Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Iddi, akiangalia waya wa umeme aina ya shaba ambao
amezuia mauzo yake hadi uongozi wa kiwanda cha sukari utapokaa pamoja na Wizara
ya fedha kufikia maamuzi, kutokana na waya huo kuuzwa chini ya thamani na baadhi
ya maafisa wa Serikali. Thamani halisi ya waya huo inakadiriwa kuwa ni
Tsh300Millioni lakini umeuzwa kwa Tsh.2.5Millioni tu.
KATIKA hali isiyo ya kawaida waya wenye
thamani ya zaidi ya Tsh300Millioni mali
ya Serikali ya mapinduzi Zanzibar
umeuzwa kwa Tsh.2.5Millioni na baadhi ya maafisa wa serikali hiyo hali
iliyosababisha makamu wa pili wa Rais Zanzibar kuzuia uuzwaji wa waya huo na kampuni
iliyonunua.
Tukio hilo
limebainika mara baada ya Makamu huyo kutembelea kwenye kiwanda Cha Sukari
kilichopo Mahonda mjini Zanzibar
na kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho, ambacho kiliuziwa waya huo kwa bei
chee.
Balozi Seif alisema zipo hitilafu
zinazotumiwa na baadhi ya maafisa wa Serikali katika mauzo ya mali za
Serikali na matokeo yake kusababisha kuitia hasara kubwa Serikali Kuu.
Amesema Mali
za Serikali zimekuwa zikinunuliwa kwa gharama kubwa lakini uuzwaji wake baada
ya matumizi hayalingani na thamani ya mali
zenyewe jambo ambalo hutoa mwanya kwa mali hizo kuuzwa kwa bei ya chini
kabisa.
“ Utashangaa kuona mali za
Serikali hununuliwa kwa gharama kubwa lakini baadhi ya maafisa na watendaji wa
serikali hutumia mwanya wa kujenga hoja ya kuuzwa mali hizo kwa kisingizio cha
kuchakaa na badala yake baadhi yao kujiuzia wenyewe kwa bei wanayoitaka wao
wenyewe bila ya kuzingatia taratibu zilizopo za tenda na mnada”. Alionya Balozi
Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza
Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo
kukaa pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari kuangalia nanma ya matumizi ya
waya huo ambao ulikuwa ukitumiwa na Kiwanda hicho.
Waya huo ulilazimika kufukuliwa na
Uongozi wa Kiwanda hicho baada ya kubainika kuanza kuhujumiwa kwa kukatwa katwa
na baadhi ya wezi kufuatia kutambulikana thamani yake katika masoko ya
Kimataifa.
Mapema Mshauri wa Kiwanda cha Sukari
Mahonda Dr. Hamza Hussein
Sabri alisema Zanzibar
inatarajiwa kujitosheleza kwa Sukari ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka
huu kufuatia uongozi wa Kiwanda cha sukari Mahonda kufanikiwa kupata washirika
zaidi katika kuongeza nguvu ya kuanza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa
matumizi ya Jamii.
Chanzo: Saidpowa blog.
No comments:
Post a Comment