Sunday, December 2, 2012

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUUNGANO WA TANZANIA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL AMUWAKILISHA RAIS KATIKA SHEREHE ZA KUMUAPISHA RAIS ENRIQUE PENA NIETO WA MEXICO


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mexico City,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amemuwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Enrique Pena Nieto wa Mexico, sherehe zilizofanyika katika jiji la Mexico Jumamosi ya Desemba Mosi 2012. Makamu wa Rais Dkt Bilal amekuwa miongoni mwa viongozi kadhaa maarufu duniani walioshiriki sherehe hizo akiwemo Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden.
Katika sherehe hizo za kuapishwa zilizofanyika katika ukumbi wa Kongresi ya Mexico, ukumbi ulio katikakati ya Jiji la Mexico, Rais Pena Nieto (46) aliapa na kisha kuhutubia taifa huku akifafanua wazi kuwa, suala la kutunza amani na utulivu katika Mexico ni agenda yake ya kwanza, huku suala la kukuza uchumi wa Mexico likifuatia.
Rais Nieto, katika hotuba yake hiyo alikuwa akizungumza kwa lugha ya ustahimilivu, upole na uvumilivu, lugha inayotafsiliwa na wachambuzi wa masuala ya siasa wa hapa kuwa, inalenga kuwatoa hofu wananchi wa Mexico kufuatia wengi hasa wakazi wa mijini kuwa na hofu ya kurejea madarakani kwa chama kikongwe kabisa cha PRI, kilichotawala nchi hii kwa zaidi ya miaka 70 na kisha kudondoshwa mwaka 2000 na Rais mstaafu Filipe Calderon.
Katika hotuba hiyo pia Rais Nieto alizungumzia suala la kukabiliana na uhalifu, ambao umekuwa ukiongezeka badala ya kupungua kadri siku zinavyoenda katika viunga mbalimbali vya nchi ya Mexico. Katika miaka 6 iliyopita, watu wapatao 50,000 walipoteza maisha yao kutokana na matukio ya kihalifu na hasa ule unatokana na makundi yanayojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya. Mexico ni moja ya nchi duniani zinazokabiliwa na uhalifu wa hali ya juu hali ambayo Rais Nieto anasema ameamua kukabiliana nayo, ili kila raia aweze kupita katika barabara za nchi hiyo sambamba na miji ya Mexico akiwa na amani tofauti na ilivyo sasa.
“Nitaheshimu kila mwananchi, nitasikiliza kila hoja. Nitaendesha serikali kwa uwazi na nitakuwa mkweli kwa wananchi wa Mexico. Nitatafuta maoni yenu na nitawasikiliza wote bila kubagua. Nitakuwa Rais ambaye yuko karibu na wananchi,” alisema Rais Nieto katika hotuba yake kwa Taifa.
Katika sherehe hizi, Mheshimiwa Makamu wa Rais ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, sambamba na maafisa kutoka Ubalozi wa Tanzania Washington. Wengine ni maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na mara baada ya shughuli hii, ujumbe wa Mheshimiwa Makamu wa Rais unarejea nyumbani kukabiliana na majukumu mengine ya kitaifa.
Tanzania na Mexico zimekuwa na uhusiano wa siku nyingi uliohasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Uhusiano huu unachagizwa pia na hali ya tamaduni na maisha ya wananchi wa nchi hizi mbili ambao wanafahamika pia kwa ukarimu na tabia yao ya kupenda na kuthamini wageni.
         Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais

---

No comments:

Post a Comment