WEDNESDAY, MARCH 20, 2013
Kumb. Na.
OMU/US/003/2013
18/03/2013
Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi,
S.L.P 9223,
Mheshimiwa:
RUFAA DHIDI AGIZO LA
ACP CHARLES KENYELA KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA KIPOLISI WA KINONDONI KUZUIA
MKUTANO WA HADHARA WA MBUNGE NA WANANCHI TAREHE 16 MACHI 2013
Kwa barua hii
nawasilisha rasmi rufaa kwa kutumia kifungu cha 43 (6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi
na Huduma za Polisi wasaidizi sura ya 322 (The Police Force and Auxilliary
Service Act Cap 322 RE 2002) dhidi ya agizo la ACP Charles Kenyela Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni kuzuia mkutano wa hadhara wa mbunge na
wananchi tarehe 16 Machi 2013.
Katika kushughulikia
rufaa hii zingatia kuwa tarehe 4 Machi 2013 niliwasilisha taarifa kwake kwa
mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge na. 3 ya
mwaka 1988 (The Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act) kuwa
tarehe 16 Machi 2013 nilipanga kufanya mkutano na wananchi Jimboni.
Katika taarifa hiyo
kupitia barua yangu yenye Kumbu. Na. OMU/US/001/2013 ambayo nilitoa pia nakala
kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Afisa
Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Afisa Mtendaji wa Kata ya Manzese na Afisa
Mtendaji wa Mtaa wa Muungano, nilieleza kwamba mkutano huo nilipanga kuufanya
katika Kata ya Manzese Eneo la Bakheresa kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 5
Asubuhi.
Katika taarifa hiyo
nilieleza kwamba lengo la mkutano huo ni kuwapa mrejesho wananchi kuhusu
masuala niliyoyawasilisha katika Mkutano wa Kumi wa Bunge uliomalizika tarehe
08 Februari 2013 na kupokea mambo ya kuyazingatia kuelekea Mkutano wa Kumi Na
Moja wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 9 Aprili 2013.
Hata hivyo, kupitia
mkutano wake na vyombo vya habari tarehe 14 Machi 2013 na barua yake iliyoletwa
ofisini kwangu tarehe 15 Machi 2013, ACP Charles Kenyela Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni alitoa agizo la kuzuia mkutano wa hadhara wa
mbunge na wananchi niliopanga kuufanya tarehe 16 Machi 2013.
Katika agizo hilo alilolitoa chini ya
kifungu cha 43 (2) na 43 (3) Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za Polisi
sababu iliyohusu mkutano kwa mujibu wa barua yake yenye Kumb. Na.
DSM/KINONDONI/SO.7/2/CHADEMA/284 ni:
“Eneo la Manzese
Bakhresa ambalo unakusudia kufanyia mkutano siyo eneo halali kwa ajili ya
mikutano. Eneo hilo
kwa mujibu wa maelekezo ya Manispaa ya Kinondoni kupitia mipango miji ni eneo
linalotumika kwa ajili ya kuegesha magari makubwa (malori) na ndio maana liko
katika eneo kuu la barabara ya Morogoro ambayo iko katika matengenezo. Kuruhusu
mkutano wako kufanyikia hapo ni kukiuka sheria ya mipango miji ya Manispaa ya
Kinondoni pamoja na kuingilia shughuli za ujenzi wa barabara unaoendelea hivi
sasa na kuwabugudhi watumiaji wengine wa eneo hilo ”.
SABABU ZA RUFAA NA
MAELEZO YA KUTORIDHIKA:
Nakata rufaa dhidi ya
agizo hilo
haramu ambalo limekiuka masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Kinga, Madaraka
na Haki za Bunge kwa sababu zifuatazo:
Mosi, Eneo la Manzese
Bakheresa limetumika na limeendelea kutumika kufanya mikutano kwa nyakati
mbalimbali. Agizo lake kuwa eneo hilo siyo
halali kwa ajili ya mikutano linamaanisha kwamba polisi waliruhusu Rais Jakaya
Kikwete kinyume cha sheria ya Mipango Miji tarehe 17 Oktoba 2010 alipofanya
mkutano katika eneo hilo .
Kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2005 mpaka 2012 nimefanya mikutano katika
eneo hilo lakini hakuna wakati wowote ambao Jeshi la Polisi au mamlaka nyingine
yoyote imewahi kutoa amri ya kukataza mikutano kufanyika katika eneo
hilo.
Pili, hakuna uhusiano
kati ya kufanya katika eneo ambalo linaendelea kutumika (ikiwemo kwa maegesho
ya molori) na kisingizio kilichotolewa kuwa mkutano ungeingilia shughuli za
ujenzi wa barabara na kuwabughudhi watumiaji wengine. Ifahamike kuwa hata baada
ya kuanza kwa ujenzi wa Barabara ya Morogoro eneo hilo limeendelea kutumika pia
kwa mikutano hiyo, kati mikutano hiyo ikiwa ni pamoja na ule uliofanywa na CCM
na kuhutubiwa na viongozi wake wa kitaifa tarehe 13 Januari 2013. Aidha, Meya
wa Manispaa ya Kinondoni Yusuph Mwenda amenukuliwa kwenye baadhi ya vyombo vya
habari tarehe 15 Machi 2013 akieleza kwamba Manispaa ya Kinondoni haijafanya
uamuzi huo kwa kuwa bado iko kwenye mashauriano na wadau kuhusu matumizi ya
eneo husika.
Tatu, sababu
iliyotolewa haikidhi masharti ya yaliyowekwa na kifungu cha 43 (3) cha Sheria
ya Jeshi la Polisi na Huduma za Polisi wasaidizi kwa kuwa Jeshi la Polisi ya
kwamba Afisa wa Polisi hatatoa amri ya kusitishwa kwa mkusanyiko kutokana na
taarifa iliyotolewa kwake isipokuwa tu kama ameridhika kwamba kufanyika kwa
mkusanyiko kuna uwezekano wa kusababisha kuvunjika kwa amani au kuathiri
usalama wa taifa au kutumika kwa dhumuni lolote lisilokuwa halali. Ikumbukwe
kuwa lengo la mkutano nililieleza wazi kuwa ni kuwapa mrejesho wananchi kuhusu
masuala niliyoyawasilisha katika Mkutano wa Kumi wa Bunge uliomalizika tarehe
08 Februari 2013 na kupokea mambo ya kuyazingatia kuelekea Mkutano wa Kumi Na
Moja wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 9 Aprili 2013.
MAAMUZI NINAYOOMBA
YAFANYWE NA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI:
Waziri wa Mambo ya
Ndani kwa kurejea kifungu cha 43 (6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za
Polisi wasaidizi maelezo hayo ya kutoridhika na amri ya kusimamisha mkutano
iliyotolewa na kufanya maamuzi kwamba :
Mosi, ACP Charles
Kenyela Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni alifanya makosa kwa
kuzuia mkutano wa hadhara wa mbunge na wananchi wa tarehe 16 Machi 2013 bila
sababu za msingi, kinyume na matakwa ya Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za
Bunge ambayo inaelekeza kwamba mbunge anao uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara
katika Jimbo lake na mamlaka zote zinazohusika zinawajibu wa kuwezesha mikutano
hiyo kufanyika.
Pili, ACP Charles
Kenyela Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni aadhibiwe kwa makosa
hayo ambayo yamewanyima pia wananchi haki za msingi kwa mujibu wa matakwa ya
Katiba ya Nchi Ibara za 8, 18, 20 na 21 na yamefanyika kinyume na misingi ya
utawala bora.
Tatu, ACP Charles
Kenyela Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni aagizwe kugharamia
mkutano mwingine wa Mbunge na wananchi kabla ya tarehe 9 Aprili 2013 ili
kufidia gharama zilizotumika kwenye maandalizi ya mkutano aliouzuia uliopaswa
kufanyika tarehe 16 Machi 2013. Izingatiwe kwamba taarifa ya mkutano alipatiwa
tarehe 4 Machi 2013 na agizo la kuzuia lilifika ofisi kwangu tarehe 15 Machi
2013, siku moja kabla ya mkutano ikiwa tayari fedha za rasilimali zingine za
maandalizi ya mkutano ikiwemo katika kufanya matangazo ikiwa zimetumika.
Irejewe kwamba kifungu cha 43 (2) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za
Polisi wasaidizi kinaruhusu baada ya kuwasilisha taarifa kuendelea kuitisha na
kuandaa mkutano.
Wako katika uwakilishi
wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Nakala:
· Spika na Katibu- Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
· Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge)
· Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
· Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
· Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma
· Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
· Katibu Mkuu na Katibu wa Jimbo- CHADEMA
No comments:
Post a Comment