Saturday, December 22, 2012

Kampala mji wenye vilima vilivyopangwa vizuri kwa kupendeza....


Na Hafidh Kido

Mara nyingi miji mikubwa katika nchi hupata hadhi kutokana na uzuri ama kuwepo na mzunguko mkubwa wa fedha. Mathalan Dar es Salaam, Nairobi, Harare ama Cape Town miji yote hiyo imepata hadhi kutokana na uzuri wa majengo na mzunguko wa fedha.

Kampala ni mji mkuu nchini Uganda, na ndiyo mji ulio katikati ya nchi kama ilivyo Dodoma kwa Tanzania na ndiyo  maana kabila maarufu nchini Uganda ‘Baganda’ ambalo jina Uganda limetokana nalo ndilo linaloushikilia mji wa KampalaUganda central’.

Siri ya waarabu na waingereza kuupenda mji wa kampala wakati walipofika Uganda kwa mara ya kwanza ni muonekano mzuri wa vilima vidogo na chanikiwiti kilichokolea mpaka waingereza wakaubatiza jina la mji wa kijani chini ya jua ‘the green city in the sun’ ama ‘the pearl of Africa’ lulu ya afrika.

Sababu ya jina Kampala wataalamu wa historia wanasema kabla ya hapo kila kilima kilikuwa kikiitwa kutokana na jina la asili mathalan ilipokuwa ikulu ya Kabaka paliitwa Mengo, lakini pembeni ya Mengo ambapo sasa upo msikiti mkubwa uliojengwa na hayati Muammar Gadaffi wa  Libya palikuwa na bonde lililojaa nyasi nzuri ambapo wanyama hasa jamii ya swala walikuwa wakila nyasi na kunywa maji.

Wanyama hao jamii ya swala kwa kizungu wanaitwa ‘impala’, mfalme wa Buganda akawa anatoka Mengo anakuja kuwinda katika bonde hilo baganda wakapaita eneo hilo ‘kasozi k’ empala’ ama kwa kizungu ‘the hills of impala’. Kutokana na sababu za kimatamshi waingereza pamoja na wenyeji wakawa wanafupisha badala ya kuanza na ‘kasozi’ ambapo kwa lugha ya luganda ni kilima wakawa wanaita ‘k’empala’ tu, ndipo likaja jina Kampala.

Kutokana na umaarufu wa eneo hilo mwakilishi wa kampuni ya kikoloni ya ‘Imperial British East African Company’ Captain Fredrick Lugard alianzisha ofisi eneo hilo mnamo mwaka 1890 ambayo ipo mpaka sasa ila kwa sasa eneo hilo linaitwa Old Kampala.

Mwaka 1962 Kampala ikatangazwa kuwa mji mkuu wa Uganda na ilikuwa na kilomita za mraba 19 ikiwa na vilima saba ikabatizwa jina la ‘City of seven hills’.

Ingawa kwa sasa baada ya mji kupanuka kuna vilima vingine vinavyokaribia ishirini vimeingia katika ramani ya mji ila vilima maarufu vilivyoanzisha mji ni saba ambavyo ni Mengo , Lubaga, Namirembe, makerere, Kololo, Nakasero na Old Kampala.

Ili kupata faida ya vilima hivi saba itabidi tukichambue kilima kimoja baada ya kingine ili ujue sababu ya jina na eneo linatumika kwa shughuli gani kwa sasa.

Mengo
Kilima hiki kipo futi 4,000 kutoka usawa wa bahari ni maarufu katika historia ya Uganda kisiasa na kiimani hasa ikizingatiwa ndipo utawala wa ‘Buganda kindom’ ambao ulijizolea umaarufu mkubwa barani Afrika ulipoanzia. Wafanyabiashara wa kiarabu na hata wakoloni wa kiingereza walipokuja walifikia hapa na inasemekana kabila hili ‘baganda’ hawakutawaliwa bali wao waliwasaidia waarabu kutafuta watumwa na kuwapa maeneo wazungu.

