Sunday, March 31, 2013

Hata Wachina wameshangazwa na aina ya zege lililochanganywa kwenye jengo lililoanguka Dar es Salaam.

 Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT)wakiwa wamejipanga kupokea miili inayofukuliwa kwenye kifusi cha jengo ghorofa 16 lililoanguka jana.Picha na Fidelis Felix.


Rais Jakaya Kikwete akiwa na baadhi ya viongozi wa Dar es Salaam, wakati alipokwenda kuangalia athari zilizosababishwa na kuanguka kwa jengo hilo juzi.

 Zoezi la kutafuta miili iliyokwama katika vifusi inaendelea, zaidi ya maiti 22 zapatikana.
Dar es Salaam. Idadi ya watu waliokufa kutokana na kufukiwa na kifusi cha jengo la ghorofa 16 lililoporomoka juzi asubuhi jijini Dar es Salaam, imefikia 22.

Habari zilizopatikana kutoka eneo la uokoaji na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova zinaeleza kuwa miili iliyopatikana imepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya Lucky Construction Limited liliporomoka saa 2.30 asubuhi wakati mafundi na vibarua wakiendelea na ujenzi huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.

Rais Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ambaye jana pia alifika katika eneo la tukio, kama ilivyokuwa juzi, alipata taarifa fupi ya maendeleo ya uokoaji kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadik na Kamanda Kova.

Baada ya kupewa taarifa hiyo, Rais Kikwete alimwagiza Kamanda Kova kuhakikisha wahusika wanakamatwa akiwamo Mkadiriaji Majengo (Quantity surveyor), mchora ramani za majengo (Architecturer), Mhandisi Mshauri (Consultant) na Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam. Juzi baada ya kutembelea eneo la tukio, Rais Kikwete aliagiza wahusika wote wa ujenzi huo wachukuliwe hatua kali.

Habari zilizopatikana jana zilidai kuwa Diwani wa Kata ya Goba, Wilaya Kinondoni, Ibrahim Kisoka ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya ujenzi, na Mhandisi Mshauri kwa pamoja wamejisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi na hadi saa 8:00 jana mchana walikuwa wakihojiwa.

Awali Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa amemtaka mmiliki wa Kampuni ya Lucky Construction Limited ambaye ni Diwani wa Kata ya Goba, Kisoka na wahusika wengine kujisamilisha kituo cha polisi, kabla hawajaamua kutumia nguvu kumtafuta.

Pinda atembelea eneo la tukio
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika eneo hilo saa 3:41 asubuhi, kujionea hali ilivyo, lakini hakutoa tamko lolote. “Sina la kusema,” alisema Waziri Mkuu alipoulizwa na waandishi wa habari kutoa kauli ya serikali kuhusiana na tukio hilo.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliyefuatana na Pinda, alisikika akimwagiza Kamanda Kova kuhakikisha mchora ramani wa jengo hilo naye anatiwa nguvuni kwa kuwa jengo hilo lilikuwa la ghorofa 10, lakini likajengwa hadi 16. Mtu mwingine ambaye anatafutwa na jeshi la polisi kukamatwa ni Mhandisi Mshauri.

Lukuvi alimwagiza Kova kuwa watu waliokuwa karibu na jengo jingine la ghorofa 15 lililojengwa na mkandarasi huyo, kuhama mara moja na ubomoaji ufanyike bila kuleta madhara.

Mwenyekiti wa CUF
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alitumia fursa hiyo kuitaka Serikali kuwabana makandarasi wasio na sifa kwani wanahatarisha maisha ya watu.
“Huu ni uzembe, wahandisi wa jiji walikuwa wapi? Wasimamizi na washauri walikuwa wapi hadi jengo linafikia ghorofa 16?” Alihoji Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba aliitaka Bodi ya Makandarasi (CRB) kufuta leseni ya kampuni hiyo, kwani imeonyesha kuwa haiwezi kusimamia ujenzi na hivyo kusababisha vifo.

Huzuni, vilio na simanzi
Vilio na huzuni viliendelea kutanda jana katika eneo hilo ambapo waokoaji walikuwa wakijitahidi kufukua vifusi na kuzingirwa na watu waliokuwa wakisubiri ndugu zao waliofukiwa na kifusi kutolewa.

