Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
anadaiwa kutumia ujanja katika wasifu na elimu yake ambapo katika maisha yake
ya kielimu ametumia majina manne tofauti.
Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake
halisi ambalo alilisomea mpaka alipohitimu
darasa la saba kwa mara ya kwanza 1988, lakini kutokana na kwamba hakufaulu
kwenda sekondari alirudia darasa hilo .
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takriban miezi mitatu sasa
umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba katika Shule ya Msingi Rukwa
ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu Hassan.
Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la saba kwa mara ya
pili, alibadili jina hilo
(kutoka Hamimu Hassan) na kuwa Hamimu Augustino ambalo aliendelea nalo wakati
akisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day)
mwaka 1990.
Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam alipuuza
tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama za kisiasa zinazofanywa na maadui zake.
Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa
akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule.
“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20
kuuliza swali kama hilo .
Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo
na kuongeza:
“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa Mbunge, tulivyokuwa
bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu walisambaza huu uvumi na
nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu, wakaviona.”
Waliomfundisha
Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu waliofanya kazi
naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa, maelezo yao yanathibitisha
mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati tofauti pia ngazi mbalimbali za
kielimu.
Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu kidato cha nne,
alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea ambako alisoma kati ya
1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu Mulugo.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi ulibaini kuwa
Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena jina pale alipotumia
cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi ya kufundisha katika Shule
ya Sekondari ya Southern Highlands.
Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo ili kumshawishi
mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni marehemu), kumpa
nafasi ya kufundisha shuleni hapo.
“Mulugo alilazimika kutumia cheti cha rafiki yake aliyekuwa
akiitwa Dick Mulungu ambaye alipata daraja la pili katika Shule ya Sekondari ya
Songea Boys, hivyo ikawa rahisi kwake kupata kazi ya ualimu katika shule hiyo,”
alisema mmoja wa waliofanya kazi naye shuleni hapo (jina tunalihifadhi kwa
sasa).
Aliongeza kuwa Mulugo alianza kama
mwalimu wa kawaida, lakini baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shule (headmaster)
wakati hakuwa hata na cheti cha ualimu. Alichukua nafasi hiyo ya ukuu wa shule
baada ya aliyekuwapo kufariki dunia.
“Unajua wale wahindi (wamiliki) walikuwa ni wafanyabiashara kwa
hiyo hawakufuatilia kiwango cha elimu ndiyo maana walimpandisha tu madaraja
bila kujali kuwango cha elimu,” alisema rafiki yake huyo na kuongeza:
“Nilimshauri aachane na cheo hicho kwani kama
ungefanyika ukaguzi wa Serikali na kumkuta bila vyeti vya ualimu angechukuliwa
hatua, hivyo alinisikiliza na akaachia nafasi hiyo na kujipa cheo cha umeneja
wa shule.”
Suala la uwezo na elimu ya Mulugo liliibua mjadala siku chache
zilizopita baada ya kutoa kauli nchini Afrika Kusini aliponukuliwa akisema Tanzania ni muungano wa nchi mbili ambazo ni Tanganyika na Zimbabwe
badala ya Zanzibar .
Alikotokea
Uchunguzi wa gazeti hili ulianzia katika kijiji alichozaliwa cha
Udinde, Kata ya Kapalala wilayani Chunya mkoani Mbeya na alisoma Shule ya
Msingi ya Rukwa.
Mmoja wa walimu waliomfundisha aliyejitambulisha kwa jina la
Nyoni anasema anakumbuka kwamba Naibu Waziri huyo 1989 na wakati huo alikuwa
akijulikana kwa jina la Hamimu Hassan.
“Mimi nilihamia hapa 1989 nikitokea Shule ya Msingi Kapalala.
Kulikuwa na mwalimu mmoja tu kwa hiyo nikawa wa pili. Namfahamu Mulugo wakati
huo akiitwa Hamimu Hassan. Sijui kabla hapo alikuwa akitumia jina gani,”
alisema Nyoni anayetarajia kustaafu kazi ya ualimu mwakani.
Mmoja wa ndugu wa karibu wa Waziri Mulugo anayeishi kijijini
hapo ambaye hakutaka kutajwa jina lake
gazetini alikiri kuwa
awali waziri huyo alikuwa akiitwa Philipo Augustino Mulugo.
“Philipo amesomea hapo Rukwa, ambayo ni Shule ya Msingi na
alikwenda Kijiji cha Mkulwe kabla ya kwenda Mbeya kuwa Mwalimu. Sijui kama
alirudia shule,” alisema ndugu huyo.
Mkazi mwingine wa kijijini hapo, Peter Kayuti alikiri kumfahamu
Waziri Mulugo tangu enzi za utoto na kwamba alirudia darasa la saba, lakini
alisema hakumbuki jina la pili alilolitumia. “Ni kweli Philipo alirudia shule,
lakini sijui kama alitumia jina jingine zaidi ya hilo la sasa,” alisema Kayuti.
Mwalimu aliyemfundisha katika Shule ya Sekondari Mbeya ambaye
pia aliomba jina lake
lihifadhiwe , alikiri
kumfahamu kwa jina la Hamimu Augustino, lakini akasema hafahamu lilibadilika
lini.
“Ni kweli, nilimfundisha Waziri Mulugo na alikuwa akiitwa Hamimu
Agustino. Sidhani kama ni jambo geni kwa wanafunzi hasa wa zamani kurudia
shule… Zamani ilikuwa kawaida kwa kuwa shule zilikuwa chache. Sijui
alibadilisha jina hilo lini, lakini hilo ni suala la kisheria
tu,” alisema mwalimu huyo.
Utata wa majina
Mwalimu mwingine aliyewahi kufanya kazi na Waziri Mulugo katika
Shule ya Southern Highlands alisema waziri
huyo alikuwa na tabia ya kuchanganya majina yake ya awali ili kuficha cheti
alichoombea kazi.
“Yule alikuwa mjanja sana ,
ndiyo maana ukiangalia kadi zake zilikuwa na majina mengi tu na yana badilika.
Leo atasaini barua kwa jina hili kesho lile. Mara utaona ameandika kifupisho
cha PHDA, yaani Philip Hamimu Dick Agustino, mara Mulungu EDM, mara Mulugu D.
Philip,” alisema mwalimu huyo na kuongeza:
“Amekuwa akijaribu kulibadilisha jina la Mulungu kuwa Mulugu
mwisho amelipeleka kuwa lake la awali la Mulugo. Yote hayo ni kuficha tu ukweli
kwamba alitumia cheti cha Dick Mulungu,” alisema mwalimu huyo.
Mmoja wa wakuregenzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
(jina tunalihifadhi) alisema: “Ili mwalimu wa
sekondari awe headmaster (mkuu wa shule) ni lazima awe na shahada ya kwanza
kutoka kwenye chuo kikuu kinachotambulika. Anatakiwa pia kuwa na uzoefu wa kazi
wa miaka isiyopungua minane.”
Kuhusu kughushi vyeti mkurugenzi huyo alisema, ikigundulika kuwa
mwalimu ameghushi cheti anafukuzwa kazi mara moja, lakini alikiri kwamba katika
shule binafsi inawezekana walimu wasio na sifa wakapenya, lakini wakaguzi
wakibaini hutoa maelekezo wafukuzwe.
“Kwanza siku hizi ili mwalimu
aajiriwe ni lazima akabidhi vyeti vyake wizarani na hupelekwa Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta) ili kuhakikiwa. Zamani ukaguzi haukuwa makini kwa
hiyo inawezekana kuna watu wasio na sifa walipenya,” alisema.
Kuhusu kurudia darasa la saba, alisema sheria haijawahi kuruhusu
watu kurudia darasa la saba na kwamba wale waliorudia hutumia mbinu zao kufanya
hivyo.
“Sheria haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la saba. Ni kweli
wengi wamerudia sijui wanatumia mbinu gani, lakini hairuhusiwi. Ukishafanya
mtihani wa darasa la saba mara moja ndiyo basi,” alisema mkurugenzi huyo.
Msemaji wa wizara hiyo, Mtandi Bunyanzu kwa kila swali
aliloulizwa alisema hana uhakika hivyo asingeweza kutoa jibu lakini kwa suala
la kughushi vyeti, alisema ni kosa la jinai siyo kwa walimu tu bali kwa kila
mtu atakayebainika.
“Kughushi vyeti ni kosa la jina siyo kwa walimu tu, hata waandishi
wa habari,” aliongeza Bunyanzu.
Kwa upande wake, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) halikuwa
tayari kutoa matokeo ya mitihani ya Mulugo na badala yake msemaji wa baraza hilo John Nchimbi alisema
matokeo hayo ni siri ya mtahiniwa na hawezi kupewa mtu mwingine.
Chanzo: Gazeti Mwananchi
No comments:
Post a Comment