Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) limeteua waamuzi kutoka Angola
kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania
(Taifa Stars) na Morocco
(Lions of the Atlas). Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam .
Ivory Coast
ndiyo
inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne na kufuatiwa na
Taifa Stars yenye pointi tatu.
Mwamuzi wa mechi hiyo ni Helder
Martins de Carvalho wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Inacio Manuel Candido
huku Ricardo Daniel Cachicumi akiwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa
mezani (fourth official) ni Antonio Muachihuissa Caxala.
Waamuzi hao watawasili nchini saa
1.20 usiku Machi 22 mwaka huu kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Luanda , Angola
kupitia Nairobi , Kenya .
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa
David Fani kutoka Botswana
anatarajiwa kuwasili Machi 22 mwaka huu saa 1.45 usiku kwa ndege ya South
African Airways.
Naye mtathmini wa waamuzi (referee
assessor) Neermal Boodhoo kutoka Afrika Kusini atawasili nchini Machi 22 mwaka
huu 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.
MECHI YA RUVU SHOOTING, YANGA
YAINGIZA MIL 62/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu
Shooting na Yanga iliyochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 62,228,000
kutokana na watazamaji 10,929.
Viingilio katika mechi hiyo namba
146 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 vilikuwa sh. 5,000,
sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh.
14,336,764.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh.
9,492,406.78.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia
15 ya uwanja sh. 7,289,880.48, tiketi sh. 4,136,390, gharama za mechi sh.
4,373,928.29, Kamati ya Ligi sh. 4,373,928.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa
Miguu (FDF) sh. 2,186,964.14, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA)
sh. 850,486.06 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.
850,486.06.
TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI KUIWINDA MOROCCO
Taifa Stars imeanza kambi jana jioni
(Machi 16 mwaka huu) ambapo wachezaji 14 kati ya 23 walioitwa wameripoti na
kufanya mazoezi leo asubuhi chini ya Kocha Kim Poulsen.
Wachezaji walioripoti ni nahodha
Juma Kaseja kutoka Simba na msaidizi wake Aggrey Morris wa Azam, Erasto Nyoni
(Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo
(Simba), Shomari Kapombe (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Wengine ni Athuman Idd (Yanga),
Amri Kiemba (Simba), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mrisho
Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).
Wachezaji Hussein Shariff, Issa
Rashid na Shabani Nditi ambao timu yao
ya Mtibwa Sugar jana ilicheza mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mjini Turiani
wataripoti kambini leo jioni.
Kikosi hicho kitakamilika Jumanne
asubuhi baada ya wachezaji walio katika kikosi cha Azam nchini Liberia kwenye
mechi ya Kombe la Shirikisho kurejea nchini. Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu
wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC) wanatarajiwa
kutua nchini kesho usiku.
Chanzo: TFF
No comments:
Post a Comment