SERIKALI ya Malawi
imesema ina wasiwasi kuhusu hatma ya mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na kwamba
hali hiyo inatokana na Tanzania
kuvunja sehemu ya makubaliano ya usuluhishi.
Kauli hiyo inakuja wakati jopo lo viongozi wastaafu kutoka nchi
wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(Sadc), likijiandaa
kuwasilisha ripoti yake baadaye mwezi huu.
Jopo hilo
linaloongozwa na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano, litakabidhi ripoti
hiyo kwa viongozi wakuu wa nchi zote mbili.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Malawi, Ephraim Chiume,
ameituhumu Tanzania kwamba imeanza kuzungumzia utatuzi wa mgogoro huo wakati
ikijua kuwa mzozo huo uko katika hatua ya upatanishi maalumu.
Waziri Chiume aliikosoa kauli iliyotolewa hivi karibuni na
Waziri wa Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa mpaka baina ya mataifa hayo mawili, unakaribia
kupatikana.
Alisema kitendo cha Membe kuzungumzia maendeleo ya
mgogoro huo kinapingana na makubaliano ya pamoja yaliyowasilishwa kwa
Chissano na kwamba hatua hiyo inavunja moyo.
Waziri Chiume aliliambia gazeti la Nyasa Times kuwa pande zote
mbili zilipokutana Nombemba 17 mwaka jana jijini Dar es Salaam , zilikubaliana kuzungumzia
mgogoro huo ili kuepuka kuingilia juhudi za upatanishi.
Alisema hata hivyo, hivi karibuni ya Serikali ya Tanzania
imekiuka sehemu ya makubaliano hayo.
“Tanzania
wamevunja makubaliano, na sisi tunasisitiza kuwa Ziwa Nyasa ni la Malawi ,”
alisema waziri.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo, wamesema kauli huyo inaashiria
kuwa huenda pande hizo mbili zikashindwa kukubaliana na mapandekezo
yatakayowasilishwa na mpatanishi wa mzozo huo.
Mpatanishi huyo mwezi huu anatazamiwa kukutana na Rais Jakaya
Kikwete na yule wa Malawi ,
Joyce Banda.
Hata hivyo, alivyotafutwa ili kuzungumzia malalamiko hayo,
waziri Membe kupatikana, lakini Naibu wake Mahadhi Maalimu, alisema:
“Ninachosema mimi kwanza hizo taarifa sijazipata na kama
zipo basi Serikali itawasiliana kupitia mikondo sahihi. Serikali haiwezi
kujibizana kupitia magazeti”
Hivi karibuni Serikali ya Tanzania
na Malawi
zilipeleka barua ya pamoja kwenye Jukwaa la Marais wa Wastaafu wa Nchi za
Kusini mwa Afrika linaloongozwa Chissano, zikiomba zipatanishwe katika mzozo
huo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya majadiliano ya pande zote
mbili kushindwa kuzaa matunda.
Kama sehemu ya kuepusha mgongano wa kimaslahi, jopo hilo la wasuluhishi halikuwahusisha viongozi wastaafu wa Tanzania
Alhaji Ali Hassani Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Hali kadhalika Bakiri Muluzi wa Malawi .
Hata hivyo, duru za kidiplomasia mjini Lilongwe
zinasema Serikali ya Malawi
imejiandaa kwenda katika Mahakama ya Haki ya Kimataifa(ICJ) kama upatanishi huo utashindwa kuzaa matunda.
Gazeti la Daily Times limewanukuu maofisa wa Serikali wakisema
kuwa karata ya mwisho kwa Malawi
itakuwa ni kwenda katika mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment