Jana, katika mahubiri yake mafupi, Papa Francis alishangaza
wengi kwa kueleza kuwa binadamu hawana budi kusameheana, kama
ambavyo Mungu amekuwa mwenye huruma kwa wanadamu.
Awali, Papa alijitokeza hadharani katika lango kuu la kuingilia
kanisa hilo la
parokia akiwa amevaa kanzu nyeupe, viatu vyeusi, kuwapungia mkono watu wote,
kisha kupeana nao mikono.
Kisha, alibusu, kuwashika mabegani watoto na kueleza kuwa jukumu
la binadamu ni kupendana.
“Ningependa sisi sote tuwe na ujasiri wa kutembea katika uwepo
wa Mungu,” alisema Papa Francis kwa Kilatini.
Mapema, Papa alifanya maombi binafsi katika Kanisa Kuu la Santa
Maria Maggiore na baadaye alikutana na watoto na wasafiri waliokwenda
kumsalimia.
Papa, pia ameanza kazi ya uteuzi wa maofisa wa juu wa Vatican , ingawa orodha hiyo haijakamilika wala kuwekwa
wazi.
Jumatano usiku muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwake,
aliusalimia umati wa watu waliofurika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro akitoa
wito wa unyenyekevu na kuwaomba waumini wamwombee baraka kabla yeye
hajawabariki.
Alhamisi, Papa Francis alirudi kwenye makazi ya watumishi
yaliyopo mjini Rome
alipokuwa akiishi mbele ya jengo la mikutano ulimofanyika uchaguzi uliomweka
madarakani.
“Alifungasha mizigo yake na kwenda kulipia chumba alichofikia
ili kuwa mfano bora.
“Pia, alivunja utamaduni wa kwenda kuwasubiri makardinali
waliokwenda kumpa pongezi, badala ya kukaa kwenye kiti cha enzi,” alisema
msemaji wa Vatican ,
Padri Federico Lombardi.
Ijumaa alikutana na makardinali 106 wakiwamo wale ambao
hawakuingia kwenye mkutano wa uchaguzi.
Jumamosi, Papa alikutana na mamia ya waandishi wa habari wa
kimataifa na kuweka msimamo wa kanisa lake.
Siku ya Ijumaa, anatarajiwa kumtembelea mtangulizi wake , Papa
Benedict XVI, eneo la Castel Gandolfo, nje kidogo ya Mji wa Rome.
Kumtembelea mtangulizi wake kunaelezwa kuwa ni muhimu kwa kuwa
kuwepo kwake kunaweza kuleta upinzani katika madaraka yake.
Papa Francis anatarajia kusimikwa rasmi Jumanne katika misa ya
uzinduzi ambayo itahusisha maelfu ya waumini.
Ingawa alitajwa kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka
2005 uliomweka madarakani Papa Benedict XVI, baadhi ya watu walitabiri kuwa
papa atakayefuatia atatoka nje ya Ulaya.
Akiwa mzaliwa wa Amerika ya Kusini, anaonekana kuwa mtu
aliyeshika mno mafundisho na mwenye misimamo.
Hali hiyo inamfanya kuonekana kama mtu wa mabadiliko katika
utendaji wa Vatican akisaidiwa na makardinali
waliomzunguka.
Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanasema Papa Francis
anakabiliwa na changamoto nyingi katika uongozi wake hasa kwa kuwa kanisa hilo linakabiliwa na
kashfa za unajisi zilizowakumba makasisi wake na tuhuma za rushwa.
Changamoto nyingine inayomkabili ni pamoja na suala la wanawake
kupewa upadri, kuibuka kwa madhehebu na kupukutika kwa waumini kunakoendelea
katika sehemu mbalimbali duniani, ikiwamo Ulaya na Marekani.
Papa Francis au Kardinali Jorge Mario Bergoglio, alizaliwa
Desemba 17, 1936 mjini Buenos Aires, Argentina. Ni mfuasi wa Shirika la
Wajesuiti tangu mwaka 1969 na alisomea Argentina na Ujerumani. Alipewa
ukardinali mwaka 1998.
*Elias Msuya kwa msaada wa mashirika ya habari ya kimataifa.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment