SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
ambalo lilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kutokana na baadhi ya wagombea kulalamika kuenguliwa sasa
litatuma ujumbe wake nchini katikati ya mwezi ujao.
Ujumbe huo ambao moja ya shughuli zake
kuwasikiliza wote walioenguliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na
hawakuridhika na uamuzi huo, utakuwepo nchini Aprili 16 na 17 mwaka huu.
Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa FIFA,
Jerome Valcke kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, kazi ya ujumbe huo ni
kubaini tatizo lililopo na kutoa ripoti kwa mamlaka zinazohusika ndani ya FIFA
kwa ajili ya kutoa mwongozo.
Ujumbe huo utakutana na pande mbalimbali
zinazohusika wakiwemo wagombea, kamati za uchaguzi za TFF. Lakini pia ujumbe
huo unatarajia kumtembelea Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk.
Fenella Mukangara pamoja na watendaji wake wizarani.
Uchaguzi wa viongozi wa TFF ulikuwa ufanyike
Februari 24 mwaka huu, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya wagombea
walioenguliwa kulalamika kuwa hawakutendewa haki na wangependa shirikisho hilo liingilie kati.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment