Leo tarehe 8 March, wanawake
duniani wanasherehekea siku yao .
Mpaka sasa sijajua wanasherehekea siku yao
kwa namna gani. Kupata uhuru, haki ama usawa.
Lakini kwa namna jambo hili
lilivyowekwa inaonyesha wanawake wanakata minyororo ya udhalilishwaji na
unyonge kutoka kwa wanaume ama mfumo dume ambao ‘unampendelea mwanaume’ kuwa
mmiliki wa dunia.
Mungu anasema mwanamme ni
kiongozi kwa mwanamke; na hata wanandoa siku yao ya harusi huambiwa na viongozi wa dini na
kijamii kuwa mume amlinde mke kwa maisha yake yote.
Na hata katika utengano mume
ndie anaeamua kuachana na mke. Lakini jamii zilizoendelea hasa nchi za
magharibi mtu yeyote anaweza kuamua mustakabali wa ndoa. Mume ama mke anaweza kusema
inatosha, kila mmoja ashike njia yake. Ila nchi za kiafrika na Asia bado mustakabali wa ndoa upo mikononi mwa mume.
Sitaki kushindana na mvumo wa
mabadiliko wa kudai usawa. Lakini mpaka sasa kuna kazi ambazo mwanaume hawezi
kuzifanya kama ambavyo mwanamke kuna kazi
hamudu kuzifanya bila msaada wa mwanamme.
Zamani ukiona mwanamke
anaendesha gari hiyo ni ajabu akidi; lakini sasa ni jambo la kawaida sana kumuona mwanammke
anaendesha gari. Ingawa kuna aina ya magari, hata imezoeleka magari yenye
maumbo madogo yananasibishwa na jinsia ya kike. Si ukariri wa mambo lakini
maumbile ndivyo yanayoisukuma akili kuamini hivyo.
Tukubali kutokubaliana kuwa
mwanamke na mwanamme katu hawawezi kuwa sawa. Udhaifu unaanza pale mwanamke
anapolazimisha kupata haki ama usawa huo.
Usawa haudaiwi, huwezi kudai
usawa bali maumbile ndiyo yanayoamua hivyo. Ikiwa unaamini aina fulani ya
shughuli inaweza kufanywa na jinsia zote basi haina haja kuutangazia umma
hivyo. Bali njia rahisi ni kutumbukia na
kuifanya.
Ukelele wa mabadiliko hauna
maana ikiwa unatawaliwa na dhana; kinachopasa kufanywa ni vitendo na si maneno.
Hujisikia uchungu sana
kusikia wanawake wanalalamika kuwa hawatendewi haki katika jamii.
Dhamira ya dhati ndiyo
inayoamua usawa, mwanamke amua sasa kupambana. Kelele haziwezi kuwafikisha
popote zaidi ya kuendelea kuwaona wasumbufu.
Siku ya wanawake duniani
haifai kutumika kudai haki za wanawake bali itumike kujipongeza kwa kuumbwa
wanawake. Mwanamke ni mtu bora sana
katika dunia hakuna mfano wake.
Mama ndie anaezaa kila
kiumbe. Mtoto anaweza kuzaliwa bila baba lakini katika historia dunia tangu
imeanzishwa hakuna kiumbe aliekuja katika dunia hii bila mama.
Waamini wa dini watakubaliana
nami kuwa Adam na Hawa ndiwo viumbe pekee wa ajabu ambao wameumbwa kimaajabu.
Baba yetu Adam aliumbwa kwa mikono mitakatifu ya Mungu, hakuwa na baba wala
mama.
Mama yetu Hawa alitoka
ubavuni mwa Baba yetu Adam hivyo bibi Hawa amekuja duniani bila mama, na Adam
hawezi kuwa baba yake maana baadae alimuoa. Mungu alitaka tu kuonyesha uwezo
wake.
Lakini yote haya yalitokea
mbinguni, na si hapa duniani. Kioja kilichowahi kutokea duniani ni kimoja tu
cha kuzaliwa Nabii wa Mungu Issa ama Yesu na mama pekee bila baba.
Hadithi hii inaonyesha
utukufu wa mwanamke, maana mama ndie anaweza kulea mtoto, kumlisha na kumpa
raha zote za mwanzo katika dunia.
Hata Mtume wa Waislamu
Mohammed (SAW), wakati anazaliwa baba yake alikuwa ameshaaga dunia. Funzo hili
linaonyesha kuwa mtoto hawezi kuzaliwa mama akiwa amekufa, ila mtoto anaweza
kuzaliwa baba akiwa amekufa. Utukufu ulioje huu wa mwanamke.
Kitu kingine cha kuonyesha
utukufu wa mwanamke katika jamii ni namna mama anavyopewa hadhi mbele ya mtoto
wake, maana mtoto anaweza kuitwa wa haramu akizaliwa nje ya ndoa, na kwa upande
wa Waislamu mtoto wa aina hiyo hafai kurithi ama kurithiwa na baba aliemzaa
bila kumuoa mama yake. Lakini mama anakuwa na haki zote kwa mtoto huyo,
wanawake wanataka nini tena mbele za Mungu mtukufu?.
Makala haya yana lengo moja
tu, kumfanya mwanamke kujiamini na kuon ana bahati kubwa sana katika jamii. Mwanamme hawezi kukamilika
bila ya kuoa. Heshima ya mwanamme inaongezeka baada ya kuoa.
Na katika kila mafanikio ya
mwanamme basi nyuma yake kuna mwanamke mwema aliemshauri. Anaweza kuwa mama ama
mke wake. Na hata katika maisha mke na mama ndiwo watu wanaouma sana kuwakosa.
Fanya utafiti katika maneno
haya na utaamini hakuna haja ya kuwa na siku ya wanawake. Bali wanawake kila
siku ni siku yao
ya kujiamini na kujipongeza kwa utukufu walio nao.
HAFIDH KIDO
8 March, 2013
No comments:
Post a Comment