Watu wengi tangu asubuhi walikuwa wamesimama karibu na eneo hilo huku wengi nyuso zao zikiwa zimegubikwa na simanzi na wengine wakilia. Mama mmoja aliyekuwa akilia mapema asubuhi katika Mtaa wa Mshihiri, alisema mwanawe ni fundi na jana hakurudi, lakini pamoja na kilio, alisema bado haamini kama mwanawe amepoteza maisha.

Mwingine aliyekuwa ameshikiliwa na wenzake, alisikika akisema miongoni mwa waliopotea ni mume wake aliyemuaga asubuhi kuwa anakwenda kibaruani lakini hadi usiku wa manane hakurudi hivyo ilibidi afike eneo hilo.

Mama mwingine wa jamii ya Kihindu aliyekuwa akilia, alizirai kabla ya kuzinduka baada ya kupatiwa huduma ya kwanza. Mama huyo alisema mtoto wake ni miongoni mwa waliokwama kwenye kifusi hicho.

Barabara zafungwa
Mbali ya watu hao barabara zote zinazoingia katika eneo hilo zimefungwa.
Barabara hizo ni Mshihiri na Morogoro, Hazrat Abbas, Mali -Asia, Mali-Zanaki, Mtaa wa Zanaki, India na Indira Ghandhi.

Wachina walishangaa ‘zege’
Wachina wa Kampuni za ujenzi za China zilizopo nchini, Beijing Construction Engineering Group, BCEG iliyojenga Uwanja wa Taifa, na ile ya China Civil Engineering Construction Company (CCECC) inayojipanga kwa ujenzi wa Daraja la Kigamboni, ni miongoni mwa waliofika kusaidia uokoaji.
Mmoja wa Wachina hao alichukua kipande cha zege kilichotoka kwenye jengo hilo, na kukisaga kwa kutumia mkono, kikapukutika.

“Hii mchanga mingi..., hakuna zege kama hii,” alisema Mchina huyo kutoka Kampuni ya CCECC ambaye hata hivyo alikataa kutaja jina lake.
Wachina hao walitoa kijiko ambacho ndicho kilichosaidia kwa kiasi kikubwa katika uokoaji huo.

Huduma za kijamii
Mashirika mbalimbali ya hisani, yalikuwa na kazi ya kuleta vyakula, maji na vitu vingine kwa waokoaji ili kazi iendelee bila kusimama.

Malori ya Kampuni ya Strabag yanayotumika kwa ujenzi wa Barabara ya Morogoro kwa mabasi yaendayo kasi, yalishiriki kikamilifu saa 24 kuzoa kifusi hicho kilichokuwa kimejaa nondo za kila saizi.

Vikosi vya uokoaji pamoja na manesi wa Hospitali ya Mwananyamala, Hospitali ya Ibrahim Hajj na Chama cha Msalaba mwekundu, wameweka kambi wakiwa na dawa, dripu, na vitu mbalimbali vya huduma ya kwanza.

Matukio mengine
Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu jengo kuanguka, kwani Februari jengo la ghorofa nne lilianguka maeneo ya Kijitonyama Mpakani jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtoto wa miaka 9.

Licha ya ujenzi wa jengo hilo kusimamishwa miaka 10 iliyopita, familia ya marehemu iliendelea kuishi katika jengo hilo.

Juni 21, 2008 jengo la ghorofa 10 lilikuwa likiendelea kujengwa na Kampuni ya NK Decorators katika Mtaa wa Mtendeni Kisutu jijini Dar es Salaam liliporomoka na kuua mtu mmoja.

Mwaka 2006 jengo la ghorofa lilianguka eneo la Chang’ombe Village Inn na kuua mtu mmoja, baada ya tukio hilo aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa aliunda tume kuchunguza tukio hilo ambayo ilibaini kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es Salaam yalikuwa yamejengwa kinyume na taratibu za ujenzi.
Imeandikwa na Ibrahim Bakari, Ibrahim Yamola, Nuzulack Deusen
Chanzo: Gazeti Mwananchi.

No comments:

Post a Comment