Wachezaji wa coastal Union wakipiga jaramba kabla ya kuanza mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar jana.
Mchezo unaopokolea halafu jua linakunyima utamu inabidi utumie akili ya ziada kufaidi soka.
Jana kigoma cha wagosi wa
kaya kimerejea mjini Tanga kutoka Manungu Turiani Mkoa wa Morogoro kikiwa na
shangwe baada ya kupata suluhu ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi ya
ligi kuu ya vodacom Tanzania Bara.
Coastal Union ilikuwa ya
kwanza kuliona lango la Mtibwa Sugar dakika nne tu baada ya mwamuzi kupuliza
kipyenga cha kuashiria mchezo huo wa jana uliojaa kukamiana kuwa umeanza katika
uwanja wa Manungu ndani ya mashamba ya miwa na kiwanda cha sukari.
Ibrahim Twaha ‘Messi’ jana
alifunga goli la kwanza tangu aanze kucheza ligi kuu, ambapo aliunganisha krosi
nzuri iliyochongwa kiustadi na Joseph Mahundi na kumlazimisha golikipa wa timu
ya Taifa Hussein Sharrif ‘Cassilas’ kushindwa kudhibiti shuti hafifu
lililopigwa na ‘Messi’ na kuishia kuumalizia kwa mkono wa kushoto mpira ule
ukaingia wavuni.
Baadae Mtibwa walibadilika
wakaanza kushambulia kwa kasi kiasi Kocha wa Coastal Union Hemed Morroco akawa
hakai kitini kila mara anainuka kuwafokea wachezaji wake. Ingawa mpaka timu
zinakwenda mapumziko matokeo ilikuwa ni 1-0.
Hata hivyo kipindi cha pili
kilipoanza Mtibwa waliingia kwa ari kubwa kiasi kufika dakika ya 67 ya mchezo Vicent
Barnabas alivuruga furaha ya wapenzi wa Coastal Union walioandamana na timu
mpaka Manungu baada ya kusawazisha bao kiubwete kwani mpira ulimgonga mguuni na
kutinga wavuni wakati mabeki wa Coastal Union walipokuwa katika harakati za
kuokoa hatari iliyodumu langoni mwao kwa dakika moja na nusu, hivyo kubadilisha
matokeo na kusomeka 1-1.
Baada ya hapo Mtibwa
walishambulia kwa kasi mpaka mwamuzi anapuliza kipyenga cha mwisho dakika ya 90
matokeo yalibaki 1-1 lakini wagosi wa kaya walikuwa katika hali mbaya sana .
Kudhihirisha hilo wakati wagosi wa kaya
wana kona tatu Mtibwa Sugar walikuwa na kona 12 mpaka mpira unaisha. Na zote
zilikuwa kona hatari kama si umahiri wa
Shaaban Kado golikipa namba moja wa Coastal Union alietokea hapohapo Mtibwa Sugar
leo habari zingekuwa nyingine.
Kikosi cha kwanza kilichoanza
jana Coastal Union ni: Shaaban Kado, Ismail suma, Othman Tamim, Philip Mugenzi,
Mbwana Kibacha, Razak Khalfan, Castro Mumbala, Danny Lyanga, Joseph Mahundi,
Gabriel Barbosa na Ibwahim Twaha.
Baadae kocha akafanya
mabadiliko akaingia Nzara Ndaro akatoka Castro Mumbala, akaingia Abdi Banda
akatoka Razak Khalfan halafu akaingia Mohammed Miraji akatoka Gabriel Barbosa.
Mtibwa Sugar walikuwa ni:
Hussein Sharrif, Said Mkopi, Isasa Issa, Rajab Mohammed, Ally Lundenga, Babu
Seif, Jamal Mnyate, Rashid Kombo, Hussein Javu, Ayub Isiko na Vicent Barnabas.
Kwa matokeo hayo Coastal
Union wataendelea kubaki nafasi ya nne kwa pont 32 wakati Mtibwa watabaki
nafasi ya tano kwa point hizohizo 32 huku Kagera Sugar wakishika nafasi ya sita
wakiwa na point 31.
Ili wagosi wa kaya wawe na
amani katika nafasi hiyo ni lazima waombe mabaya kwa Kagera Sugar kwenye mechi yao tarehe 27 March, uwanja wa nyumbani Kaitaba mjini
Bukoba ambapo wanashuka na Simba
SC.
Mechi nyingine ya Coastal
Union itachezwa jumamosi ijayo jijini Dar es Salaam dhidi ya African Lyon
inayotishia kushuka daraja.
HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
Turiani, Morogoro
17 March, 2013
No comments:
Post a Comment