Mzee Kitwana Suleiman Kondo, Mwenyekiti
wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF);Mheshimiwa Joel Bendera, Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro; Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro;
Profesa Hamza Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha
Morogoro; Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na Jumuiya
mliohudhuria; Wageni waalikwa; Mabibi na Mabwana;-
Niruhusuni niungane na wenzangu walionitangulia kumshukuru Mwenyezi
Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa.
Nakushukuru sana
Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro na viongozi
wenzako kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya ufunguzi wa
jengo la Kitivo cha Sayansi katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro.
Mmenipa heshima kubwa ya kuwa sehemu ya historia ya Chuo hiki. Kwa kweli,
nimefarijika sana
kuona Chuo chetu kinazidi kupata mafanikio ya kutia moyo hasa ukizingatia
ukweli kwamba kina muda mfupi tu tangu kuanzishwa kwake. Ndugu Mkuu wa
Chuo;
Natoa pongezi nyingi kwako, Makamu Mkuu wa Chuo na wale wote
walioshiriki kubuni wazo la kuwa na jengo la Kitivo cha Sayansi na kufanikisha
ujenzi wake. Juhudi zao na moyo wao wa kupenda maendeleo ndio umetufanya sisi
kujumuika hapa leo kushuhudia mafanikio haya. Hakika ni jambo la kujivunia.
Pia, nawapongeza sana
Wajenzi na Mhandisi Mshauri kwa kazi nzuri waliyofanya ya ujenzi wa jengo hili.
Sote tunaliona jengo lilivyojengwa vizuri na kwa namna yake linapendezesha
mandhari ya Chuo.
Kwa namna ya pekee napenda kwa niaba yenu nitoe shukrani zangu za
moyoni kwa taasisi ya Al-Barakah kwa kufadhili ujenzi wa jengo hili. Asanteni sana kwa ukarimu wenu na
upendo mkubwa mliouonesha kwa nchi yetu na watu wake. Naomba taasisi nyingine
na watu binafsi waige mfano huu mzuri wa kusaidia miradi mbalimbali
inayonufaisha jamii. Tukumbuke ule msemo wa wahenga kuwa “kutoa ni moyo, usambe
si utajiri”.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Mabibi na Mabwana;
Kwa miaka mingi madhehebu ya dini na mashirika ya dini yamekuwa washirika
muhimu sana wa
Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Yamekuwa
yanajihusisha na kutoa huduma kwa jamii kama
vile afya, elimu na nyinginezo. Kwa ajili hiyo watu wengi sana nchini wamenufaika na wanaendelea
kunufaika na huduma zinazotolewa na mashirika ya dini.
Kwa miaka mingi mashirika na taasisi za madhehebu ya dini ya
Kikristo ndiyo yaliyokuwa yakionekana kutoa huduma hizo. Kwa upande wa
Waislamu, ukiacha Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, mchango umekuwa mdogo sana . Ni jambo la faraja
kubwa kuona Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF) ikionyesha njia. Kwa
kumiliki na kuendesha Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro kwa ufanisi, MDF
inatoa mchango muhimu katika kuendeleza elimu ya juu na maendeleo nchini. Idadi
kubwa ya wanafunzi waliofuzu masomo yao
na waliopo katika Chuo hiki tangu kilipoanzishwa mwaka 2005 ni ushahidi tosha
wa kazi nzuri inayofanywa na MDF. Hongereni sana . Tunawaombea kwa Mola mpate mafanikio
makubwa zaidi miaka ya usoni kwa upande wa elimu na huduma nyingine muhimu.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Katika kipindi cha miaka saba sasa, Serikali yetu imeongeza sana uwekezaji katika
upanuzi wa elimu tangu ya awali hadi elimu ya juu. Tumeamua kufanya hivyo kwa
sababu vijana wengi waliokuwa wanastahili kupata elimu ya awali, msingi,
sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwa hawapati. Tanzania
ni kubwa kuliko Kenya na Uganda kwa eneo
na idadi ya watu lakini ndiyo tuliokuwa na idadi ndogo ya wanafunzi kwa ngazi
zote hizo. Kwa mfano, mwaka 2005 idadi ya wanafunzi waliokuwa Chuo Kikuu nchini
Kenya ilikuwa 108,407, Uganda 88,360 na kwa baadhi ya nchi za SADC kama vile Afrika Kusini idadi hiyo ilikuwa 717,973.
Wakati wenzetu wakiwa na idadi hiyo, sisi tulikuwa na wanafunzi 40,719 tu
katika vyuo vikuu nchini. Hali ilikuwa hivyo pia kwa elimu ya sekondari. Kenya ilikuwa na wanafunzi925,341, Uganda 619,519 na Afrika Kusini 4,186,882wakati Tanzania
ilikuwa na wanafunzi 524,325tu waliokuwa katika shule za sekondari.
Tuliona hali hii haikubaliki hivyo tukaamua hatuwezi kuiacha
iendelee. Tukaamua kudhibiti. Tukachukua hatua tulizochukua za kupanua elimu
katika ngazi zote. Matokeo ya uamuzi huo ni kwamba vijana wanaopata fursa ya
kupata elimu katika ngazi zote wamekuwa wengi kuliko wakati mwingine wo wote
katika historia ya nchi yetu, tumewafikia na kuwapita majirani zetu. Kazi kubwa
tunayoendelea nayo sasa ni kuwekeza katika kuimarisha ubora wa elimu waipatayo
vijana wetu kwa kuongeza walimu, vifaa vya kufundishia, vitabu na huduma
nyinginezo. Inshallah hata kwa dhamira yetu, hii njema Mola atatuwezesha.
Mwanzo mgumu lakini hatma itakuwa nzuri.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Kufuatia juhudi hizo, idadi ya wanafunzi waliopo kwenye vyuo vikuu
nchini imeongezeka sana ,
kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi wanafunzi 166,484 mwaka 2012. Kwa
upande wa sekondari mwaka 2011 tulikuwa na wanafunzi milioni 1.79 na wenzetu wa
Kenya
walikuwa na wanafunzi milioni 1.77. Haya ni mafanikio makubwa.
Serikali itaendelea kuwekeza kwenye upanuzi wa fursa za elimu na
ubora wake. Hata hivyo ushiriki wa wadau wengine kuunga mkono juhudi za
serikali ni jambo muhimu sana .
Tumeweka mazingira mazuri kwa wadau hao kufanya hivyo na mafanikio yanaonekana
wazi. Kama nilivyokwishasema awali, mashirika
ya dini yamekuwa wadau wa kutumainiwa na mchango wao uko wazi. Unajieleza
wenyewe. Kwa mfano, katika vyuo vikuu 49 vilivyopo nchini, vinavyomilikiwa na
umma ni 14 tu. Vyuo vikuu 24 vinamilikiwa na mashirika ya dini na 11 na sekta
binafsi.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa na muhimu
unaotolewa na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na sekta binafsi.
Ninyi mmekuwa washirika wazuri na wa uhakika katika kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo ya elimu katika nchi yetu. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali
itaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nanyi ili kuwawezesha vijana na
Watanzania wengi zaidi waweze kupata elimu. Uamuzi wa kufanya utaratibu wa
mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu uhusishe wanafunzi wa vyuo visivyokuwa vya
umma ni moja ya mambo mengi muhimu yanayofanywa na Serikali kuthibitisha usemi
wangu huo.
Tulipoingia madarakani mwaka 2005 tulifanya mambo mawili muhimu
kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Kwanza
uamuzi kwamba, mikopo itolewe kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma na vile
visivyokuwa vya serikali. Kabla ya hapo ilihusu vyuo vya umma pekee. Pili
kwamba, kila mwaka tuongeze fedha zinazotengwa kwa ajili ya Mfuko huo ili idadi
ya wanafunzi wanaonufaika iongezeke. Tulikuta Mfuko ukiwa na shillingi billioni
56.1 unanufaisha wanafunzi 16,345 mwaka 2005. Tukaongeza kila mwaka na katika
mwaka huu wa fedha (2012/13) tumetenga shillingi bilioni 345 zinazowanufaisha
wanafunzi 98,772.
Tutaendelea kuongeza fedha katika Mfuko huo ili wanafunzi wengi
zaidi wanufaike na hata ifikie siku moja tuweze kuwakopesha wote bila ya kujali
sifa ya uwezo wa wazazi au walezi kulipa ada. Kwa kasi tuliyonayo na kwa jinsi
tunavyozidi kufanikiwa katika kukusanya mapato ya serikali, naamini miaka
michache ijayo tunaweza kufikia lengo hilo .
Nawasihi Bodi ya Mikopo iwekeze katika kuimarisha uwezo wa kuwafuatilia
waliokopeshwa kulipa mikopo waliyopewa. Matamanio yangu ni kuwa fedha
zilizotolewa zizunguke ili tupunguze kiasi kinachotolewa na bajeti ya serikali
kila mwaka.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Mabibi na Mabwana;
Niruhusuni nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Mkuu wa Chuo,
Makamu Mkuu wa Chuo, Wahadhiri na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu hiki kwa kazi
kubwa na nzuri muifanyayo ya kuendeleza na kuboresha Chuo. Tumeshuhudia ujenzi
wa jengo nililolifungua leo. Tumeona mafanikio kwa upande wa ongezeko la idadi
ya wanafunzi, walimu, wafanyakazi na fani zinazofundishwa katika kipindi hiki
kifupi cha uhai wa Chuo hiki.
