina ya viongozi wa jiji hatimae ujenzi ulihamia maeneo ya Masiwani Shamba pembeni kidogo ya Mwakidila.

Taarifa tulizozipata baada ya timu ya kidojembe kukaa jijini Tanga kwa wiki nzima zinaonyesha kuwa utaratibu uliotumika kuhamisha ujenzi huo kutoka Mwakidila kuenda Masiwani Shamba sambamba na kuuzwa eneo hilo kwa wazungu kutoka Italy kwa bei chee, kumesababishwa na chuki za kisiasa na kulipizana visasi baada ya Mbunge huyo wa Tanga kukosa kura katika kata ya Mwakidila ambapo ndipo alipozaliwa na kukulia tangu akiwa mdogo.

Akizungumza na mwandishi wetu mmoja wa wazee wa Mwakidila Zaid Mbasha ambae anadai Mheshimiwa Nundu baada ya kupata kura tano tu kutoka Mwakidila aliapa kumshughulikia na kuhakikisha hapati kazi katika mkoa huo na wakazi wa Mwakidila watakiona cha moto kwa kumnyima kura.

“Mimi shughuli zangu ni ujenzi, ninapata ‘tenda’ nyingi kutoka halmashauri za kujenga vyumba vya madarasa, zahanati na vituo vingi vya maendeleo ya jiji la Tanga. Lakini tangu Nundu aingie madarakani sijawahi kupata ‘tenda’ hata ya kujenga choo, lakini sioni ajabu kwani alishanitamkia kuwa atahakikisha ananishughulikia kwani nilionekana ni kinara wa kumkataa.

“Mimi ni mwana CCM damu na Nundu namfahamu tangu akiwa shule, ni mbinafsi na ana roho mbaya; watu wa Mwakidila wanamfahamu na chaguo letu lilikuwa ni Salim Kisauji, ambae alikuwa Meya wa Tanga hivyo katika kura za maoni Nundu alipata kura tano tu katika kata ya Mwakidila hivyo alitutamkia wazi kuwa atatufanyia kitu kibaya sana ambacho hatutokisahau,” alisema mzee Mbasha.

Mzee Mbasha aliendelea kueleza kuwa wakati Mheshimiwa Nundu anaingia madarakani mwaka 2010 alikuta suala la ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Tanga itajengwa kata ya Mwakidila, kwa maelezo ya Mzee huyo inadaiwa Nundu kwa kushirikiana na Mstahiki Meya wa jiji la Tanga Omar Guledi, walihakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unahamishiwa Masiwani Shamba kata ya Tanga sisi ili kutekeleza ile ahadi yake ya kuwaonyesha cha moto baada ya kuwanyima kura.

“Hili suala la hospitali kujengwa Mwakidila lilishakwisha kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010 na Nundu amekuta watu waliotoa maeneo yao walishalipwa fidia tangu mwaka 2008, aliona hospitali ikijengwa hapa sisi tutafaidika iweje mbunge anakuwa na mamlaka ya kubatilisha maamuzi ya baraza la madiwani ambao walishapitisha katika ‘full council’ kuwa hospitali ijengwe hapa? Hapa kunanukia harufu ya rushwa na maamuzi ya chuki. Ninachotaka kukwambia mwanangu watu wa kata ya Mwakidila na Mwaminji hatuitaki tena serikali ya CCM, kadi zetu bado tunazo lakini uchaguzi wa mwaka huu wa CCM wananchi wa Mwakidila na Mwaminji hatujapiga kura hatuitaki CCM tumechoka na manyanyaso” alieleza kwa masikitiko mzee Mbasha.    

Mwandishi alitembelea eneo la Masiwani Shamba ambako alikuta ujenzi wa hospitali unaendelea, wakazi wa eneo hilo wakiwakilishwa na mzee Salim Juma wanaonekana kufurahia ushindi huo baada ya mvutano wa takriban miaka sita juu ya wapi hospitali ijengwe.

“Huu ni ushindi kwetu na inadhihirisha ni kiasi gani Rais wetu ni msikivu, nilimwandikia barua Rais Kikwete kumueleza juu ya matatizo haya ya kuporwa haki yetu ya eneo la Masiwani Shamba kupata bahati ya kujengwa hospitali ya wilaya. Hatukuomba bali wenyewe watu wa halmashauri walipendekeza na kwa kuthibitisha Meya Kisauji alitamka hivyo mwaka 2007 siku Rais alipotembelea mkoa wetu iweje leo anaturuka?,” alihoji mzee Salim.

Alipoulizwa na mwandishi juu ya upatikanaji wa maji, umeme na barabara katika eneo la ujenzi mzee Salim alijibu “hatuna maji wala umeme na barabara ni kama unavyoona haipitiki ila kikubwa tunachoamini hii itasaidia mji kupanuka na hayo yatafanyika kidogokidogo.”

Nae diwani wa kata ya Mwanzange kwa tiketi ya chama cha CUF Rashid Jumbe, aliiambia kidojembe kuwa anashangazwa na kinachotokea kwani yeye alikuwapo tangu baraza la mwaka 2005, na yeye alishiriki kikao kilichopitisha eneo la Mwakidila kutumika kwa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Tanga.

“Nilikuwepo katika kikao hicho kilichopitisha eneo la Mwakidila na mchakato huu ulikuwa chini ya kamati ya afya ya wilaya na wataalamu wa ardhi ndiwo waliozunguka kila eneo kuhakikisha wanapata eneo zuri na la uhakika kwa ujenzi, hata sijui ni nini kilichotokea mpaka Mstahiki Meya Guledi kubadilisha maamuzi hayo na kuamua ujenzi ufanyike Masiwani Shamba,” Rashid Jumbe.

Mwandishi alipomuuliza diwani huyo juu ya taarifa za maamuzi ya kubadilisha eneo la ujenzi kupitishwa na baraza la madiwani Januari mwaka 2011, alisema “ni kweli baraza lilipitisha maamuzi hayo lakini kile kikao hakikuwa na baraka zote kwani kilikuwa batili kwa mujibu wa sheria. Maamuzi lazima yafanywe na wajumbe wanaofikia theluthi mbili.

“Madiwani wa CCM hawafikii theluthi mbili na sisi wa upinzani tulitoka nje ya kikao kupinga maamuzi yao . Sasa iweje waseme madiwani ndiwo walioamua hayo labda iwe ni madiwani wa CCM pekee lakini hili suala si la kichama ni suala linalohusu maendeleo ya Tanga lazima watu wawe makini katika hili,” alisisitiza Jumbe.

Alipoulizwa huhusu Mbunge wa Tanga Omar Nundu kuuza eneo la Mwakidila kwa bei chee Jumbe alijibu, “Hata mimi nashindwa kuelewa hiki ni kichekesho cha hali ya juu kuona mali za halmashauri zinachezewa kwa maslahi ya wachache kwa chuki za kisiasa, wakazi wa eneo lile walilipwa Tsh mil 48, ukiunganisha na taratibu za kiserikali katika kupima eneo na kupata vibali vyote maana eneo lile ni kubwa linafikia ekari 17 gharama zinafikia mil 70.

“Tazama eneo lenye thamani ya mil 70 kuuzwa mil 9 tena kwa taasisi inayoendeshwa na mtu ambae si raia wa Tanzania huo ni uendawazimu. Nikuhakikishie kitu kimoja ndugu yangu mimi ni mjumbe katika kamati ya fedha katika baraza la madiwani, tangu eneo lile liuzwe bila ya baraza kushirikishwa kamati imeomba kupewa risiti za manunuzi vimeshapita vikao vitatu bado hatujapewa risiti hizo,” aling’aka Jumbe.

Jumbe aliendelea kueleza “hawa wataliano walionunua lile eneo mimi siwafahamu sana lakini wana historia ya kuiba maeneo katika mkoa huu kwa kutumia kivuli cha taasisi ya kulea watoto yatima ya Casa Familia, miezi miwili iliyopita Waziri wa Ardhi na maendeleo ya  makazi Prof. Anna Tibaijuka alikuja Tanga katika wilaya ya Mkinga kufuatilia uporwaji wa ardhi uliofanywa na jamaa hawa, kapora hekari 50 Mkinga hawa si watu wazuri. Na wanasaidiwa na mbunge wa Muheza Herbert Mtangi.”

Nae diwani wa kata ya Mabawa (CCM) ambae pia ni naibu Meya wa Tanga Mzamini Shemdoe, aliiambia kidojembe kuwa Meya aliemaliza muda wake Salim Kisauji ndie anaesababisha matatizo yote haya kwani kipindi cha uongozi wake maamuzi ya wataalamu yaliamua hospitali ijengwe Masiwani Shamba lakini wakati alipotangaza nia ya kugombea ubunge kwa jimbo la Tanga aliwaahidi wakazi wa Mwakidila kuhamishia ujenzi wa hospitali hiyo hapo ikiwa watamuunga mkono katika kura za maoni.

“Unajua matatizo yote haya yasingekuwepo kama Kisauji asingebadili uamuzi wake wakati alipotangaza nia ya kugombea ubunge, alijua Nundu anatoka kata ya Mwakidila hivyo aliwashawishi wakaazi hao kumpigia debe ili akipata ubunge ahamishie ujenzi wa hospitali hapo na alifanikiwa kuwashawishi ingawa alibwagwa katika maeneo mengine,Nundu hakupata kura kabisa eneo la Mwakidila ingawa ndipo alipozaliwa,” alisema.

kidojembe ilipomuuliza Shemdoe, juu ya sakata la kuuzwa kwa eneo hilo kwa bei chee alijibu “Sikubaliani na tuhuma hizo kwani hazina ukweli ndani yake, eneo lile halijauzwa bali tulilitoa bure kwa taasisi ya Casa Familia ambayo inahusiana na kulea watoto yatima. Wataliano Fulani ndiwo walioitumia taasisis hii ya Casa Familia kununua eneo lile ambapo walituahidi kujenga chuo cha udaktari na hospitali kubwa ambayo itatumika kwa mafunzo na tiba.

“Mbunge Nundu ndie aliekuja na habari hizo njema na kuzungumza  na Mstahiki Meya ambae alikubaliana na uamuzi wa kulitoa eneo hilo . Hatukuwauzia narudia tena bali tuliwataka walipie taratibu zote za ununuzi wa ardhi ambapo walitoa Tsh mil 9. Sababu ya kufanya yote hayo ni kuhakikisha Tanga inanufaika na wawekezaji aina hii Nundu alituambia wataliano hao walitaka kuenda kujenga kituo hiki Mtwara ambapo walipewa eneo bure na wakazi wa mkoa huo, awali tulitaka kuwauzia kwa mil 200 lakini wakakataa na kusema wataondoka baada ya Mbunge kuongea na Mstahiki Meya tukaamua kuwapa bure ila walipie gharama za uhamishaji ardhi.”

Alipofuatwa Meya aliepita Salim Kisauji kujibu tuhuma zinazomkabili alisema anashangaa sana maamuzi yanayofanywa na baraza jipya la madiwani chini ya Meya mpya, kwani haoni sababu ya kuhusishwa na uhamishwaji wa eneo kutoka Masiwani Shamba kuenda Mwakidila kwani kwa maelezo yake hakukuwa na mpango wa kujenga hospitali Masiwani Shamba, bali kutofahamu ramani ya Tanga ndipo kunapowachanganya watu.

“Mwaka 2007 alipokuja Rais Kikwete kwa ziara ya Mkoa wa Tanga katika hotuba yangu pale Hospitali ya Bombo nilisema hospitali itajengwa maeneo ya ‘Masiwani area’ lakini sikusema ni wapi kwani wataalamu tuliowatuma walitamka hivyo katika utafiti wao. Sasa kwa mujibu wa ramani Mwakidila na Masiwani Shamba kata zote zipo chini ya Masiwani area hivyo mimi kuamua hospitali ijengwe Mwakidila hakuna makosa na si mimi tu bali maamuzi sikufanya peke yangu bali yalipata baraka zote za baraza la madiwani,” alieleza Kisauji.

Kuhusu tuhuma za kubadili eneo la ujenzi kwa kufuata maslahi ya kisiasa Kisauji alisema “hili linachekesha mimi nilitangaza nia mwaka gani, na eneo lilipatikana mwaka gani haiingii akilini hata kidogo watu walishalipwa tangu mwaka 2008 na uchaguzi ulifanyika mwaka 2010 wapi na wapi.

“Siku moja nikitokea kwetu maeneo ya Wilaya ya Pangani nilipita Mwakidila nikakutana na bwana Mbasha ambae alinieleza hizi habari za wataalamu kupita eneo hilo na kupima mimi skujua hata kidogo ni nini kinaendelea mpaka nilipokuja kuambiwa na wataalamu hao kuwa wamependekeza Mwakidila kuwa eneo muafaka kwa ujenzi wa hospitali hiyo sasa ukinambia mimi ndie niliependekeza eneo hilo ninakushangaa.

“Labda nikupe historia fupi ya ujenzi wa hospitali hii, miaka ya nyuma mkoa wa Tanga uliona haja ya kuwa na hospitali ya wilaya ili kupunguza msongamano katika hospitali ya Mkoa Bombo, tukawapa kazi kamati ya afya ya wilaya kutafuta eneo, wataalamu walipendekeza eneo linaitwa Maere lipo njia ya Pangani wakaona ardhi yake si nzuri, wakaenda Pongwe, Amboni, Kange, mwisho wakaenda Masiwani Shamba kote walipita ila wakavutiwa na Masiwani Shamba lakini eneo likaonekana halifai lina mashimo makubwa na liliwahi kuwa dampo hivyo ikashauriwa kusogezwa mbele kidogo ambapo ndipo lilipo eneo la Mwakidila.

“Wataalamu wakapendekeza eneo hilo na baraza la madiwani likapitisha na kitu kikishapitishwa na baraza la madiwani hiyo ni sheria,” alieleza Kisauji.

kidojembe haikuishia hapo ilimtafuta Mstahiki Meya wa Tanga Omar Guledi na kufanya nae mahojiano nyumbani kwake. Aliafikiana na mchakato wote wa upatikanaji wa eneo na kukiri baraza la madiwani kabla yeye hajaingia madarakani liliidhinisha eneo la Mwakidila kujengwa hospitali lakini baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wazee wa Masiwani Shamba ndipo akaamua kulifuatilia kwa undani suala hilo .

“Mimi nilikuwa miongoni mwa wanakamati ya afya waliokuwa wakihangaika kutafuta eneo, wakati huo sikuwa katika siasa kabisa. Tulihangaika sana na mwisho tukafika Masiwani Shamba, wataalamu wa ardhi wakasema eneo si zuri kuna mashimo mengi na liliwahi kuwa dampo hapafai, wakaamua kusogeza mbele kidogo ambapo ndipo palipopatikana hili eneo la Mwakidila baada ya hapo sikujua kilichoendelea ila najua kuwa baraza la madiwani lilishapitisha eneo hilo na watu walishalipwa fidia zao.

“Baada ya kuingia ofisini kama Meya mwaka 2010 malalamiko ya kwanza kupokea yalikuwa ni haya ya watu wa Masiwani Shamba wakiwakilishwa na diwani wao wa Tanga Sisi Abdi Abu, niliwataka waandike barua ya malalamiko kisha watie saini wawakilishi wote na walifanya hivyo. Nilipopitia ‘mafile’ ya halmashauri niliona kuwa maamuzi ya hospitali kujengwa Masiwani Shamba yalipitishwa na baraza mwaka 2008 halafu baraza hilohilo kupitia kamati ya fedha ambayo kimsingi haina mamlaka ya kutengua maamuzi ya kamati ya afya ilitengua na kufanya eneo kuwa Mwakidili mwanzoni mwa mwaka 2010 kabla ya uchaguzi. Nikashauriana na Mkurugenzi wa jiji lakini tukaona hii itakuwa tabu kwani maamuzi yote yalishapitishwa na baraza la madiwani kuwa hospitali ijengwe Mwakidila hivyo imeshakuwa sheria.

“Nilichofanya ni kusubiri kikao cha ‘full council’ na kuongea na madiwani juu ya malalamiko haya na kuafikiana kuwa mchakato huu uanze upya ili kuondoa malalamiko baina ya Masiwani Shamba na Mwakidila, tukawatuma wataalamu upya kutafuta eneo ndipo wakaamua hospitali ijengwe Masiwani Shamba, ambapo wakazi wa eneo hilo walisema hawataki chochote bali wanatoa bure eneo hilo.”

