Dar es Salaam. Wamiliki wa vituo vya utangazaji vya
televisheni nchini, wamesema watasitisha kurusha matangazo ndani ya mwezi mmoja
kuanzia sasa kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji.
Hatua hiyo inatokana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima mitambo
ya analojia na kuhamia dijitali Desemba 31, mwaka jana kitendo walichodai
kimepunguza mapato yanayotokana na matangazo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania
(Moat), Reginald Mengi alisema hakuna haja ya kurusha matangazo kwa hasara.
Mengi alisema kutokana na kuanza kwa mfumo wa dijitali, watangazaji wamesitisha
kutoa matangazo kwa sababu wananchi wengi hawana ving’amuzi.
“Kama mamlaka itashindwa kurudisha ule mfumo
wa analojia kuwa sambamba na dijitali hadi wananchi watakapokuwa na ving’amuzi,
tutazima televisheni zetu ndani ya mwezi mmoja ujao,” alisema Mengi.
“Ibara ya 18 ya Katiba imekiukwa kutokana na wananchi kunyimwa fursa ya kupata
habari, hivyo hali hii hatutaki iendelee,” alisema Mengi.
Mengi ambaye pia ni mmiliki wa vituo vya televisheni vya ITV, EATV na Capital
TV, alisema licha ya nchi za Afrika,
Tanzania
imekuwa ya kwanza kuzima mitambo ilhali wananchi hawakuwezeshwa kumudu gharama
za ving’amuzi.
“Nchi ambazo zimeendelea kwa kila kitu kama
Uingereza, Marekani, Japan na kwingineko kuzima mitambo ya analojia walitumia
zaidi ya miaka minane kwa nini sisi tumewahi hivi wakati hatujajipanga?”
alihoji Mengi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Sahara Media Group na mmiliki wa Kituo cha Star Tv,
Samwel Nyalla alisema hivi sasa wanaendesha biashara hiyo kwa hasara.
Nyalla alisema hadi mwaka 2015, hali itakuwa mbaya kutokana na kukosa
ving’amuzi.
Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA, Habby Gunze alisema wao hawakualikwa katika
mkutano huo hivyo hawajui chochote. Gunze alimtaka mwandishi kwenda ofisini
leo.
“Sisi hatujui chochote na kama unataka maelezo
mengine njoo kesho (leo) ofisini kwetu uonane na Mkurugenzi Mkuu (Profesa John
Nkoma), ili tuzungumze kwa ‘fact’ (kwa ushahidi) kipi kinachoendelea,” alisema
Gunze.
Nukuu
“Kama mamlaka itashindwa kurudisha ule mfumo
wa analojia kuwa sambamba na dijitali hadi pale wananchi watakapokuwa na
ving’amuzi tutazima televisheni zetu ndani ya mwezi mmoja ujao labda TBC ndiyo itakayobaki”.
Chanzo: Gazeti Mwananchi.
No comments:
Post a Comment