Monday, December 31, 2012

Soma namna mhasibu wa Simba SC Erick Sekete alivyoporwa mapato ya Simba Vs Tusker ya Kenya...


MHASIBU wa Klabu ya Simba, Erick Sekete Jumamosi wiki hii ameavamiwa na watu wasiojulikana na kuporwa zaidi ya Sh7 milioni.
Fedha hizo zilikuwa ni za mgao wa klabu hiyo ilizopata katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya mabingwa wa Kenya, Tusker FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kuwa tukio hilo lilitokea maeneo ya Sinza.
“Ni kweli, tukio hilo limetokea mhasibu wetu, Erick alivamiwa na watu waosiojulikana wakati akitoka Uwanja wa Taifa kwenye mechi yetu ya kirafiki dhidi ya Tusker Kenya.
“Ameporwa kiasi cha Sh7 milioni, mgao wa mechi ya kirafiki dhidi ya Tusker,” alisema Kamwaga.
“Wakati Erick akikumbwa na tukio hilo alikuwa pamoja na Stanley Philipo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na yupo hapa Simba kwa ajili ya masomo kwa vitendo ya mawasiliono ya umma,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo walitoa taarifa Kituo cha Polisi Magomeni ambapo sasa suala hilo linashughulikiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Polisi wa Kinondoni, Charles Kenyela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na watalitolea ufafanuzi baadaye.
“Tumepokea taarifa ya tukio hilo, tutalitolea ufafanuzi baadaye,” alisema Kinyela.
Wakati huohuo, aliyekuwa kocha wa Simba, Milovan Cirkovic amesema bado anaikumbuka klabu ya Simba na anaamini siku moja atarejea kuifundisha.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya mtandao wa Facebook, Cirkovic alisema yuko tayari kurudi kuinoa Simba wakati wowote endapo uongozi wa klabu hiyo utamhitaji.
“Simba ipo kwenye moyo wangu na ndiyo maana kila wakati naikumbuka, malengo yangu yalikuwa kuiacha ikiwa na rekodi mpya katika michuano ya kimataifa nasikitika sijafanikiwa.
“Mwaka jana tulikuwa na uwezo wa kufika mbali zaidi katika michuano ya Kombe la Shirikisho tukafanya uzembe tukaondolewa.
“Nilikuwa na ndoto ya kufanya vizuri katika michuano ijayo lakini yamekuja mambo haya kwa kweli nimesikitika sana,” alisema Cirkovic. “Unajua ili uweze kufanikiwa katika taaluma ya ukocha lazima uwe na maelewano mazuri na wachezaji wako jambo ambalo mimi nililifurahia Simba. Wachezaji walinipenda na mimi niliwapenda.”
“Siwezi kuichukia Simba kwa sababu mkataba wangu umesitishwa, ninasikitika kuondoka mapema na ndiyo maana, leo ama kesho nipo tayari kurudi kama watanihitaji,” alisema Cirkovic.
Cirkovic anayeishi katika Mji wa Cacak nchini Serbia pia aliushauri uongozi wa Simba kuendelea kuipa kipaumbele timu yao ya soka ya vijana akisema ndiyo dira ya mafanikio kama wanahitaji mafanikio ya kweli.
“Shomari Kapombe, Christopher Edward na Jonas Mkude ni matunda ya utaratibu mzuri wa kulea vijana, ushauri wangu waendelee kuitunza na mafanikio watayaona,” alisema Cirkovic.
 Chanzo: mwananchi.com

No comments:

Post a Comment