Hata hivyo kidojembe ilipokwenda katika eneo la Masiwani Shamba lilikuta eneo ni la hekari 7 tofauti na Mwakidila la hekari 17, halafu kuna malalamiko ya wananchi wa eneo hilo kuchukuliwa ardhi yao bila ya kushirikishwa na kuandika barua kwa afisa ardhi mkoa wa Tanga ambapo nakala ya barua hiyo kidojembe inayo pamoja na majina ya wanafamilia ya Riko kinyume na maelezo ya viongozi wa Mkoa kudai kuwa wakazi wa eneo hilo waliamua kulitoa bure. 

Aidha kidojembe, ilikwenda hatua moja mbele na kupata nakala ya hansard namba 139 ya Bunge la Tanzania, katika kikao cha bunge cha june 29, 2011 kikao cha nne ambapo Mh Amina Mwindau Mbunge wa viti Maalum Tanga (CUF) alimuuliza Mbunge Omar Nundu katika maswali mawili ya nyongeza juu ya malalamiko ya wakaazi wa Masiwani Shamba kudai maeneo yao tofauti na ilivyoelezwa kuwa eneo hilo lilitolewa bure.

Lakini majibu ya Nundu ambae wakati huo bado alikuwa ni waziri wa uchukuzi yalikuwa ni kusisitiza kutopata taarifa za malalamiko ya wakazi wa Masiwani shamba kudai fidia ya maeneo yao. Na kuongeza kuwa eneo la Mwakidila lilishalipiwa fidia na yupo katika mazungumzo na wawekezaji wanaotaka kujenga chuo cha utabibu ingawa hakutaja jina la wawekezaji hao.

Mwandishi alipomuuliza Mstahiki Meya Guledi, juu ya tuhuma za kuhusika na uuzaji wa eneo la Mwakidila akishirikiana na Mbunge Nundu alipingana na naibu wake Shemdoe, na kueleza kuwa eneo hilo halikutolewa bure bali liliuzwa kwa Tsh mil 9, lakini alikiri kuomba radhi mbele ya kikao cha madiwani wa CCM juu ya kufanya mchakato wa uuzaji wa eneo hilo bila ya kufuata taratibu za baraza la madiwani.

“Ni kweli zipo hizo taarifa za Mheshimiwa Nundu kuwa na chuki dhidi ya wakazi wa Mwakidila ambapo ndipo alipozaliwa ila sina uhakika kama kuna uhusiano wowote katika hili, wale wataliano waliletwa na Nundu ambapo alinambia aliunganishwa nao na mbunge wa Muheza Herbert Mtangi, ambapo zipo taarifa Mtangi na wataliano hao wana uhusiano wa kibiashara kwa muda mrefu.

“Hajawahi kuniita Dar es Salaam kama inavyosemwa kuenda kunishawishi nikubaliane na wazo la kuuza eneo lile lakini alinifuata ofisini na kunieleza wazo hilo nami nikazungumza na watendaji wangu ila kosa nililofanya sikulihusisha baraza la madiwani wakati mchakato unaendelea, nikaamua kuzungumza na katibu wa CCM Wilaya ili kuwaita madiwani wa CCM na kuomba radhi juu ya hili, nashukuru walinielewa ndipo tukaamua kuliingiza katika ajenda za vikao vya madiwani.

“Madiwani wa upinzani hawakukubaliana na wazo hili la kuuza eneo la Mwakidila, walitoka katika kikao lakini kutoka kwao hakujaathiri maamuzi yale kwa idadi wapo 13 na CCM tupo 23 hatufiki theluthi mbili lakini hili la theluthi mbili kwa mujibu wa sheria linafanyika ikiwa kuna uchaguzi lakini katika mambo ya maamuzi ya kimaendeleo halifanyi kazi,” alieleza Guledi.

kidojembe ilipotaka kujua gharama za ujenzi wa hospitali hiyo Mstahiki Meya alisema mpaka ujenzi ukamilike halmashauri inahitaji bil 15, lakini mpaka sasa wana mil 400 ambazo zitatumika kwa jengo la awali wakati mengine yanaendelea.

Mwandishi alipotaka kujua namna watakavyoshughulika na ujenzi wa miundombinu ambapo kwa mchanganuo zinahitajika takriban bil 4 kwa ajili ya barabara inayofikia kilomita tano kutoka barabara kuu mpaka kufikia eneo ujenzi, ambapo kwa viwango vya sasa kilomita moja inagharimu kiasi cha mil 800, kuunganisha maji kutoka bomba kuu lililo takriban kilomita nane kutoka eneo la ujenzi, na gharama za kuvuta umeme ambapo kunahitajika takriban nguzo ishirini ili kufikia eneo la ujenzi.

Guledi alijibu, “kimsingi halmashauri haina pesa hilo lazima nikiri na serikali inatoa pesa zake kidogodogo, angalia hizo mil 400 za ujenzi tumezipata ndani ya miaka miwili sasa hata sijui hayo mabilioni tutayapata ndani ya miaka mingapi,” alieleza kwa masikitiko.

Alipoulizwa juu ya Mbunge wa Tanga kutumia nafasi yake kuwakandamiza wakazi wa Mwakidila alijibu “Mhh… sina la kusema lakini ukweli ni kuwa Mwakidila mheshimiwa Nundu hakupata kura kuanzia za maoni mpaka za uchaguzi mkuu. Ndipo akasema atawaonyesha, niliwahi kuhudhuria kikao kimoja hapa Tanga nikiwa nae akawaambia kabisa kuwa hana kazi na watu wa Mwakidila kwani hawajamchagua.

“umeshawahi kukaa meza moja na Nundu… ni mkali sana na inachukua muda kumzoea siwezi kushangaa nikisikia amewajibu vibaya wapiga kura wake.”

kidojembe, ilipojaribu kumtafuta kwa simu mheshimiwa Nundu kujibu tuhuma hizi alijibu kwa ufupi tu kuwa hawezi kuzungumza chochote juu ya habari hizo kwani alidai mwandishi hajui chochote.

“Sipo tayari kuzungumza chochote juu ya vitu hivyo vitu ambavyo huna ujuzi navyo, nenda halmashauri ukawaulize,” alisema.

Hata baada ya mwandishi kumfahamisha kuwa alishaonana na watu wa halmashauri na majibu yao ni kuwa yeye Nundu ndie aliewaleta wale wawekezaji, alitoa sauti ya kukasirishwa na kukata simu. Baada ya mwandishi kujaribu kumpigia tena simu ilikuwa haipatikani.

Baada ya kidojembe, kukita kambi mjini Tanga imegundua kuwa mambo mengi ya kimaendeleo katika Mkoa wa Tanga yameshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na tofauti za kisiasa ama kikata, huku baadhi ya kata wakijiona ni wenyeji zaidi ya kata nyingine.

Aidha Mbunge wa Tanga Omar Nundu amekuwa akichukiwa na wakazi wengi wa Tanga tofauti na wajibu wake wa kazi unaomtaka kuunganisha wananchi na kuwa chachu ya maendeleo ya Mkoa huo, mbali na Mwakidila ambapo ndipo alipozaliwa Mbunge huyo ameonekana kikwazo katika utendaji kazi hasa kutokana na maamuzi yake yaliyojaa ukali na ubinafsi. 

Kitu kingine kidojembe ilichojifunza ni kuwa huyo mwekezaji mbali ya kudaiwa kuletwa na mbunge wa Tanga lakini hakuna hata kiongozi mmoja wa halmashauri anaejua jina lake kamili zaidi ya kumuita kwa jina la nchi yake ‘muitaliano.’

Uchunguzi uliofanya blogu hii ya kijamii umebaini kuwa shinikizo la kuuzwa kwa kiwanja hicho cha manispaa ni kutaka kuumaliza utata huo wa wapi hospitali ya Wilaya ijengwe kwa kudhani kuwa eneo hilo likipata mtu wa kulitumia itasaidia kuwanyamazisha wakaazi wa Mwakidila lakini hali imekuwa tofauti kwani wenyeji waliouza maeneo yao kwa bei ya kutupa sasa wanailalamikia halmashauri kwa kuwadanganya. Baadhi ya nakala za barua za malalamiko kidojembe ilifanikiwa kuzipata.

HAFIDH KIDO
TANGA, TANZANIA
JUNE, 2012

NB: Habari hii niliifanyia utafiti miezi mitano iliyopita, lakini kila gazeti niliyoipeleka haikufanikiwa kuchapwa, si kwasababu za kitaaluma wala maadili bali mgongano wa kimaslahi. Maana habari imefuata taratibu zote zinazopasa kufuatwa…. Hivyo ni ya kitambo kidogo…

No comments:

Post a Comment