Thursday, March 28, 2013

Waziri Kigoda azomewa Mtwara...


Kigoda na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, walikutwa na kadhia hiyo walipokuwa wakihutubia wananchi wa Mtwara katika Uwanja wa Umoja.

Mawaziri hao pamoja na Balozi wa Nigeria Nchini, Nshaya Manjabu walikuwa mkoani Mtwara kwa ajili ya makabidhiano ya vifaa vya ujenzi wa kiwanda cha saruji kinachotarajiwa kutumia malighafi ya gesi asilia.

Itakumbukwa kuwa Januari 30, mwaka huu Waziri Mkuu Mizengo Pinda alituliza jazba za wakazi wa Mkoa wa Mtwara baada ya kueleza jinsi watakavyonufaika na gesi itakayozalishwa mkoani humo kabla ya kusafirishwa kwa bomba hadi Dar es Salaam.

Katika mkutano wa majumuisho, Pinda alisema gesi ghafi haitosafirishwa kwa njia ya bomba na kwamba kiwanda cha kusindika gesi kitajengwa mkoani humo ili mabaki yatumike kama malighafi ya viwanda.

Hata hivyo, jana ilionekana kama wakazi hao wamekwishasahau mipango waliyoelezwa na Pinda, hivyo kusababisha kadhia hiyo kwa RC na mawaziri katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa.

Mkutano huo ulitanguliwa na hafla ya Dk Tizeba kumkabidhi Dk Kigoda makontena 38 yenye vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote pamoja na magari ya kubebea mizigo.

Halfa hiyo ambayo ilifanyika kwenye Bandari ya Mtwara pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Dangote, Deva Kumar. Ujumbe huo pia ulitembelea Kijiji cha Msijute, Kata ya Namayanga kitakapojengwa kiwanda cha Dangote, kisha kuzungumza na wanakijiji.
Viwanja vya Mashujaa.

Mkuu wa Mkoa, Simbakalia ndiye aliyefungua pazia la kuzomewa baada ya kupanda jukwaani kwa lengo la kutoa utangulizi wa ziara hiyo. Wananchi walianza kutawanyika na kwenda kusimama mbali na eneo la mkutano huku wakipaza sauti: “hatukutaki…haitoki.”

Hata pale alipojaribu kusema; “Mtwara oyee” alijibiwa, “Haitokiii” na wengine wakisema: “hatukutakii...” hali iliyompa ugumu kiongozi huyo kuendelea na hotuba yake.

Kuona hawezi tena kuendelea, alimkaribisha Dk Tizeba ambaye naye alikutana na kadhia hiyo, kwani alipoanza kusalimia wakazi wa Mtwara, alipokewa kwa majibu “haitoki...”. Baada ya majibu hayo, akasema “Mtwara oyeee”,ndipo kukaibuka kikundi cha wananchi waliokuwa wakiimba “Haitokiii…Haitokiii…Haitokiii”

Zomea zomea hiyo iliyoambatana na mabango yenye ujumbe wa kupinga mradi wa kusafirisha gesi, ulisababisha kukosekana kwa utulivu wakati wote wa hotuba yake.
Pamoja na kelele za wananchi hao, hakukupoteza mwelekeo kwani aliendelea kuwaeleza wananchi kwamba hivi sasa Serikali inaendelea kuboresha barabara zinazoingia mkoani humo ili bandari iweze kufanya kazi vizuri.

Dk Tizeba alisoma moja ya mabango lililoandikwa “Gesi ndiyo roho yetu Wanamtwara” na alionyesha kuunga mkono madai ya wananchi ya kutaka kufaidika na rasilimali hiyo. Hata hivyo alijibiwa “siasa hizoo...hatutakiii”
Dk Tizeba alisema tayari wawekezaji 12 wameomba kuwekeza katika Bandari ya Mtwara na kutoa wito kwa wengine wenye nia ya kufanya hivyo kujitokeza.

Dk Kigoda kwa upande wake lipopanda jukwaani mambo yakawa kama ilivyo kwa watanguzi wake, hali iliyomlazimu kuongea kwa muda mfupi kutokana na kukosekana kwa utulivu.

“Madai ya wananchi wa Mtwara ni ya msingi sana, wanataka kufaidika na rasilimali inayotoka katika eneo lao… Serikali tumeamua kushawishi wawekezaji kujenga viwanda Mtwara ili wananchi wafaidike…lakini suala la kuzuia gesi kwenda Dar es Salaam siyo sahihi kwa sababu gesi ipo nyingi,” alisema Kigoda huku wananchi wakimpinga hali iliyomlazimu kukatisha hotuba yake.

Imeandikwa na Abdallah Bakari, Mary Sanyiwa na Haika Kimaro
Chanzo: Mwananchi.
; ma4 � -

No comments:

Post a Comment