Katika kilima hiki linapatikana ziwa kubwa lililochimbwa kwa mikono linaitwa  ziwa la Kabaka. Mwaka 1880 Kabaka Basamula Mwanga alitaka kuunganisha jumba lake la kupumzikia liitwalo ‘Twekobe’ na ikulu yake nyingine iliyopo Munyonyo karibu na ziwa Victoria ambapo pia alitaka kuitumia kama njia ya kutorokea ikiwa patatokea matata. Ziwa lilikadiriwa kuwa na urefu wa kilomita kumi na moja na kina cha futi 200 kuenda chini, walichukuliwa watu wa kila aina kufanya kazi hiyo na kazi ya kuchimba kwa majembe na vifaa vingine duni ilikuwa inaanza saa tatu asubuhi mpaka saa kumi jioni kila siku bila kupumzika na ilitakiwa ikamilike baada ya miezi 11 bila kupumzika.

Lakini ziwa hilo halikukamilika kwani wachimbaji ambao wengi ambao awali walikuwa wapagani wakahamia katika imani ya Kikristo walitaka mapumziko kila jumapili ili waende kanisani, kabaka akakataa. Hivyo waligoma kwa hasira Kabaka akawaua kwa kuwachoma moto idadi kubwa.

Ziwa lilikuwa limefikia eneo la Najjanankumbi kilomita mbili kutoka Mengo, lakini mbali ya kutokamilika bado ukiliona linaonekana ni ziwa la kihistoria na linavutia sana hasa unaposikia lilichimbwa kwa vifaa duni.

Mpaka sasa siku hiyo ya mwezi June waliyouwawa wafanyakazi wale inakumbukwa na waumini wa dini ya kikristo kama ni siku ya mashujaa watu walioifia dini, inaitwa ‘Uganda martyrs’, na inasherehekewa nchi nzima watu hawaendi kazini. Lakini kabila la baganda wanaichukia sana siku hii maana inamdhalilisha mfalme wao anaonekana ni mkatili.

Namirembe
Kilima hiki kipo futi 4,134 kutoka usawa wa bahari kimepakana na kilima cha Mengo. Katika kilima hiki lipo kanisa la kwanza la ki-protestant liitwalo St. Paul’s Cathedral, pia ipo hospitali ya kwanza kujengwa nchini Uganda iliyoanzishwa na Sir Albert Ruskin Cook mwaka 1897 ambapo mpaka sasa ipo na inaitwa Mengo Hospital.

Pia katika kilima hiki ndipo panapopatikana makaburi ya familia ya kifalme Buganda ‘Kasubi Tombs’ ambayo yameingizwa katika urithi wa dunia ingawa yaliteketea kwa moto mwaka 2010.

Aidha katika kilimo hiki ipo ‘Bulange’ hili ni bunge la Buganda kingdom ambapo machief na mawaziri wanakutana kujadili mustakabali wao pia Kabaka akitaka kukutana na viongozi wake anakuja hapa. Kwa jina lingine inaitwa ‘Lukiiko’ ikimaanisha bunge.

Makerere
Ni futi 4,188 kutoka usawa wa bahari, kilima hiki kwa jina lingine kinaitwa ‘chemchem ya taaluma’ ama ‘kilima cha wasomi’. Kwasababu ndipo kilipo chuo kikuu cha kwanza Afrika mashariki kilichoanzishwa mwaka 1922.

Lakini wenyeji wanasema awali kilima hiki kilikuwa kikijulikana kama ‘Bwaise’, ila miaka ya nyuma mmoja wa wafalme wa Buganda alikuja katika kilima hicho kufuata (hawara), lakini akajisahau mpaka usiku ukaingia bila kurudi Mengo ilipo ikulu.

Kutokana na aibu ya kukaa kwa mwanamke wa pembeni mpaka kiza kimeingia akashituka na kusema kwa lugha ya ki-baganda, luganda ‘Ganno makerere’ yaani giza limeingia bila kujijua. Tangu siku hiyo kilima hicho kikapewa jina la utani la Makerere, hivyo hata waingereza walipojenga chuo hapo waliamua kukipa jina hiloMakerere University’.

Old Kampala
Inapatikana katika futi 4,000 kutoka usawa wa bahari, hapa ndipo mji wa Kampala ulipoanzia kwa sasa ni eneo la biashara na makazi ya watu.

Wakati wa utawala wa Idd Amin Dada ambae alikuwa ni Muislam kiimani alilitoa eneo hili kwa waislam ili wafanyie ibada. Maelezo yake ni kuwa katika kampala kuna vilima viwili Namirembe na Lubaga ambavyo vinashikiliwa na makanisa ya Anglican na Catholic, hivyo akataka kilima cha Old Kampala kishikiliwe na waislam.

Ndipo akaamua kujenga msikiti ambao hakufanikiwa kuumaliza baada kuondolewa madarakani na jeshi la Tanzania mwaka 1979. baadae Rais wa Libya Muammar Gadaffi alikuja kuumalizia mwaka 2008. Katika kilima hiki ndipo panapopatikana ofisi za baraza la waislam Uganda.

Lubaga
Kilima kipo futi 4,134 kutoka usawa wa bahari, kipo karibu sana na vilima vya Mengo na Namirembe kihistoria na kieneo.

Katika kilima hiki ndipo yalipokuwa makao makuu ya Buganda Kingdom lakini alipoingia Kabaka Muteesa I, aliamua kuhamisha makazi yake katika kilima cha Mengo.

Kwakuwa tayari kanisa Anglican walishapewa eneo la kilima cha Namirembe na kabaka hivyo walipokuja wamishenari wa kikatoliki ama white fathers kutoka Ufaransa kabaka aliamua kuwapa eneo katika kilima cha Lubaga ili kuondoa migongano baina ya Anglican na Catholics.

Mpaka leo kilima cha Lubaga ndiyo makao makuu ya kanisa katoliki nchini Uganda, ndipo yalipo makazi ya kardinali wa Uganda, pia lipo kaburi la kardinali wa kwanza mweusi Uganda Emmanuel Nsubuga.

Nakasero
Hapa ndipo ulipo moyo wa Kampala, kwa Tanzania tunaweza kusema ndiyo Posta. Kunapatikana kila kitu mahoteli makubwa, soko, ofisi za serikali, mahakama kuu, bunge la Uganda na hata wauza maneno (matapeli) wanapatikana katika kilima hiki.

Nakasero ipo futi 4,134 kutoka usawa wa bahari ambapo hata ikulu ya nchi inapatikana hapo na televisheni ya taifa UBC.

Kololo
Kama vilivyo vilima vingine kololo ipo futi 4,305 kutoka usawa wa bahari, na kilipata jina hili la ‘kololo’ kutoka kwa chifu wa Payiira kabila la Acholi alieitwa Rwot Awich, ambae aligombana na waingereza na kutupwa katika kilima hicho mnamo mwaka 1912.

Chief Awich, alikuwa akipiga yowe kwa lugha ya kiacholi akisema ‘kololo’ alilirudia neno hilo mara nyingi huku akionyesha ana maumivu makali. Maana ya neno hilo kwa lugha ya kiacholi ni ‘upweke’ akimaanisha wazungu wamemuacha mpweke katika kilima hicho ili afe.

Kwa bahati mbaya walinzi wa kiafrika ambao waliambiwa wamlinde hawakujua maana ya neno hilo kwani hawakuwa waacholi, hivyo wakawa wanakiita kilima hicho ‘kilima cha kololo’.

Kwa sasa kilima hicho kina nyumba za maofisa wa serikali, kiwanja cha ndege za kijeshi na nyumba za wanajeshi. Pia pamefanywa ni eneo la kuzikia mashujaa, lakini mpaka sasa mashujaa wawili tu wamezikwa mmoja ni mpigania uhuru ambae alianzisha chama cha kwanza cha siasa cha kiafrika ‘Uganda National Congress’ I.K. Musaazi pamoja na mwanzilishi na mwenyekiti wa kwanza wa chama cha sasa kinachotawala Uganda National Resistance Movement (NRM) ambae pia alikuwa Rais wa Uganda baada ya kuondolewa Idd Amin Dada mwaka 1979 Yusuf Kironde Lule.

Hata hivyo vilima vingine vilivyoongezeka ambavyo ni maarufu na vina maendeleo ya hali ya juu ni kibuli (kilima hiki kinakaliwa na waislam wengi sana hata kabla ya uhuru, alama kubwa ya kilima hicho ni msikiti na hospitali ambavyo vilijengwa na mwana wa mfalme wa Buganda Prince Badru Kakungulu. Kadhalika katika kilima hiki kuna makao makuu ya jeshi la polisi na chuo cha maofisa wa polisi).

Kilima cha Nsambya (panapatikana kituo cha kimisheni ambapo kuna shule na hospitali ya kimisheni maarufu Nsambya Hospital, kadhalika ni kituo cha biashara na wachonga vinyago kuna maendeleo makubwa katika kilima hiki maana hata ubalozi wa Marekani unapatikana katika kilima hiki.

Naguru (hiki ndicho kilima kikubwa kuliko vyote Kampala kina urefu wa futi 4,331 kutoka usawa wa bahari, kinatumika kuweka mitambo ya mawasiliano kama simu na radio).

Kilima cha Mbuya (ndipo ilipo hospitali ya rufaa ya jeshi na kanisa la kikatoliki liitwalo ‘the tower of lady of Africa), kilima cha Mulago (ndipo ilipo hospitali kuu ya Uganda ilijengwa mwaka 1917, ambapo iliongezwa mwaka 1960 na kuwa hospitali kubwa Afrika mashariki ikipewa jina la kilima hicho Mulago Hospital), kilima cha Buziga (kipo njia ya Gabba kuelekea ziwa Victoria, ndipo palipo na nyumba za matajiri ambapo ni eneo la pili kwa nyumba za matajiri baada ya Muyenga, pia ndicho kilima cha pili kwa urefu kampala kina urefu wa futi 4,322 kutoka usawa wa bahari).

Kilima kingine ni Muyenga (kabla ya mwaka 1970 kilima hiki hakikuwa na watu wengi lakini kufikia mwaka 1986 baada ya Rais Museven kuchukua nchi matajiri wakaanza kujenga majumba ya kifahari na mahoteli ya kisasa ambapo kwa sasa ndilo eneo lenye matajiri wengi kuliko eneo lolote mjini Kampala. Hata eneo maarufu la Kabalagala kwenye starehe za kila aina lipo Muyenga, na njia ya kuelekea munyonyo ilipo Hoteli panapofanyika mikutano mikubwa ya kimataifa inapatikana katika kilima hiki, chuo maarufu cha Kampala Internationala University (KIU) pia kipo katika kilima hiki).

Mutundwe (kilima hiki bado hakijaguswa sana na watu, ila kuna shule, viwanda na baadhi ya shughuli za kiuchumi mbali ya hivyo ni kilima ambacho unaweza kuuona mji wa Entebbe kutoka umbali wa kilomita 30, unaweza kuona ndege zikipaa na kutua ukiwa katika kilima hiki), kilima cha Mutungo (ukiwa hapa unaweza kuuona uwanja mkubwa wa michezo Namboole na ziwa Victoria, pembeni ya kilima hiki kunapatikana eneo la bugolobi maarufu kwa viwanda na biashara kadhalika gereza maarufu Uganda la Luzira unaweza kuliona ukiwa hapa).

Kireka (katika kilima hiki ndipo ikulu ndogo ya mfalme wa sasa wa Buganda Kabaka Ronald Muwenda Mutebi ilipo, pia Namboole Stadium inapatikana katika kilima hiki), Makindye (mwaka 1920 wakoloni wa kiingereza walitenga kilima hiki kuwa ni makazi yao, wakoloni walichagua eneo hili kwa maana walipaona ni salama kwani Buganda Kingdom walikuwa na nyumba za askari wao eneo hilo.

Na waingereza waliwaamini sana baganda, ambapo kwa sasa eneo hilo lililokuwa nyumba za askari wa Buganda limekabidhiwa kwa askari wa Uganda, mwaka 1962 Uganda ilipopata uhuru Rais wa kwanza wa Uganda Muteesa II ambae pia alikuwa mfalme wa Buganda alijenga nyumba yake ya kupumzikia. Hivyo kufanya eneo hilo kuwa la watu wa serikali na wazungu, hata sasa wananchi wa kampala wanaliita eneo hilo ‘Makindye Kizungu’ yaani eneo la wazungu.

kilima cha Banda (zamani kilima hiki kilijulikana kama Bandabalogo, kina historia kubwa na kabila la baganda katika kilima hiki Sekabaka Muteesa I alikumbana na matatizo mengi kama maradhi na uchawi mpaka kufikia kuhama.
Muteesa I ambae alikuwa na wake 84 alihamishia makazi yake eneo la Nabulagala ambapo baadae alibadili jina na kupaita Kasubi akifananisha na eneo alipozaliwa mama yake katika kijiji cha Kyaggwe. Kasubi ndipo palipo na makaburi ya ukoo wa kifalme wa Buganda.

Hata hivyo mfalme wa sasa wa Buganda Ronald Mutebi ameamua kujenga tena ikulu ndogo katika kilima cha Banda akikumbuka matatizo yaliyompata babu yake mfalme Muteesa I.

Kilima cha banda pia panapatikana chuo kikuu cha serikali Kyambogo, shule ya wasichana ya Nabisunga na maduka mengi ambapo pana shughuli nyingi za biashara.
Hiyo ndiyo Kampala nadhani ndiyo mji pekee barani Afrika ambao vitongoji vyake vyote vipo katika vilima na majina ya vilima yote yana maana na historia kubwa kwa ufalme wa Buganda wenyeji wa Kampala. Kitu kinachofurahisha tangu kuja kwa waarabu na waingereza nchini Uganda kabila la baganda wanapata bahati ya kusikilizwa sana na watawala.

Maana hata sasa mtu yeyote anaetaka kugombea urais nchini Uganda lazima apate baraka kutoka kwa mfalme wa Buganda. Hata wakati waziri mkuu wa kwanza wa Uganda Milton Obote alivyompindua Rais wa kwanza wa Uganda ambae alikuwa mfalme wa Buganda Muteesa II alipata tabu sana katika kuiongoza nchi hiyo bila ya baraka za kabila la baganda.

Ndipo Idd Amin alipochukua madaraka mwaka 1971 baada ya kumpindua Milton Obote aliamua kuurudisha mwili wa Muteesa II ambae alifia uhamishoni nchini Uingereza, lengo likiwa ni kupata baraka za baganda.

Ingawa Obote alifuta utawala wa kikabila ‘kingdoms’ nchini Uganda lakini mwaka 1986 Rais Yoweri Museven alipoingia madarakani alirudisha utawala wa makabila na kuwapa kipaumbele kikubwa kabila la Baganda ambao wanashikilia Kampala. 

Cha kushangaza Rais Museven ameruhusu kurudi wafalme wa makabila mengine kama bateeso, baganda, batoro, lakini katika kabila lake la banyankole linalojulikana hajaruhusu. Wadadisi wa mambo ya siasa wanasema aliogopa kuwa chini ya mfalme wa kabila lake aliejulikana kama Omugabe wakati yeye ni Rais wa nchi. Maana kwa taratibu za makabala ya Uganda mfalme wako unamuheshimu kuliko mtu yeyote duniani hata akikuambia ufanye nini hutakiwi kupinga.

HAFIDH KIDO
KAMPALA, UGANDA
DECEMBER, 2012







 Picha za juu ni mitaa ya kampala inavyoonekana Nakasero....

No comments:

Post a Comment