Na Hafidh Kido
VYAMA vinavyosimamia ndondi
za kulipwa nchini, katika hali isiyokuwa ya kawaida, vinamcheka bondia Francis
Cheka badala ya kumsikitikia kwa hujuma anazodai alifanyiwa nchini Ujerumani
hivi karibuni.
Wakizungumza na kidojembe kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama vya PST na TPBO wameeleza ya kuwa
hawashangai kusikia Cheka alihujumiwa na Promota wa Kenya , Thomas Mutua aliyekwenda
naye Ujerumani kucheza pambano la kusaka
ubingwa wa Shirikisho la Ndondi la Kimataifa (IBF).
Katika pambano hilo Cheka anadai ya kuwa Promota huyo aliyekuwa kwenye
kona yake kama kocha , alitupa taulo ulingoni
kuashiria mwamuzi asimamishe pambano kumwokoa ilhali alikuwa yuko
‘fiti’kuendelea kupambana na Mjerumani, Uensal Arik aliyekuwa akichuana naye.
Hiyo ilikuwa kwenye raundi ya saba.
“Hii si mara ya kwanza kupata
malalamiko yanayomuhusu huyu ‘promota’ Thomas Mutua kutoka Kenya kuwahujumu mabondia wa Tanzania . Tulishakubaliana
tusimpe kibali cha kuondoka na mabondia wetu, mimi nashangaa sana amepata wapi kibali cha kuondoka na
Cheka,” alisema Emmannuel Mlundwa, muasisi wa ndondi hizo nchini anayekiongoza
chama cha PST.
kidojembe ilipowasiliana na
Yassin Abdallah ‘Ustadh’ Rais wa chama kingine cha ndondi za kulipwa cha TPBO naye
aliungana na Mlundwa kwa kuondoka na mtu
ambaye hana baraka zozote nchini.
“Muulize Cheka aliondoka kwa
kibali cha nani. Kama aliondoka kienyeji
hatuhusiki. Cheka ameondoka bila kufuata kanuni za ngumi hivyo hana msaada. Katiba
ya Tanzania inaruhusu mtu
kusafiri popote anapotaka kama amefuata katiba ya nchi ni sawa alikuwa na haki
kuenda Ujerumani lakini kwa mujibu wa kanuni za ngumi amefeli, na hili litakuwa
funzo kwa mabondia wote wanaofuata mapromota kutoka Kenya ,” alisema Yassin.
Cheka mwenyewe, Francis Cheka
‘SMG’ ambaye ni bingwa wa IBF Afrika uzani wa Super Middle, alikiri kutopewa
ushirikiano na chama chochote cha ngumi za kulipwa Tanzania kwa ajili ya safari yake
ya Ujerumani ingawa alidai kutoa taarifa kwa Rais wa kamisheni ya ngumi za
kulipwa Tanzania (TPBC), Onesmo Ngowi.
“Nilizungumza na Ngowi
kuhusiana na hujuma nilizofanyiwa lakini naye aliniambia hili litakuwa funzo
kwangu, simuelewi kwa kweli,” alisema.
Kuhusu ni nini hasa
kilichotokea, Cheka anasema kwamba aliombwa kupokea rushwa ili apoteze pambano hilo lakini
akakataa. “Ndugu yangu nilifuatwa
hotelini mara tano wakitaka niuze pambano kwa Euro 6,000 nikakataa,” alisema
Cheka.
“Nadhani baada ya kuona nimekuwa
mbishi, walimfuata Mutua pamoja na mwamuzi, maana taulo lilirushwa na Mutua
kutoka kona yangu, nilikuwa fiti na yule jamaa alishaanguka mara moja.
Nashangaa kwanini mwamuzi alikubali kumaliza pambano,” aliongeza.
Cheka alisema ya kuwa mpaka
sasa hajalipwa pesa zake zote. “Mkataba unasema nilipwe (Euro 11,000), lakini
mpaka sasa nimelipwa Euro 4,500.
Kuhusu vyama vya ndondi za
kulipwa nchini, Cheka aliviponda. “Mimi
naona kama vya kinafiki tu hasa chama cha
‘Ustadh’ (TPBO),” alisema bila kufafanua ni kwa nini hicho ndicho anachokiponda
zaidi.
kidojembe ilipowasiliana na
Mutua kwa njia ya simu kutoka Nairobi alisema aliamua kutupa taulo ulingoni
kumuokoa Cheka baada ya kumuona amepatwa na tatizo.
“Niliamua kurusha taulo kwa sababu
niliona bondia wangu ameumia mkono wa kulia hivyo sioni kama kuna tatizo lolote
kufanya hivyo kwani ni kitu cha kawaida sana
kumsaidia bondia anapozidiwa,” alisema Mutua anayedai pia kwamba alipata kibali
cha kumchukua nchini kutoka kwa Ngowi.
Kuhusu Cheka kufuatwa mara
tano kutakiwa auze pambano, Mutua alisema hajaambiwa kitu kama hicho na bondia
wake kwani ikiwa alifuatwa basi mtu wa kwanza kujua ilipasa kuwa ni yeye lakini
hajui chochote na kuongeza kuwa mabondia wengi wa Tanzania wanapenda kupotosha umma
wanaposhindwa.
“Kitu ambacho hatujamalizana
na Cheka ni pesa zake mkataba unasema anatakiwa kulipwa Euro 11,000 lakini
mpaka sasa amelipwa Euro 5,500 na sababu kubwa ni matatizo ambayo yalitokea
bana yetu na promota Eva Arole ambaye aliandaa pambano lile lakini mpaka sasa
tunajitahidi kuwasiliana naye kuhakikisha pesa hizo zinatumwa,” alisema Mutua.
kidojembe ilijaribu
kuwasiliana na Onesmo Ngowi, ili kupata ukweli kuhusu yeye kutoa kibali kwa
Mutua kumchukua Cheka lakini simu yake
ilikuwa ikiita bila kupokewa.
Mwandishi alituma ujumbe kwenye
simu uliomtaka kutoa ufafanuzi juu ya chama chake kuhusika kutoa ama kutotoa kibali kwa Cheka lakini hakujibu
ujumbe huo ingawa ulionyesha kumfikia.
Dar es Salaam, Tanzania
26 March, 2013
No comments:
Post a Comment