Wakati Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare anatarajiwa kufikishwa mahakamani
leo, jana mchana ofisi za makao makuu ya chama hicho zilipekuliwa na polisi na
kuondoka na nyaraka mbalimbali.
Tukio hilo
lilitokea jana ikiwa ni mwendelezo wa upelelezi wa tuhuma zinazomkabili
Lwakatare ambazo zinazomhusisha na picha ya video iliyorushwa kwenye mitandao
ya kijamii. Lwakatare alikamatwa Jumatano iliyopita akihusishwa na picha hiyo
iliyomwonyesha Lwakatare akiwaelekeza watu ambao hawakuonekana, kufanya vitendo
vya uvunjifu wa amani au uhalifu.
Upekuzi katika ofisi
Polisi hao wakiwa na Lwakatare na mmoja wa mawakili wake,
Nyaronyo Kicheere walikwenda kwenye ofisi za Chadema saa 9.00 alasiri kwa ajili
ya kufanya upekuzi.
Upekuzi huo uliendeshwa zaidi kwenye ofisi za Lwakatare kwenye
Makao Makuu ya Chadema yaliyoko Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam .
Upelelezi wa kesi hiyo unaongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP), Obadia Jonas. Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa upekuzi huo
ulikuwa na lengo la kupata hati zenye mwandiko wa Lwakatare ili kufananisha na
nyaraka mbalimbali walizonazo polisi. Kwa nyakati tofauti, Nyaronyo Kicheere na
Ofisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene walithibitisha juu ya
upekuzi huo.
Kicheere alisema aliitwa jana kwenda Kituo Kikuu cha Polisi,
alipofika alielekezwa kufuatana na mteja wake na polisi kwenda Makao Makuu ya
Chadema.
“Walifanya upekuzi kusaka nyaraka kwa ajili ya kuongeza ushahidi
wa uchunguzi wao,” alisema Kicheere.
Naye Makene alikiri kufanyika kwa upekuzi na kufafanua
ulifanyika ndani ya ofisi za Chadema.
Lwakatare kufikishwa mahakamani
Pia kwa nyakati tofauti Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi, Isaiah
Mungulu na Msemaji wa Polisi, Advera Senso waliithibitishia Mwananchi kuwa
Lwakatare atapandishwa kizimbani leo.
“Upelelezi umekwenda vizuri na kesho (leo) atapandishwa
kizimbani ili kujibu mashtaka yanayomkabili,” alisema Mungulu.
Alipoulizwa kuhusu kupekuliwa kwa ofisi za Chadema jana alasiri,
Mungulu alijibu suala hilo
lilikuwa la kiufundi zaidi.
“Hilo
suala ni `technical’ (kiufundi). Hilo
siwezi kukujibu bwana,” aliongeza Mungullu.
Senso alisema kuwa upelelezi ulikuwa kwenye hatua nzuri na
alithibitisha kuwa walimwita Kicheere kwa mahojiano zaidi kuhusu mteja wake.
“Tumemwita tena leo (jana) Wakili wa Lwakatare kama
mwendelezo wa upelelezi wetu, suala hili linatakiwa lifanyiwe uchunguzi wa kina
kwa hiyo siyo vibaya kumwita mara kwa mara,” alisema Senso.
Lwakatare alikamatwa saa saba mchana Machi 13, mwaka huu katika makao
makuu ya chama hicho Kinondoni, ambapo alipelekwa katika Makao Makuu ya Polisi
kwa mahojiano na baadaye kushikiliwa katika Kituo Kikuu jijini Dar es Salaam.
Chanzo: Gazeti Mwananchi.
No comments:
Post a Comment