Monday, March 25, 2013

Taifa Stars yawapa raha watanzania kwa kuifunga Morocco 3-1 jana.

 Mfungaji wa mabao mawili ya jana kati ya matatu Mbwana Samatta akiambaa na mpira huku mabeki wa Morocco wakitafuta mbinu za kumdhibiti.




Timu ya taifa ya Tanzania,Taifa Stars hii leo imeendeleza rekodi yake nzuri kwenye uwanja wa nyumbani baada ya kuitandika kwa jumla ya mabao matatu kwa moja timu ya taifa ya Morocco ambayo inaundwa na wachezaji wanocheza soka kwenye nchi za bara la Ulaya.
Tanzania ikiwa ni moja timu ya nne zinazounda kundi C barani Afrika,ikiwemo pia Ivory Cost,Morocco na Gambia zinazosaka nafasi ya kushiriki michuano ya kombe la dunia hapo mwakani nchini Brazil,Ilikuwa ya kwanza kupata bao la katika kipindi cha pili dakika ya 46,bao lililofungwa na Mshambuliaji wa kimataifa anayeichezea klabu ya TP Mazembe ya DRC,Thomas Ulimwengu aliyeingia akitokea benchi.
Wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Benjamini Wiiliam Mkapa,mbele ya mashabiki wao,Stars ilipata bao la pili dakika ya 67 kupitia kwa Mbwana Samata ambaye pia anaichezea klabu ya TP Mazembe na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa soka wa Tanzania ambao wamekuwa na kiu ya zaidi ya miaka 30 ya kutoiona timu yao ya taifa ikishiriki michuano ya kimataifa tangu mwaka 1980 waliposhiriki kombe la mataifa huru barani Afrika iliyofanyika nchini Nigeria.
Mbwana Ally Samata,Mzaliwa wa Dar es Salam,mtoto wa Askari polisi wa zamani wa jeshi la Tanzania,aliiendelea kuwafurahisha watanzania baada ya kuandika bao la tatu dakika ya 80 na kufanya Taifa Stars kuiongoza mchezo huo kwa mabao matatu kwa bila kabla ya Morocco hawajazinduka na kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Yousef El Arabi anayeicheza klabu ya Granada ya nchini Hispania.
Dakika 90 zilimalizika kwa Tanzania kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja na kuwafanya kusalia kwenye nafasi ya pili wakiwa na point sita nyuma ya Ivory Cost ambao wana point saba wakiwa na tofauti ya point moja,ambapo Ivory Cost wao jana jumamosi waliwafunga Gambia kwa mabao matatu kwa bila.
Mechi ijayo Tanzania itasafiri hadi nchini Morocco hapo tarehe 6 mwezi wa sita mwaka huu kurudiana na Simba hao wa Milima ya Atlas ambao walipata kuwa mabingwa wa bara la Afrika mwaka 1976 katika Fainal zilizofanyika nchini Ethiopia.
Chanzo: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment