Wednesday, March 27, 2013

Mwanafunzi wa kitanzania Afariki Airport ya China akirudi nchini.


Dar es Salaam. Mwanafunzi wa Kitanzania aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Huazhong nchini China, Leonard Peter Tambalu amefariki dunia ghafla katika mazingira ya kutatanisha wakati akiwa anajiandaa kurejea  nchini.
Tambalu aliyekuwa mwaka wa pili katika chuo hicho kilichopo kwenye mji wa Wuhan, alifikwa na mauti hayo Machi 17 mwaka huu wakati akiwa katika Uwanja wa Ndege mjini Beijing. Marehemu alikuwa Ofisa Kilimo Mwandamizi kutoka wilayani Iramba mkoani Singida.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Christina Midelo hakukubali wala kukanusha kuwapo kwa tukio hilo. “Sina taarifa za kifo cha kijana huyo, wanaoweza kuzungumza ni Ubalozi wa China kwa kuwa ndio waliokuwa wakimsomesha.”
Balozi wa Tanzania nchini China, Philip Marmo, ambaye yupo nchini kutokana na ushiriki wake katika mapokezi ya Rais wa China,  Xi Jinping, alikiri kufahamu suala hilo. Katibu wa Umoja wa Wanafunzi wanaosoma vyuo mbalimbali katika mji wa Wuhan (Wtasa), Humphrey Sikauki, alithibitisha kifo cha Tambalu na kwamba mwili wake ulikuwa unafanyiwa uchunguzi na maofisa wa serikali ya China wakishirikiana na wale wa Tanzania.
“Tangu alipofariki madaktari walisema ripoti ingetolewa baada ya siku saba ambazo ziliisha Jumatatu, mpaka sasa hiyo ripoti hatujaipata lakini Mwambata wa Elimu katika Ubalozi wa Tanzania nadhani atakuwa ameipata kwa sababu ndiye alikuwa akiiwakilisha Tanzania katika uchunguzi huo,” alisema Sikauki.
Gazeti hili lilijaribu mara kadhaa kuwasiliana na Mwambata wa Elimu katika Ubalozi wa Tanzania nchini China, George Manongi lakini  mawasiliano yalikuwa magumu, kutokana kushindwa kusikilizana.
Kifo cha Tambalu
Tambulu ambaye alifika China Septemba  2011 kwa ajili ya masomo yake ya fani ya Kilimo, alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Chinese -Japanese Friendship.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, baada ya kufika Uwanja wa Ndege wa Beijing alianguka, kabla ya kupelekwa hospitalini, ambako ilibainika kwamba alikuwa amekwishafariki.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa, uongozi wa hospitali ulitoa siku saba za uchunguzi kabla ya kutoa mwili wa marehemu, lakini tatizo kubwa limekuwa ni uwezo wa kuusafirisha mwili huo.
Habari zinasema Wizara ya Kilimo haiwezi kuwajibika moja kwa moja kuusafirisha mwili wa marehemu isipokuwa  halmashauri yake.
Marmo kwa upande wake alisema ni vigumu kwa Serikali kusafirisha mwili huo kwani haina bajeti ya masuala hayo na kwamba yeye atachangia kama Watanzania wengine.
Habari zaidi zinasema Serikali ya China imekataa kumsafirisha marehemu kutokana na kifo hicho kutokuwa cha kawaida (natural death).
“Manongi aliwaambia ndugu wa marehemu Tanzania kuwa kampuni aliyowasiliana nayo inaweza kusafirisha mwili huo kwa Dola za Marekani 40,000 au 45,000,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kinapasha pia kuwa,  Mwambata huyo aliwasiliana na mwajiri wa marehemu (Wizara ya Kilimo) kuhusu kumsafirisha na mwajiri akakataa kwa sababu marehemu alikuwa mikononi mwa Serikali ya China.
“Alitaka ndugu wawajibike kuusafirisha mwili hadi nyumbani kwao Shinyanga kwa mazishi,”kilisema.
Chanzo hicho kinaeleza kuwa, Mwambata pia aliwaeleza ndugu kuwa chuo alichokuwa akisoma kilisema hakiwezi kuusafirisha mwili kutokana na ukubwa wa gharama lakini kinaweza kuuchoma na kusafirisha majivu.
Gazeti hili liliwasiliana na Mwambata huyo, lakini alipokuwa akipokea simu yake  na mwandishi anamsikia lakini kwa upande wake alikuwa hasikii hivyo kuitika tu “haloo, haloo…”
Alipotumia ujumbe mfupi wa maneno, alijibu kuwa simu yake imeshindwa kuutambua ujumbe huo kwani maandishi yalikuwa hayasomeki.
Chanzo: Mwananchi.

</

No comments:

Post a Comment