Na: Mashaka Mhando,Tanga
WATU wanaosadikiwa kuiba vitu vya
marehemu Hussein Mkiety maarufu kwa jina la 'Sharo Milionea' aliyefariki kwa
ajali ya gari katika kijiji cha Songa Kibaoni wilayani Muheza Novemba 26 mwaka
huu, wamesalimisha baadhi ya vitu hivyo kwa mwenyekiti wa Kijiji hicho huku
wakiendelea kuishi mafichoni kuogopa kutiwa mbaroni.
Watu hao wamesalimisha vitu hivyo
baada ya Mkuu wa wilaya ya Muheza Subira Mgalu ambaye ni mwenyekiti wa kamati
ya ulinzi na usalama kuwatangazia kwamba wale wote waliomwibia marehemu
watasakwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kufutia kitendo walichokifanya
kutokuwa cha kiungwana.
Mkuu huyo pamoja na jeshi la polisi
wilayani humo waliendesha msako juzi usiku lakini hawakuweza kuwakuta watu
baada ya kuzihama nyumba zao kuogopa kutiwa mbaroni na mkuu huyo kuwalazimsha
baadhi ya familia walizozikuta kuendesha zoezi la kuwataja watu wanaohofiwa
kwamba huenda watakuwa wamchukua vitu hivyo.
Kamanda wa polisi mkoani Tanga ACP
Constatine Masawe, aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake kuwa, usiku wa
kuamkia juzi mwenyekiti wa kijiji hicho Abdi Zawadi alipelekewa vifaa mbalimbali
ikiwemo nguo ambazo marehemu alikuwa amezivaa pamoja na spea tairi ambalo
waliling'oa na kutokomea porini.
Kamanda huyo alitaja vitu
vilivyokabidhiwa kwa mwenyekiti huyo kuwa ni pamoja na begi lake lililokuwa na
'viwaro' nguo zake, betri ya gari hilo lililokuwa na namba T 478 BVR aina ya
Toyota Harrier, saa yake ya mkononi, simu yake aina ya Blackberry na redio ya
gari iliyokuwa pia imeng'olewa na wezi hao.
Kamanda huyo alisema vitu hivyo
vilipelekwa na mtu mmoja ambaye kwasasa jeshi hilo linashindwa kumtaja jina
lake kwa vile alijitambulisha kwamba ana undugu na wezi hao ambao walimpa vitu
hivyo avipeleke kwa uongozi wa kijiji hicho hatua ambayo alidai kwamba
wanafanya uchunguzi ili kuwatia nguvuni wale wote waliohusika na tukio hilo.
Alisema waliweka mtego baada ya
kusikia kwamba kuna mwizi mmoja wapo anaitafutia mteja simu ya mkononi ya
marehemu lakini wakati wameweka mtego huo kijana huyo alipokuwa akijadiliana
bei na mtu waliyemweka, alibaini na alipompa mkononi alikimbia vichakani kuogopa
kukamatwa.
Kamanda huyo aliwashukuru baadhi ya
wananchi wa kijiji hicho pamoja na Mkuu wa wilaya kuhakikisha wanashirikiana na
jeshi hilo ili kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika katika tukio hilo
ambalo limetokea huku wananchi kadhaa wakiomboleza kifo cha msanii huyo ambaye
alizikwa kijijini kwao Lusanga wilayani Muheza juzi.
Katika hatua nyingine kamanda huyo
alisema katika matukio ya ajali yaliyotokea mwezi huu wa Novemba jumla ya ajali
10 zilitokea ambazo zimesababisha vifo ni 7 na zilizosababisha watu kujeruhiwa
ni tatu, kati ya hizo watu 12 walipoteza maisha na wengine wanane walijeruhiwa.
Kamanda Masawe alisema jumla ya
makosa 2,365 yalitendeka na kupigwa faini iliyosababisha serikali kujiingiza
kiasi cha sh. 70,950,000 hatua ambayo kamanda huyo alisema haioneshi kwamba
watumiaji barabara wamekuwa wakifuata wakitii sheria za usalama barabarani.
No comments:
Post a Comment