Monday, March 18, 2013

Coastal wakana kumtosa Nsa Job

 Nsa Job akiwa nchini India baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti la kushoto aliloumia mwaka jana kwenye mechi ya ligi kuu dhidi ya JKT Ruvu.

Tarehe 28 October 2012 uwanja wa Chamazi Coastal Union dhidi ya JKT Ruvu Nsa Job aliumizwa vibaya goti lake na kukimbizwa hospitali kabla ya kupelekwa indi siku chache baadae.


NA SOMOE NG`ITU
18th March 2013
Uongozi wa timu ya Coastal Union ya jijini Tanga umekanusha taarifa za kumtelekeza mshambuliaji wake,Nsa Job na pia ikisema nyota huyo ana mkataba na klabu hiyo hadi Mei mwakani. Akizungumza na gazeti hili msemaji wa Coastal Union, Eddo Kumwembe, alisema kuwa wanasikitika kusikia taarifa za kumtelekeza Job wakati uongozi unampa huduma zote muhimu kama wachezaji wenzake wanavyopata licha ya kutocheza. 

Kumwembe alisema kuwa Job ambaye alipelekwa India na timu hiyo kwa ajili ya upasuaji, analipwa mishahara yake kila mwezi na pia motisha. 

Alisema pia mmoja wa viongozi wa timu aliyeko jijini Dar es Salaam, Nassor Binslum, amekuwa akimpa fedha kwa ajili ya kwenda hospitali kila anapohitaji kufanya hivyo.

''Ukweli ni kwamba uongozi wa Coastal unashangazwa sana na taarifa hizo ambazo kwa upande mmoja au mwingine inasemekana Nsa mwenyewe anachangia kuzisambaza,'' alisema Kumwembe. 

Aliongeza kwa kusema kwamba uongozi unamkaribisha mshambuliaji huyo kwa mazungumzo ya kuvunja mkataba wake kama anafikiria kufanya hivyo. Pia alimaliza kwa kuwataka wachezaji wa Coastal wenye mikataba  kutozungumza na vyombo vya habari bila ya ruhusa ya klabu. Nsa hakupatikana kuzungumzia suala hilo 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment