Monday, December 24, 2012

Tumilioni 85 tunamuhusu Godbless Lema.....




MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema, huenda akazo kitita cha Sh85 milioni ambazo ni malimbikizo ya mishahara na posho mbalimbali ambazo hakulipwa wakati alipokuwa nje ya Bunge.
Lema amekuwa nje ya Bunge kwa miezi minane, kuanzia Aprili 5 mwaka huu wakati alipovuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, hadi aliporejeshewa ubunge wake Ijumaa wiki iliyopita na Mahakama ya Rufani ambayo ilikubali rufaa yake iliyopinga uamuzi huo.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah jana alisema baada ya kurejea bungeni, Lema atalipwa stahili zake zote anazostahili kwa muda wote wa siku 260 ambao alikwa nje ya Bunge.
Ingawa ofisi hiyo ya bunge haikusema atalipwa shilingi ngapi, uchambuzi wa malipo na stahili za wabunge umebaini kuwa mbunge huyo kupitia Chadema, atalipwa kitita cha Sh85 milioni ikiwa ni mshahara wake na posho kwa kipindi cha miezi nane alichokuwa nje ya Bunge.
Hata hivyo, Lema mwenyewe aliliambia gazeti hili jana kuwa, malipo yake yanaweza kufikia Sh60 milioni.
Lema aliyeibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, April 5, 2012, kufuatia kesi iliyofunguliwa na makanda watatu wa CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel, wakipinga ushindi wake.  Hata hivyo, Desemba 21,2012, Mahakama ya Rufani ilimrejesha bungeni, baada ya kushinda rufaa yake aliyokata mahakamani hapo kupinga hukumu na tuzo ya Mahakama Kuu Arusha iliyomvua wadhifa huo.
Tangu alipovuliwa ubunge hadi Mahakama ya Rufani ilipomrejesha tena bungeni, Lema alikuwa amekosa mikutano mitatu ya Bunge yenye jumla ya vikao 84.
Mikutano hiyo ni ule wa mwezi Aprili, mkutano wa Bunge la Bajeti Juni hadi Agosti na mkutano wa Novemba.
Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Bunge na wakiwamo wabunge wa upinzani na wale wa CCM vilisema kwamba malipo ya mbunge kwa mwezi ni Sh10.7 milioni, yakijumuisha Sh2.3 milioni za mshahara, Sh2.5 milioni za mafuta, posho ya jimbo inayokaribia Sh5 milioni na malipo mengineyo.
Kwa muda wa miezi zaidi ya minane ambao amekuwa nje ya Bunge, malimbikizo ya mshahara wake yanafikia Sh18.4 milioni, posho ya jimbo Sh40 milioni, mafuta Sh20 milioni na posho nyingine Sh6.6 milioni.
Kauli ya Lema
Hata hivyo akizungumza na Mwananchi jana, Lema alisema kuwa ingawa hajui kwa hakika kuwa malipo yake ni kiasi gani, lakini kwa hesabu za haraka, yanafikia Sh60 milioni.
Alisema wakati wa kesi hiyo ikiendelea hakuwahi kuwaza kwamba angerejeshwa bungeni, hivyo hakuwahi atalipwa kiasi gani na Bunge.
“Sijui kwanza nitalipwa nini kwani sikuwahi kukaa na kupiga hesabu za malipo haya, maana  najua ubunge  siyo faraja bali ni kuongoza harakati  za kuwasaidia wananchi kutetea haki zao mbalimbali,” alisema Lema.
Alisema alichokuwa akijua ni kwamba  kama akishinda basi, atarejeshewa gharama za kesi yake na makada wa CCM ambao walimfungulia kesi kwani ni malipo yanayotambulika kisheria.
“Najua lazima hawa makada wa CCM, walipe gharama zangu za kesi.Baada ya wao kushinda kesi Mahakama Kuu, Arusha, waliniletea madai ya kuwalipa Sh139 milioni na sasa mimi nawadai zaidi ya milioni 250,” alisema Lema na kuongeza:
“Kwa sasa nina imani nitapewa taarifa za malipo yangu na stahiki zangu zote za kibunge baada ya kurejeshwa bungeni. Katika hesabu za haraka haraka fedha hizo ni zaidi ya 60 milioni, ambazo zinaunganisha mishahara yangu tangu nilipovuliwa ubunge.”
Kauli ya Dk Kashillilah
Dk Kashillilah, licha ya kuweka wazi kuwa mbunge huyo atalipwa haki zake zote anazosahili kwa muda wote aliokaa nje, hata hivyo hakuweza kubainisha mara moja ni stahiki gani hasa akisema kuwa anasubiri kupata nakala  ya hukumu ya Mahakama ya Rufani ili kuona maelekezo yaliyomo.
Hata hivyo, Dk Kashillilah alifafanua kuwa kuna malipo ya aina mbili, yaani malipo ya  lazima, ambayo ni mshahara na stahiki nyingine anazostahili kutokana na wadhifa wake wa ubunge, na malipo yasiyo ya lazima, ambayo ni pamoja na posho za aina mbalimbali.
“Lema atalipwa masilahi yake yote lakini ni kwa yale tu anayostahili si kwa kila kitu. Kuna malipo ambao ni ya lazima kwa mfano mshahara, lakini kuna malipo mengine ambayo mpaka awe ameyafanyia kazi,” alisema Dk Kashillilah na kufafanua:
“Kwa mfano huwezi kumlipa per diem (posho ya kujikimu) au posho ya vikao ambavyo hakuhudhuria.”
Pamoja na ufafanuzi huo, katibu huyo wa Bunge alisisitiza kuwa bado wanasubiri kupata nakala ya hukumu yake ili kuona kile ambacho mahakama imeelekeza, na kwamba baada ya kuipata nakala hiyo ndipo watajua ni kipi anastahili kulipwa zaidi.
Akizungumzia matokeo ya hukumu hiyo, Dk Kashillilah alisema kuwa ushindi wa Lema umeonyesha kuwa mihimili mitatu ya Serikali, inafanya kazi zake kwa kujitegemea na siyo kubebana.
“Ushindi huu umeonyesha mgawanyiko sahihi wa madaraka katika Bunge, Serikali na Mahakama. Kila mhimili unafanya kazi zake bila kuingiliwa,” alisema Kashillilah.
Akataa pongezi za CCM
Katika hatua nyingine, Lema amekataa pongezi zilizotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kutokana na ushindi wa rufaa yake kwa madai kwamba Nape ni miongoni mwa watu waliokuwa wakimwombea ashindwe.
Pia aliukataa ushauri wa Nape unaomtaka aachane na maandamano, akisema kuwa maandamano ya Chadema hata siku moja hayakuwahi kulenga kwenda kwake (Nape), bali yalilenga kutetea haki na masilahi ya Watanzania.
“Napenda kumwambia Nape ajue, siasa za upinzani huwezi kuzitenganisha na maandamano kwani maandamano ni silaha kubwa ya kudai haki. Nasema maandamano ya Arusha na maeneo mengine nchini yataongezeka zaidi kwani tayari wamenipa ujasiri,” alisema Lema.
Alisisitiza kuwa woga kwake sasa umekwisha na kwamba  ataendelea kuwatetea wakazi wa Arusha hata kwa gharama ya maisha yake na kwamba kauli hiyo ni sawa na ile ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema ambaye walipokutana naye hivi karibuni alimtamkia kwamba walimvua ubunge ili kumpunguza kasi yake.
“Wakati ule sikuwa na ujasiri, lakini sasa wameniongezea ujasiri na kunitoa woga na ninawatetea wananchi kwa nguvu zangu zote ndani ya Bunge na nje na kamwe hawawezi kunifunga mdomo,”alisema Lema.
Chanzo: Mwananchi
<

No comments:

Post a Comment