HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es
Salaam , Victoria Nongwa amesema Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Tanzania ,
Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49 wana kesi ya kujibu kwa mashtaka yote matano
yanayowakabili.
Sheikh Ponda na wenzake hao wanakabiliwa na mashtaka matano,
likiwamo la kula njama, wizi wa mali
yenye thamani ya Sh59.6 milioni, uchochezi na kuingia katika ardhi
inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Limited kwa nia ya kujimilikisha visivyo
halali.
Akitangaza uamuzi huo, Hakimu Nongwa alisema: “Mahakama imepitia
ushahidi uliotolewa na mashahidi 17 wa upande wa mashtaka... inaonekana wazi
shauri hili linatokana na kipande cha ardhi.”
Kiongozi huyo na wenzake wanatarajiwa kuanza kujitetea Jumatano
na Alhamisi.
Hakimu Nongwa alieleza kuwa baada ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(Bakwata), kubadilisha ardhi ya ekari nne zilizopo Chang’ombe Markazi na 40 za
Kampuni ya Agritanza Ltd zilizopo Kisarawe, kuna baadhi ya Waislamu
hawakuridhika.
Alisema Mahakama haitaujadili kwa undani ushahidi uliotolewa na
upande wa mashtaka, bali itawapa nafasi upande wa utetezi kujitetea... “Kila
mshtakiwa anatakiwa aseme alikuwa anatafuta nini katika maeneo yale ya
Chang’ombe Markazi.,”
Alisema kabla ya Sheikh Ponda na wenzake kuanza kujitetea,
Wakili wao Juma Nassor anatakiwa apeleke vielelezo watakavyovitumia na kueleza
watatoa utetezi kwa njia ya kiapo ama la.
Katika kesi hiyo, Sheikh Ponda, Saleh Mukadam na wenzao 48,
wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6
milioni.
Mbali na mashtaka hayo, pia Ponda na Mukadam wanakabiliwa na
shtaka la uchochezi ikidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu katika
eneo la Chang’ombe Markazi, wakiwa viongozi wa Taasisi na Jumuiya za
Kiislamu Tanzania ,
waliwashawishi wafuasi wao kutenda makosa hayo.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini
Kweka alisema Oktoba 12, mwaka huu katika eneo hilo lililopo Wilaya ya Temeke,
kwa jinai na pasipo sababu za msingi walivamia ardhi inayomilikiwa na Kampuni
ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.
Kweka alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo la kuingia kwa nguvu kwa nia ya kutenda
kosa, kinyume na Kifungu cha 85 na 35 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Alidai kuwa kati ya Oktoba 21 na 16, mwaka huu katika eneo
hilohilo, washtakiwa hao pasipo uhalali wowote na hali iliyosababisha uvunjifu
wa amani, walijimilikisha ardhi hiyo mali ya Agritanza Limited.
Aidha Hakimu Nongwa alisema washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vifaa
na malighafi mbalimbali za ujenzi, yakiwamo matofali 1500, tani 36 za kokoto na
nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh 59,650,000, mali ya Kampuni ya Agritanza Ltd,
kati ya Oktoba 12 na 16.
Awali, baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka
yanayowakabili kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwasilisha
hati za kuzuia dhamana zao chini ya Kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo
wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Mara ya kwanza kesi hiyo ilifika Mahakama ya Kisutu Oktoba 18 na
tangu wakati huo ilikuwa ikisikiliza mashahidi upande wa utetezi na kabla ya
kufikia uamuzi huo.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment