Friday, March 8, 2013

Simba yapata wa kukaimu nafasi ya Kaburu.

Wanahabari pamoja na wajumbe wa Simba wakiwa katika mkutano leo mchana wakati kaimu makamu mwenyekiti Mzee Kines alipokuwa akizungumzia suala la kujiuzulu kwa baadhi ya viongozi wa Simba.


Mabingwa watetezi ligi kuu ya vodacom Tanzania bara Simba SC, wameunda kamati maalum ya ushindi iliyo chini ya uenyekiti wa malkia wa nyuki El Kharus kabla ya kukutana na wagosi wa kaya siku ya jumapili hii.

Akitoa taarifa hizo ofisi za timu hiyo mtaa wa msimbazi katika mkutano na waandishi wa habari mchana huu kaimu makamu mwenyekiti Joseph Itangale ;Mzee kines’ alisema baada ya kujiengua makamu mwenyekiti Godfrey Nyange ‘Kaburu’ na mwenyekiti wa kamati ya usajili Zacharia Hans Poppe timu ya Simba bado ipo imara ya tayari imeunda kamati ya ushindi.

“Sisi hatuna matatizo, hao walioamua kujiondoka kwenye uongozi watabaki wanachama wa kawaida na kwa kudhihirisha hilo leo jioni tutakwenda kurudisha uhusiano wetu na tawi la mpira pesa.

“Timu ipo imara na tutahakikisha mechi nane zilizobaki kukamilisha msimu Simba tunashinda zote chini ya kamati ya ushindi inayoongozwa na Rahma Al Kharoos,” alisema mzee Kines.

Nae kocha msaidizi wa Simba Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ amesema timu yake imejiandaa vizuri na anawaahidi mashabiki wa Simba wasivunjike moyo na matokeo mabaya, kwani kujiuzulu siyo dawa ya kuondoa matokeo mabaya.

“Nimesikia Coastal Union wanasema watatufunga mapema wana haki ya kusema hivyo maana nao wapo ligi kuu na sisi tutacheza mpira mzuri maana wachezaji wote 25 wapo katika hali nzuri na 11 watakaopata bahati ya kuanza kikosi cha kwanza tuna hakika watacheza vizuri.

“Sote tunamtegemea Mungu na tunamuomba, kubahatika ama kutobahatika yote ni mipango yake. Hakuna haja ya kumlaumu Mungu kwa matokeo mabaya maana kuna watu wanamuomba Mungu tangu wamezaliwa lakini hawajawahi kuokata hata laki moja lakini hawakati tamaa,” alisema Julio.

Julio aliongeza “Mimi ndie kocha bora baada ya kufariki Mzirai na kama huamini angalia timu zote nilizowahi kufundisha namna mafanikio waliyopata. Hivyo najiamini na ninaamini mechi ya Coastal Union tutashinda.”

Timu ya Simba itacheza na Coastal Union kutoka Tanga katika uwanja wa taifa siku ya jumapili tarehe 10 mwezi huu katika mechi ya ligi kuu ya voadacom Tanzania bara ambapo mshindi wa mechi hiyo ndie atakaeshika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi wenye timu 14.

Simba inacheza mchezo wake wa 19 wakiwa na historia ya matokeo mabaya hivyo mashabiki wa soka Tanzania wanaamini wekundu hao wa mtaa wa msimbazi walioanza kucheza soka mwaka 1936 wana kazi kubwa ya kurudisha heshima yao kisoka na kutetea ubingwa walioupata msimu uliopita.
 HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
8 March, 2013
Dar es Salaam, Tanzania

No comments:

Post a Comment