Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya
Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia Tanzania
iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia
taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa mujibu wa barua ya jana (Machi 10
mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari
vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia
Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa
kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na
Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda
iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua hiyo
iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.
FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na
vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa
wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa
wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa
na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara
za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.
“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa
kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za
juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania
kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na
uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala yake pia
imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari
ambazo Tanzania
itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu
kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na
maofisa wengine watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo
yanayotolewa na FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli
kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa
sasa na kutoa mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa
uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu
kushughulikia tatizo hili kwanza.
“Katika mazingira haya tunaomba
ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo
mpira wa miguu wa Tanzania
utakumbana nazo. Tunakushukuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua
inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF)
11 March, 2013
No comments:
Post a Comment