Nimefurahishwa na kufarijika sana
kusikia kuwa ubora wa elimu inayotolewa hapa chuoni ni jambo linalopewa kipaumbele
cha kwanza. Jambo hili ni muhimu sana
kulisisitiza kwani tunataka wahitimu wa Chuo hiki wafanane na wahitimu wa Chuo
chochote kizuri nchini na hata duniani. Ningependa kuona wahitimu wa Chuo hiki
wanagombewa katika soko la ajira. Hili ni jambo linalowezekana. Kinachotakiwa
ni uamuzi wa Baraza na Seneti kuwa iwe hivyo na kuchukua hatua zipasazo. Sina
shaka kuwa mnaweza kufanya hivyo. Hakika mnaweza, na sote kwa umoja wetu
tunaweza.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Nimefurahi sana ,
pia, kusikia kuwa Chuo kinatoa mafunzo ya ualimu. Bila ya shaka mnaelewa kwa
nini nafurahi. Tuna uhaba mkubwa wa walimu nchini hivyo Chuo cho chote
kinachotoa mafunzo ya ualimu hunifurahisha. Endeleeni kuimarisha mafunzo hayo
ili Chuo chenu kitambulike na kukubalika nchini kwa sifa ya kutoa walimu
wazuri. Walimu wa kutoka Chuo hiki wawe wale wanaojua vyema masomo
wanayofundisha, mahiri kufundisha na waadilifu. Naomba pia mtoe kipaumbele cha
juu kwa mafunzo ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati. Mkifanya hivyo,
mtakuwa mnatoa mchango mkubwa katika jitihada za kupunguza uhaba wa walimu wa
masomo hayo nchini. Naamini kitendo cha kuzindua Jengo la Kitivo cha Sayansi,
kilichofanyika muda mfupi uliopita kinatoa matumaini ya Chuo Kikuu cha Waislamu
cha Morogoro kuchangia katika jitihada za kupunguza pengo la walimu wa sayansi
nchini.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Nimewasikia mkieleza kwa ufasaha changamoto kubwa na ndogo ambazo
Chuo inakabiliana nazo. Nawapongeza kwa dhati, wewe na viongozi wenzako kwa
ubunifu wenu na hatua mnazochukua kuzikabili changamoto hizo. Nawaahidi msaada
na ushirikiano wangu na wa serikali kwa yale yaliyoko kwenye uwezo wangu na wa
serikali katika kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zinazowakabili.
Nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kutafuta vyuo vikuu rafiki
vilivyoko katika nchi mbalimbali duniani mnavyoweza kushirikiana navyo.
Endeleeni kufanya hivyo kwani vyuo vikuu vingi duniani hufanya hivyo. Hamtakuwa
wa kwanza na wala hamtakuwa mnafanya jambo la kustaajabisha. Mnaweza, mkipenda,
kuwaomba Mabalozi wetu waliopo katika nchi mbalimbali duniani wawasaidie. Ni
wajibu wao kufanya hivyo kwani kusaidia kusukuma maendeleo ya hapa nchini
kutoka huko waliko ndilo jukumu lao la msingi. Vile vile, nimefurahishwa na
mipango yenu ya baadaye ya kuwa na matawi katika mikoa mbalimbali nchini. Hongereni
kwa uamuzi wenu wa busara. Lazima Chuo kitanuke kwa maana ya kuwa kikubwa
zaidi, makao makuu na kwa kuwa na vyuo vishiriki na shule au vitivo sehemu
mbalimbali nchini.
Ndugu Mkuu wa Chuo;
Kazi iliyo mbele yenu ni kubwa, hivyo ni vyema kuweka mikakati
mizuri na mipango thabiti ya utekelezaji na ufuatiliaji wa dhamira yenu hiyo
njema. Rai yangu kwenu ni kuwaomba muwe wabunifu zaidi hasa katika kutafuta
vyanzo vingine vya mapato vitakavyosaidia Chuo kujiendesha bila kutegemea ada
peke yake. Chuo kiangalie uwezekano wa kufanya shughuli zitakazowaingizia
mapato kama vile kufanya shughuli za kutoa
ushauri. Pia muangalie uwezekano wa kuwekeza wenyewe kwenye miradi ya kiuchumi
au kwa kushirikiana na wawekezaji katika baadhi ya maeneo.
Kuhusu nafasi mbili za ufadhili nilizopewa na Chuo kikuu cha Tun
Abdul Razak cha Malaysia ,
nitafuatilia kujua kilichoendelea na kinachoendelea. Je, nafasi hizo bado zipo?
Zikiwepo, nitawasiliana na wahusika waangalie uwezekano wa kuwapeni. Kama zimeshagawiwa basi tusubiri safari ijayo. Kwa
masuala ya ardhi na maombi mengine nimeyasikia, yaleteni tuangalie namna ya
kusaidiana.
Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo, na
Wafanyakazi wote wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;
Napenda kuwakumbusha kuwa mnayo dhamana kubwa na wajibu mkubwa na
wa kihistoria. Ule ukweli kwamba ni mara ya kwanza kwa Taasisi ya Waislamu
wazawa kuwa na Chuo Kikuu inawapeni wajibu maalum wa kuhakikisha Chuo
kinafanikiwa. Ni mtihani na changamoto ya aina yake kuthibitisha kuwa Waislamu
nao wanaweza kuwa na Chuo kizuri na chenye kutoa elimu ya ubora wa hali ya juu.
Kwa sababu hiyo hamna budi kuhakikisha kuwa mna mipango mizuri ya kujenga Chuo
cha hadhi na ubora wa hali ya juu. Ihakikishwe kuwa mipango hiyo inatekelezwa
kwa ukamilifu.
Aidha jumuiya yote inao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu,
maarifa na weledi ili dhima hiyo ya Chuo iweze kutimizwa kwa ukamilifu.
Timizeni wajibu wenu ipasavyo ili jina la Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro
likue haraka. Sifa yake isambae na kuvuma kote nchini. Chuo kifanye vizuri ili
wanafunzi waone fahari kuwa wahitimu wa Chuo hiki. Chuo ambacho, wazazi wapende
kuleta vijana wao kuja kusoma hapa. Kwa jinsi Mkuu wa Chuo alivyoeleza, mimi
nina imani mnaweza, fanyeni kweli.
Ndugu Wanafunzi wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;
Naomba wote muone fahari ya kuwa wanafunzi katika Chuo cha
kihistoria hapa nchini. Nawasihi mjitume kwa kadri ya uwezo na vipaji
mlivyopewa na Mwenyezi Mungu mfanikishe kile kilichowaleta. Jifunzeni kwa bidii
mfaulu vizuri ili mkihitimu muwe kielelezo kizuri cha mafanikio na ubora wa
Chuo Kikuu Cha Waislamu cha Morogoro. Muwe Mabalozi na kioo cha ufanisi wa Chuo
hiki. Nawasihi mjiepushe na mambo yatakayowapunguzia muda au kuwaondoa katika
shughuli ya msingi iliyowaleta hapa ya kujifunza mpate digrii katika fani
mliyochagua mwenyewe kuisomea. Vishawishi ni vingi na wapo watu wengi
wanaopanga kuwashawishi mtumie muda wenu adhimu kufanya wanayoyataka wao ambayo
mkishiriki huwatoa kwenye malengo na kutekeleza yao . Mambo ya dunia ya nje ya Chuo ni mengi
huna budi kutambua lipi ufanye na lipi usifanye na kwa wakati gani!
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu ni mtu mzima, si mtoto. Lazima ujue kuwa
unawajibika kwa kila unaloamua na kutenda. Amua kuwajibika vizuri. Fikiri kabla
ya kutenda, changanua lipi ni lipi kabla ya kufanya uamuzi wa kile unachotaka
kufanya. Wakati wote uongozwe na busara na hekima na siyo jazba na ushabiki wa
matakwa ya kundi. Kama ni jema fanya na kama
si jema usifanye. Kwanza tambua wewe ni nani
na uko hapa kwa ajili gani. Lazima ujue kuwa hatma ya yote uko peke yako.
Utafaulu au kufeli wewe. Utapata shahada wewe na si mtu mwingine. Hakuna ubia
wa kufaulu au kufeli au kiwango cha kufaulu. It will always remain personal.
Katika masomo unanufaika wewe. Shirikiana na wengi lakini usisahau kujali
maslahi yako. Maslahi ya wengi yasiyojumuisha yako, yahoji vizuri kabla ya
kuamua kushiriki au kufanya. Vinginevyo labda kama
umeamua kujitoa muhanga, uwe shujaa. Hata kwa hilo , sijui utakuwa shujaa wa nani.
Mabibi na Mabwana;
Kabla ya kumaliza napenda kutambua na kumshukuru Rais wa Awamu ya
Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa na viongozi wa MDF kwa juhudi zao za pamoja
zilizowezesha Chuo hiki kuwepo. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru
wananchi wanaokizunguka Chuo kwa ujirani mwema na wakazi wa Morogoro kwa ujumla
kwa kukipokea vizuri na kuishi na wanajumuiya wa Chuo hiki kwa upendo mkubwa.
Naomba muendelee na moyo na ushirikiano huo.
Baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunialika. Nawatakia kila la heri na
mafanikio tele.
Asanteni sana
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment