Monday, March 4, 2013

Sakata la katiba ya TFF lafikia hapa....


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema ipo haja kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufikiria upya uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya TFF ya mwaka 2012 na kutaka itumike ya mwaka 2006, kwani hautekelezeki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana, mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema ni muhimu jambo hilo likaangaliwa upya kwa sababu athari zake ni mbaya, na pengine Dk. Mukangara hakushauriwa vizuri kabla ya kufanya uamuzi huo.

“Kamati ya Utendaji ya TFF haitaki kubishana na Mheshimiwa Waziri hata kidogo, ila tunaamini wakati anatamka haya hakufahamu madhara yake, athari zake na ugumu wa utekelezaji wake. Kwa waliomshauri hili, wamemshauri vibaya,” amesema Rais Tenga.

Amesema rai ya TFF kwa Waziri ni kuwaita ili wamweleze ni kitu gani wafanye kunusuru mpira wa miguu wa Tanzania, kwani wanaamini jambo hili litakwisha baada ya kumwelimisha hasa kutokana na ukweli kuwa kabla ya kufanya uamuzi huo hakuwasikiliza.

Katika mkutano huo, Rais Tenga alianza kwa kusema kuwa TFF inaiheshimu sana Serikali, hivyo inaheshimu maagizo yaliyotolewa na Waziri, lakini akaongeza kuwa TFF ina wajibu wa kutoa ufafanuzi juu ya maagizo hayo.

Amesema lengo la kuelezea historia ya TFF ilikotoka ni kubaini migongano ya maagizo hayo na taratibu za TFF ambazo kwa bahati mbaya zinasigana na maagizo hayo.

Rais Tenga amesema TFF ni chombo cha wanachama, ambapo wanachama wake ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, na ina taratibu za kufanya uamuzi kwa mujibu wa Katiba yake na za wanachama wake ambazo zimeidhinishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema si TFF pekee, bali vyama vya nchi zote ambavyo vimeunganishwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), zinaheshimu na kufuata maagizo na miongozi ya shirikisho hilo la kimataifa la mpira wa miguu.

Rais Tenga amesema TFF haitakiwi kuingiliwa katika uongozi na uendeshaji wake, kwani jambo hilo likitokea rungu la FIFA litaiangukia TFF, na madhara yake ni makubwa. Miongozo ya FIFA inasisitiza uhuru wa wanachama wake katika uendeshaji shughuli za mpira wa miguu, na iko kwenye Katiba ya TFF.

“Sheria za nchi ndizo zilizozaa Katiba ya TFF. TFF ni chama kamili kinatakiwa kufanya uamuzi wake ili mradi uzingatie madhumuni ya kuanzishwa kwake. Leo TFF ikiacha mpira wa miguu na kuanza kujishughulisha na gofu, hapo Msajili ana haki ya kuingilia,” amesema Rais Tenga.

Kuhusu maagizo ya Waziri, Rais Tenga amesema kifungu cha 11 cha Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kinazungumzia usajili wa chama, na si marekebisho ya katiba, ingawa kanuni zinahusu marekebisho ambapo ameongeza kuwa uamuzi wa marekebisho ni wa Mkutano Mkuu na si Msajili.
“Ukienda kuomba viza, fomu unapewa na yule anayekupa viza.

TFF tulipowasilisha marekebisho ya Katiba hatukupewa fomu. Msajili akasema sawa. Jambo la kujaza fomu si la TFF, ndiyo maana tunasema ipo haja ya jambo hili kufikiriwa upya.

“Usajili tayari umepita, kwamba Msajili hakutoa fomu, mwathirika anakuwaje TFF? Tunaona ni muhimu jambo hili likaangaliwa upya,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa utaratibu wa kusajili Katiba ya 2006 ambayo ndiyo Waziri ameagiza itumike ulikuwa huo huo uliosajili Katiba ya 2012.

Akizungumzia historia ya TFF kutoka mikononi mwa BMT, Rais Tenga amesema ni zao za Katiba ya 2004 ambayo ilifanyiwa marekebisho ukumbini na kugongwa mhuri na Msajili hapo hapo na kuingia kwenye uchaguzi. Katiba hiyo ndiyo iliyoiondoa BMT kuisimamia TFF.

“Huko ndiko tulikotoka, si kwa kulazimishwa, bali kwa kupewa Katiba ya 2004. Katiba ina utaratibu mzima wa kufanya uamuzi. Maelekezo ya Waziri yamesahau huko tulikotoka siku nyingi. Uhalali wa marekebisho unatokana na ridhaa ya Mkutano Mkuu. Hiyo ni kwa mujibu wa Katiba yenyewe, hakuna nafasi ya BMT,” amesema.

Amesema katika maagizo ya Waziri, ameitaka TFF kufuata Katiba ya 2006 na kanuni za BMT, lakini Katiba hiyo hiyo ya 2006 haina nafasi ya BMT, na hata kama TFF ingetaka kutekeleza hilo haliwezekani.

“Kwa maagizo haya inaonekana Waziri kashauriwa vibaya. Tunajua hakuwepo katika nafasi hiyo (2004) wakati wa makubaliano kati ya Serikali na FIFA kuacha mpira wa miguu ujiendeshe wenyewe,” amesema Rais Tenga.

Pia amezungumzia umuhimu wa Katiba toleo la 2012, kwani kuna marekebisho mengi yalifanyika mwaka 2007, 2008, 2009 na 2011 ambapo ukiyafuta maana yake unakiweka pembeni Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Bodi ya Wadhamini, wanachama wapya (mikoa), Bodi ya Ligi, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi, Leseni za Klabu na Kanuni za Fedha.
“Kwa uamuzi huu yote yaliyofanyika hayana maana. Waziri sidhani kama alikuwa anafahamu athari za maagizo yake. Kama angelijua asingefanya uamuzi huo. Si rahisi kurudi katika Katiba ya 2006. Hao wajumbe wa Katiba ya 2006 unawapata wapi? Maana yake hata vyama wanachama ni batili kwa vile vimerekebisha Katiba zao 2009 na 2010,” amesema Rais Tenga.
Amesema kwa Serikali kufuta, maana yake ni kutengua uamuzi wa TFF ambapo madhara yake ni nchi kufungiwa, ambapo timu za Taifa hazitacheza mpira, klabu hazitashiriki michuano ya kimataifa na wadhamini nao watakaa pembeni kwa vile hawawezi kudhamini timu ambazo hazishindani kimataifa.
“Dhana kwamba tukae tu tusicheze nje, ni dhana ya watu walio nje ya mpira wa miguu. Dhamira yetu ni kuhakikisha hatufungiwi. Waziri ametuagiza tupeleke barua FIFA kuwa ametengua marekebisho ya katiba. Hatupeleki hivyo, kwani hiyo ni Government interference, watatufungia.
“Nia yetu bado ni Waziri kutupa nafasi ya kutusikiliza,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa kuhusu uchaguzi kwa vile FIFA wanakuja ombi la TFF kwa Waziri ni kuacha kwanza mchakato uendelee hadi ufike mwisho.
“FIFA wanakuja, tuwasubiri. Nilidhani utaratibu huo utaheshimika. Kama mtu wa mpira haitaki FIFA anataka nini? Ahadi yetu ni kuhakikisha watu wanapewa haki. Hiyo ndiyo ahadi yetu na tumeisimamia, na ndiyo maana FIFA wanakuja,” amesema.
Akijibu swali kuhusu waraka, Rais Tenga amesema marekebisho ya Katiba hayakufanywa kwa siri, ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya marekebisho hayo kwa njia ya waraka ilipatikana ambapo 70 waliunga mkono na 33 walikataa.



Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment