Thursday, December 6, 2012

Walimu wakimbia shule kwa kuogopa kubakwa na wanafunzi..


Na Amini Yasini, Rufiji
WALIMU wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Ruaruke wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani, wameitelekeza shule hiyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya baadhi ya wanafunzi kuwadhalilisha kimapenzi, ikiwamo kuwabaka baadhi yao.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa mbali na udhalilishaji huo, wanafunzi hao wamekuwa wakiwatishia maisha walimu wao kwa namna mbalimbali. Katika moja ya vitisho hivyo, wamechoma moto nyumba zao tatu.

Habari hizo zimeeleza kwamba walimu hao wamelazimika kuikimbia shule hiyo baada ya baadhi ya walimu wa kike kutongozwa na wanafunzi, kupigwa mabusu kwa nguvu hadharani, kutishiwa kuchomwa visu na kuchorwa vikatuni vya kudhalilisha.

Mmoja wa walimu hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini akihofia kushughulikiwa na wanafunzi hao alisema amelazimika kuikimbia pamoja na walimu wenzake wote, kwa kuwa wameshindwa kudhibiti tabia hiyo kutokana na vijana hao kuungwa mkono na wazazi wao.

Akizungumza kwa simu akiwa Dar es Salaam, mwalimu huyo alisema shule hiyo yenye wanafunzi 485, imepoteza mwelekeo, haitawaliki na mazingira yake hayavutii walimu, hasa wa kike, kuishi na kufanya kazi.

“Tumevumilia vya kutosha, lakini kila kukicha hali inazidi kuwa mbaya. Walimu wanafikia mahala wanabakwa! Kibaya zaidi wazazi na mamlaka nyingine hazionyeshi ushirikiano kwetu, wazazi wanawa-support (wanawaunga mkono) watoto wao,” alieleza.
Hata hivyo, mwalimu huyo hakuwa tayari kueleza kwa undani kuhusu vitendo hivyo vya ubakaji lakini alieleza kwamba vimekuwa vikitokea walimu hao wanapokuwa katika matembezi usiku.

Vitendo hivyo vimekuwa vikitokea baada ya wanafunzi hao kuwatongoza walimu wao na kukataa kufanya nao mapenzi.

Mwalimu huyo alidai kuwa walimu wamekuwa wakitishiwa kuchomwa visu na nyumba zao kuchomwa moto, huku walimu wanne wa kike wakidhalilishwa kimapenzi kwa kupigwa mabusu na kutongozwa na wanafunzi.
“Wanafunzi wamefanya mtihani wa kidato cha pili chini ya ulinzi wa askari polisi wenye silaha kitu ambacho si cha kawaida,” aliongeza.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Ofisa Elimu Sekondari, Adnan Mwenda alisema asingependa kuzungumzia tatizo hilo kwa kuwa siyo msemaji. Akashauri atafutwe mkurugenzi wa wilaya… “Unaweza kuzungumza mambo mengine yakakuletea matatizo,” alisema Mwenda kabla ya kuelekeza atafutwe mkurugenzi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Leonard Rwegasira alithibitisha walimu hao kuikimbia shule hiyo na kusema kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, itakutana hivi karibuni kujadili suala hilo.
“Ni kweli shule hiyo imetelekezwa, walimu wamekimbia na wanafunzi hawaendi shule. Tatizo tunalifahamu na Mkuu wa Wilaya anafanya jitihada mbalimbali kurekebisha tatizo hilo,’ alisema.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruaruke, Hemedi Mpullu pia alithibitisha walimu hao kuitelekeza shule hiyo na kusema Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu ameagiza kufanyika kwa kikao cha dharura ili kupatikana mwafaka kati ya walimu hao, wanafunzi na wazazi.
“Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa amepanga pia kufanya mkutano hapa Ruaruke ili kutafuta mwafaka,” alisema Mpullu.
Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT), Wilaya ya Rufiji,  Manyama Lazaro alisema kuondoka kwa walimu hao, kumefanya shule hiyo ijifunge yenyewe, kwani wanafunzi nao sasa hawaendi shule.

“Wanafunzi wamefikia hatua ya kuwachora walimu wa kike wakifanya mapenzi na walimu wa kiume katika kuta za vyoo! Huu ni udhalilishaji mkubwa,” alisema.
Lazaro alieleza kuwa katika siku za hivi karibuni, wanafunzi hao walichoma moto nyumba tatu za walimu na Bodi ya Shule iliamua kuwa wanafunzi hao waitwe na wazazi wao ili walipe gharama za uharibifu.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment