Mama Sitti Bint Saad akipiga tari, ala aliyoipenda sana na kumudu kuipiga kiustadi wakati wa uhai wake.
Na Hafidh Kido
WANAUME wengi
wanaojishughulisha na Muziki wa Taarab maarufu ‘Mipasho’ huonekana wamepotea
kwa kuchagua burudani inayopendwa na kinamama.
Muziki wa Taarab umechangia
kuongezeka kwa misamiati mingi katika miji ya pwani hasa Dar es Salaam, Tanga
na Zanzibar
ambapo kinadada huitumia kunogesha mazungumzo wenyewe huita ‘kupashana.’
Lakini wengi hawafahamu kuwa
Muziki wa Taarab ulipofika pwani ya Afrika Mashariki katika karne ya 19 mjini
Unguja wanawake hawakuruhusiwa kuimba, kupiga vyombo wala kucheza muziki huo.
Alieleta burudani hii katika Afrika
Mashariki ni Sultan Seyyid Baraghash Bin Said ambae alitawala Zanzibar (1870-1888).
Alikuwa akipenda sana Muziki huu akawa
anaagiza vikundi kutoka Misri ambapo wanaume tu ndiwo walikuwa wakiimba na
kupiga ala zote katika jumba la burudani Beit El-Ajaib.
Mzanzibari wa kwanza
kuonyesha uwezo wa kuimba Taarab alikuwa ni Mohammed Ibrahim, ambapo Sultani
aliagiza apelekwe Misri ili akajifunze kupiga ala na uimbaji ili akiweza
awafundishe wengine na kupunguza gharama za kuagiza vikundi kutoka nje.
Ibrahim, alipokuwa Misri
alijifunza kupiga chombo cha Kanuni ama ‘Ganuni’ ambacho ni chombo kigumu
kuliko vyote kwenye Muziki wa Taarab, ni mfano wa kinanda chenye nyuzi za
chuma, mpaka sasa ni watu wachache sana
wanaojua kucheza chobo hicho.
Baadae Mohammed Ibrahim
alipowafunza Wazanzibari wengine kuimba na kupiga vyombo vya Taarab wakaamua
kuanzisha kikundi cha kwanza cha Taarab Afrika Mashariki kilichitwa ‘Zanzibar
Taarab Orchestra’ baadae kikaitwa (Cultural Musical Club) mpaka sasa kipo na
kinatumika kama chuo cha Taarab mjini Unguja.
Baadae mwaka 1905 kikundi cha
pili cha Nadi Ikhwani Swafaa kikaanzishwa. Ikawa ukoo wa kisultani haupati
gharama tena ya kuagiza vikundi kutoka Misri, kumbuka wakati wote huo wanaume
ndiwo waliokuwa na ruhusa ya kuimba na kupiga vyombo vya Taarab.
Miaka ya 1920 mwanamke wa
kwanza Afrika Mashariki kakata minyororo ya utumwa na kupaza sauti kwa uimbaji
Taarab alikuwa ni Bi Mtumwa Saad maarufu Sitti Bint Saad. Na wakati huo Taarab
ilikuwa ikiimbwa kwa lugha ya kiarabu, ila Kiswahili kilitumika kwa kiasi
kidogo.
Hata hivyo, mashairi
yaliandikwa kwa hati za kiarabu ingawa yalisomeka kwa Kiswahili. Hii ilikuwa
kasumba ya waarabu kwani iliaminika asili ya Muziki huo ni lugha ya kiarabu
hivyo kutumia lugha nyingine ilikuwa ni kama
kuupunguzia ladha.
Zingatia, wakati wote huo
Taarab ilikuwa ikitumika kuwaburudisha mabwanyenye wa kiarabu ‘ukoo wa
kisultani’. Ulitumbuizwa katika kasri la Sultani tu haukuruhusiwa kupigwa
mitaani, yaani haukutumika kwa kupata kipato kama
inavyofanyika sasa.
Sitti Bint Saad huyohuyo ndie
mtu wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kurekodi sauti yake akiimba Taarab nchini
India
katika Studio maarufu kwa wakati huo ‘His Master’s voice’, ingawa vipo vitabu
vingine vinaandika ilikuwa ni kampuni ya ‘Columbia Records’.
Mpaka sasa jina la Sitti Bint
Saad aliefariki June 1950 halisahauliki midomoni mwa wapenzi wa Taarab kwani ndie aliewakomboa
wanawake mpaka sasa Taarab ikiimbwa na wanaume inaonekana ajabu.
HAFIDH KIDO
13 March, 2013
No comments:
Post a Comment