Michezo
Wanafunzi
wazipaisha Kili Stars na Zbar Heroes
Kampala
Toleo la 271
5 Dec 2012
·
Huzifuata kila zichezapo
·
Kelele zao zatisha viwanjani
·
Kina Ngassa, Bocco wako juu
MICHUANO ya CECAFA
inayofanyika nchini Uganda
katika jiji la Kampala imefikia hatua ya nusu
fainali kwa timu mbili za Tanzania
kupenya hatua hiyo ikiwa ni habari njema katika timu nne kuingiza timu mbili.
Mwandishi wetu Hafidh Kido
alieko Kampala anaeleza haikuwa kazi ndogo
kuweza kuzichapa timu ngumu katika hatua ya robo fainali kwa Kilimanjaro Stars
kuichapa Rwanda 2-0, na
Zanzibar Heroes wakimaliza dakika 90 bila kufungana na Burundi
iliyokuwa ikiongozwa na mchezaji aliyewahi kuchezea timu za Tanzania Suleiman
Ndikumana ambaye alionekana mwiba mkali kwa golikipa wa Heroes kwa vipindi
vyote viwili.
Wazanzibari hawana budi
kumsifia golikipa wao Mwadini Ally ambae alifanikiwa kupangua penati kati ya
mbili ambazo Burundi waliosa
ikiwamo ya kwanza ya Ndikumana jumla iliyoipeleka Zanzibar nusu fainali ikiwa ni ya mikwaju
6-5.
Nia ya makala hii kuzungumzia
maandalizi ya timu mbili hizi za nyumbani kushiriki michuano ya kimataifa.
Imetokea bahati tu kwamba michuano hii ya CECAFA inafanyika nikiwa Kampala, na kwa bahati nzuri mji wa Kampala una Watanzania wengi ambao wanasoma
na kufanya kazi, hivyo haikuwa tabu kupata washabiki wanaowapa moyo wachezaji
wanapokuwa uwanjani.
Nimeona katika mitandao ya
jamii na kutazama baadhi ya vyombo vya habari hasa vya Uganda na Tanzania
watu wanashangazwa na kikundi kidogo ambacho kinaonekana kushangilia kwa nguvu
kila timu za Tanzania
zinapokuwa uwanjani.
Hiyo ni kama bahati lakini
inaonekana wazi vyama cha mpira wa miguu Tanzania
na Zanzibar
havikujiandaa kuja na timu ya washabiki ili kuwapa moyo wachezaji. Hili ni kosa
la kiufundi maana hakuna kitu kibaya kama timu
kucheza ugenini bila ya kelele za mashabiki wanaowaunga mkono.
Kikundi hicho kinachosifiwa
kwa kelele nyingi kila timu za Tanzania
zinapocheza ni cha wanafunzi wa Watanzania wanaosoma Chuo Kikuu cha Kimataifa
cha Kampala (KIU), waliomua kujikusanya na kuchangishana pesa za usafiri kwenda
na kurudi kila mechi.
Nilikutana na kiongozi wa
kikundi hicho ambae alijitambukisha kwa jina moja la Yassin ambaye anasema:
“Hakuna mtu yeyote anayetudhamini. Sisi ni Watanzania tunasoma KIU na tuna timu
yetu ya Hostel inaitwa Machakos FC, hivyo tunapenda mpira na tunazipenda timu
zetu za Taifa, hatuoni hasara kupoteza elfu kumi kwa siku kwenda na kurudi kila
zinapocheza.”
Binafsi nimehudhuria mechi
mbili tangu michuano ianze, mechi ya Kilimanjaro Stars dhidi ya Somalia iliyochezwa uwanja wa Lugogo na baadaye
nikajiunga na kikundi cha Machakos FC kwenda uwanja wa Wankulukuku kuwaunga
mkono Zanzibar Heroes waliokuwa wakicheza na Malawi.
Katika viwanja vyote viwili
ambavyo umbali kutoka uwanja mmoja mpaka mwingine ni dakika 30, hakukuwa na
mashabiki wa Tanzania.
Ni Machakos FC peke yao
ndio waliokuwa wakishangilia kuanzia mwanzo mpaka filimbi ya mwisho.
Hii maana yake ni kuwa kama vijana hawa wasingekuwa hapa, basi timu zetu
zingecheza mwanzo mpaka mwisho wa michuano bila mashabiki. Wapenzi wa soka
wanajua athari ya timu kucheza bila mashabiki.
Sikubahatika kukutana na
viongozi wa TFF lakini nilionana na mbunge Juma Nkamia ambaye ni mwanahabari
aliyekuwa hapa kutoa hamasa.
Alisema Nkamia kuhusu vijana
hao washangiliaji wa Kitanzania: “Hakika vijana hawa wamenifurahisha sana. Mwanzo sikujua kama
ni Watanzania, lakini nilipoona wamevalia fulana za timu yetu na bendera ya Tanzania nikajua
ni Watanzania hivyo nimezungumza nao na pia nimewapa nauli kidogo ziwasaidie
hasa baada ya kusikia ni wanafunzi.
“ Inaonyesha wana uzalendo wa
hali ya juu. Maana walipotoka kule Lugogo kwenye mechi ya Kilimanjaro Stars
wakaja na huku kwenye mechi ya Zanzibar Heroes. Huu ni upendo wa hali ya juu.”
Nadhani sasa kuna haja kwa
vyama vyetu vya soka kuwa na mfumo wa kuviwezesha baadhi ya vikundi vya
washangiliaji kwa maana ya nauli na matumizi kila timu zetu zinapocheza mechi
za kimataifa ili kuwaonyesha wachezaji ya kuwa hawapo peke yao hasa kwa
michuano hii inayoandaliwa ndani ya nchi za Afrika Mashariki ambako gharama za
safari na kuishi bado ziko chini kidogo.
Maajabu
ya Mrisho Ngasa
Mshambuliaji Mrisho Ngasa
amekuwa akionyesha uwezo mkubwa hapa pamoja na nidhamu ya hali ya juu kiasi
watu wanamtabiria kuwa mfungaji bora na hata kuwa mchezaji bora wa michuno hii.
Ni maajabu kwa mchezaji kuwa
mwenye magoli mengi katika mechi moja tu, Ngasa hakufanikiwa kufunga goli hata
moja katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Sudan
na Burundi, lakini
akaushangaza umma wa Waganda na wageni waliopo hapa baada ya kufunga magoli
matano peke yake siku Kilimanjaro Stars ilipoinyuka Somalia kwa mabao 7-0. Kati ya
magoli hayo ya Ngassa, la kwanza lilikuwa goli la mapema zaidi katika michuano
hii akiwa amelipachika katika sekunde ya 47 ya mchezo.
Siku hiyo magoli mengine
mawili yalifungwa na John Bocco ambaye naye yumo katika orodha ya wafungaji
bora akiwa na magoli matano, goli moja akiwa amefunga dhidi Rwanda juzi
Jumatatu.
CECAFA
kushindwa kujipanga
Waswahili wanasema kila
masika hayakosi mbu, Chama cha Soka cha Uganda (FUFA) ambao ni wenyeji wa
michuano hii kimebabaika baada ya uwanja walioutegemea wa Namboole kujaa maji
kiasi mechi kuhamishiwa katika viwanja ambavyo havina hadhi ya michuano hiyo
mikubwa katika nchi za Afrika Mashariki.
Awali michuano hii ilitakiwa
kuchezwa katika viwanja viwili vya mjini Kampala;
Nakivubo kilicho katikati ya mji pembeni ya Soko la Owino, na uwanja mkubwa
wenye hadhi ya kimataifa Namboole ambao unajulikana kama
Mandela Stadium kwakuwa ulijengwa kwa msaada kutoka kwa Rais wa zamani wa
Afrika Kusini Nelson Mandela.
Lakini mpaka michuano inaanza
ni Namboole tu uliokuwa tayari kwa michuano hiyo baada ya Nakivubo unaomilikiwa
na Jiji la Kampala (KCC) kushindwa kuwa tayari kwa michuano, hivyo FUFA
wakaamua kupendekeza uwanja wa Lugogo ambao nao upo chini ya (KCC) ambao hadhi
yake ni kama uwanja wa Azam Chamazi. Hivyo
kuwa na viwanja viwili Namboole na Lugogo.
Hata hivyo baada ya Namboole
kujaa maji ikabidi kipendekezwe kiwanja kingine cha Wankulukuku kilichopo
karibu na kilima cha Mengo njia ya kuelekea Masaka, mashariki mwa Uganda. Kwa
hakika kiwanja hicho ni cha hadhi ya chini. Kimetumika tu kwa kuwa ni lazima
kitumike.
Katika hatua nyingine,
taarifa zilizopamba magazeti ya Jumanne zilikuwa ni za kusimamishwa kazi kwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Uwanja wa Nakivubo, Geoffrey Kisseka, akidaiwa na Waziri
wa Michezo wa Uganda, Charles Bakkabulindi, ya kuwa ameshindwa kuitisha mkutano
wa Bodi kwa muda mrefu na kushindwa kuuandaa uwanja kwa ajili ya michuano ya
CECAFA hali iliyofanya nchi kupata aibu kubwa.
Hakuna marefu yasiyo na ncha,
michuano hii inatarajiwa kukamilika Jumamosi hii huku nusu fainali zikipigwa
kesho Alhamisi.
Fainali itachezwa kwenye
Uwanja wa Namboole kuhitimisha michuano hiyo iliyosisimua na kuonyesha vipaji
vya hali ya juu kwa timu washiriki ambazo ni Tanzania Bara, Zanzibar,
Kenya, Uganda, Burundi,
Sudan, Sudan ya Kusini (ambayo inashiriki kwa mara ya
kwanza), Eritrea, Ethiopia, Somalia,
na Malawi
ambayo ni timu mwaalikwa.
Mpaka sasa wafungaji
wanaoongoza ni Mrisho Ngasa (5, Kilimanjaro Stars), John Bocco( 5, Tanzania), Umony (3, Uganda),
Ndikumana (3, Burundi),
Nduwagira (3, Burundi) na
Msowoya (3, Malawi).
No comments:
Post a Comment