Monday, March 11, 2013

Tangu dunia iumbwe huyu ndie mtu wa kwanza kufika chuo kikuu kwa kabila la Wahadzabe...


Diwani wa Kata ya Yaedachini, Bryceson Isaack anakiri kwamba juhudi za maendeleo katika jamii ya Wahadzabe zinaweza kuchukua muda mrefu kutokana na kabila hilo kubobea katika mila na desturi zake.
Katika eneo la Kipamba ipo shule pekee ya msingi  kijijini hapo, lakini wakati gazeti hili lilipofika katika shule hii hakukuwa na mwananfunzi haya mmoja, licha ya kwamba ilikuwa Ijumaa.
Mary Linza, ambaye anaishi jirani na shule hii anasema ina walimu wawili, ambao wote siku hiyo walikwenda  harusini katika Kijiji cha Domanga pamoja na wanafunzi wao.
Anasema  walimu hao wamekata tamaa kwa sababu wanafunzi hawahudhurii masomo shuleni hapo  na wazazi nao hawafanyi juhudi zozote kuwahamasisha watoto kwenda shule.
Katika Kata ya Yaedachini imejengwa shule ya sekondari kwa ajili ya Wahadzabe lakini Mkuu wa Shule hiyo, Petro Ringo anasema wengi wa wananfunzi wanaosoma hapo siyo Wahadzabe kama ilivyokusudiwa.
“Mpaka sasa shule ina Muhadzabe mmoja tu, wengine wote wameshaacha,” anasema.
Shule hiyo ambayo wanafunzi wa kwanza  wa kidato cha nne wamemaliza mwaka jana, ina walimu saba na wanafunzi 139 tu. Ringo anasema wahadzabe wana msukumo mdogo mno wa elimu kwa sababu ya kuelemea tamaduni zao.
“Wanaacha shule kwa sababu wanapenda mazingira ya porini, ni vigumu mno kwao kuyazoea mazingira mengine,” anasema. Anatoa mfano na kusema  watoto wa Kihadzabe waliofaulu kidato cha kwanza mwaka huu ni 48 lakini si ajabu wakafika wanafunzi 20 tu.
Anasema taasisi zinawasaidia kwa kiais kikubwa  kwa kuwalipia ada na kuwapa mahitaji yote ya muhimu lakini bado wanaacha shule.
Mwalimu huyo anasema kitu kingine kinachowafanya waache shule ni kubanwa na sheria za shule, kwa mfano wanakatazwa kuwinda, kubeba mishale shuleni na bakora nazo zinawakimbiza.
Anaongeza kuwa msukumo huo mdogo wa elimu wakati mwingine unasababishwa na wazazi.“Visingizio vinaletwa na wazazi ili watoto wasije shule. Mzazi anaweza kusema mtoto hawezi kuja shule kwa sababu ana njaa,” anasema Ringo.
Wanasaidiwaje?
Zipo taasisi kadhaa zinazowasaidia Wahadzabe na mojawapo ni Taasisi ya kusaidia wafugaji, wawindaji na wakusanyaji (UCRT) ambayo imekuwa ikiwasaidia katika suala la elimu.
Kila mwaka UCRT imekuwa ikiwasomesha vijana wa Kihadzabe, sambamba na kuwapa mahitaji muhimu, lakini Mratibu wa Miradi wa taasisi hiyo Dismas Mataiya, anasema bado kuna msukumo mdogo wa elimu kwa Wahadzabe.
“Wazazi wa Kihadzabe hawatoi ushirikiano kwa taasisi, wakati mwingine wanawaficha watoto wasiende shule,” anasema Mataiya na kuongeza kuwa wakati mwingine UCRT huwabembeleza wasichana wakasome lakini wao hukataa na kubaki katika mapori yao ya asili.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Yaedachini, Jovita Edward anasema  maisha ya Wahadzabe ni magumu na pengine wanaweza kupotea kabisa katika ramani kwa sababu wanakosa huduma zao za asili.
Anasema mwingiliano na makabila mengine unawakosesha huduma zao za asili ambazo zinatumiwa vibaya. “Maeneo yao yanapotea kwa sababu ya mwingiliano huo, nina wasiwasi wapo katika hatari ya kutoweka,” anasema Edward na kuongeza:
“Majangili wanaoua wanyamapori wamekuwa wakiingia katika vijiji vya jamii hiyo na kuua wanyama ambao ni chakula chao muhimu”.
Richard Baallow, ambaye ni kiongozi wa Wahadzabe anasema serikali imetenga kilomita za mraba 23,375 za hifadhi  na matumizi asili ya Hadzabe  kwa ajili ya uwindaji na urinaji asali.
Anasema uhamiaji wa makabila mengine umechangia kwa kiasi kikubwa kuharibu uoto wa asili uliokuwepo katika makazi yao. Baallow anasema juhudi kubwa zinafanyika kuwapatia maendelo ingawa kuna changamoto nyingi.
“Wengi hawazikubali fursa hizi za maendeleo kwa sababu ya kuthamini tamaduni zao,” anasema.
Edward Lekaite ambaye ni wakili katika taasisi ya UCRT anasema  tatizo kubwa walilonalo Wahadzabe ni kukosa viongozi na sheria zitakazowalinda na kwamba makabila mengine yanautumia udhaifu huo kuvamia maeneo yao.
“Wahadzabe hawana viongozi, waliopo wanatoka katika makabila mengine na sheria za kuwasaidia hazitekelezwi kwa sababu viongozi waliopo wanapendelea makabila yao,” anasema Lekaite.
SHANI Msafiri, hakuwahi kusikia nini maana ya elimu. Alizaliwa porini, akajifunza kuwinda na kurina asali. Alikulia katika nyumba ya nyasi, akakua kwa kula matunda, nyama na asali.
Hakuwahi kufikiri kuwa ipo siku ataliacha pori hilo lililompa furaha ya utoto wake na kwenda kuchangamana na jamii yenye vitabu, sayansi, teknolojia. Wala hakuwahi kudhani kuwa ataonja vyakula vilivyokaangwa na vinjwaji vilivyohifadhiwa kwenye majokofu.
Lakini leo hii, Shani amekuwa kama kiongozi wa kitaaluma wa kabila la Wahadzabe.  Ni Muhadzabe wa kwanza kufika Chuo Kikuu, akisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Makumira, Arusha.
Safari yake ya kielimu
Mwaka 1998 serikali ilifika katika kijiji cha Mongoa Mono kata ya Yaedachini, na kuamrisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule, wapelekwe shule mara moja.
Wazazi walitii amri… siku ya siku ilipowadia, gari la serikali lilijongea  na kumbeba Shani kuelekea ‘kwenye elimu’ ambako kwake kulikuwa ni msamiati.
Akiwa ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika watoto saba wa familia ya mzee Msafiri, alitakiwa kuamka alfajiri toka Mongoa Mono hadi YaedaChini ilipo shule yake, kiasi cha kilomita 30 kila siku.
Shani amezaliwa katika mazingira ambayo ni nadra kwa vijana kupata elimu ya darasani.
Anasema: “Nilisoma katika mazingira ya kimaskini mno, wenzangu wengi nilioanza nao waliacha shule na kuendelea na shughuli za uwindaji, lakini mimi nilipiga moyo konde,”
Anasema wazazi walifanya biashara za kuuza asali na nyama ili wampatie japo mahitaji machache ya shule.
Mwaka 2005 alimaliza darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Diego, wilayani Karatu.

 Chanzo: Gazeti Mwananchi.

No comments:

Post a Comment