Marehem Benson Mollel wa kwanza kulia mwenye saa, akiwa katika shughuli za kijamii mjini Arusha enzi za uhai wake.
MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) taifa, kupitia Mkoa wa Arusha, Benson Mollel (26) amekutwa amefariki
dunia ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business, iliyopo Mtaa wa Jacaranda
katikati ya Jiji la Arusha.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema
Mollel alikutwa akiwa amekufa jana mchana na kwamba tukio hilo limezua hofu kwa wakazi wa Jiji la
Arusha, huku wakijiuliza chanzo cha kifo chake.
Kifo cha mwanasiasa huyo mchanga ambaye pia alikuwa ni
mfanyabiashara wa madini mkoani hapa, kimezusha maswali mengi wakati wengine
wakihusisha tukio hilo
na masuala ya kisiasa na upande mwingine wakidai ni masuala la kibiashara.
Hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba Arusha ni jiji lenye hekaheka
za kisiasa hasa ndani ya CCM ambapo Mollel alikuwa mmoja wa vinara wake.
Polisi waliwasili hotelini hapo saa 8.00 mchana na kuupakia
mwili wa marehemu kwenye gari na kisha kuupeleka Hospitali ya Mount Meru kwa
ajili ya kuhifadhiwa.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya wa Arusha (OCD), Gilles Muruta
akizungumza katika eneo la tukio alisema: “Tunachunguza tukio hili ambalo
ni la ghafla.”
Akizungumzia kifo hicho, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela
alisema: "Tumepokea kwa masikitiko kifo cha Mollel japokuwa sifahamu nini
hasa kimejiri huko."
"Kuna rafiki yake alinipigia simu kuniarifu kuhusu kifo
hicho na nikawaambia kama UVCCM Taifa tupate
maelezo kamili na tujue nini cha kufanya. Iwapo familia itakuwa na mipango
yoyote watutaarifu," alisema Shigela.
Baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa madini mkoani Arusha
walionekana nje ya hoteli hiyo baada ya taarifa za kifo hicho kusambaa na
wengine walishindwa kujizuia kisha kuangua vilio.
Miongoni mwao ni kada wa Chadema, James ole Millya na diwani wa
CCM Kata ya Mlangarini, Mathias Manga. Katibu Mwenezi wa CCM wa Mkoa wa
Arusha, Isaack Kadogoo ambaye pia alifika eneo hilo
alisema kwamba wamepokea taarifa za tukio hilo
kwa mshtuko mkubwa.
Uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari kulizungumzia kwa madai
kwamba limefikishwa katika vyombo vya usalama.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya hoteli hiyo
vilidai marehemu aliwasili usiku, juzi Jumamosi hotelini hapo akiongozana na
mwanamke aliyetambulika kwa jina la Nancy
na kuchukua chumba namba 208.
Mmoja wa walinzi hotelini hapo aliyetembulika kwa jina la Obeid
Mollel kutoka Kampuni ya Ulinzi ya Victoria Support Services, alisimulia kuwa
marehemu aliingia na mwanamke huyo na kisha kuondoka ghafla kabla ya kurejea
tena wakiwa wote usiku.
Alisema kuwa wakati wakiwa hotelini hapo marehemu aliomba
kuegesha gari lake
jipya aina ya Mark II
Grande ambalo halijasajiliwa na kwamba alipokubaliwa alifanya hivyo kisha
akaenda chumbani. Ilibainika kuwa mwanamke huyo aliondoka jana asubuhi.
Taarifa zaidi
Mmoja wa wahudumu hotelini hapo (jina lake limehifadhiwa ),
alisema kuwa mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Mariam aliwasili hotelini
hapo saa 5.00 asubuhi na kuomba kupelekwa moja kwa moja chumba alichokuwapo
marehemu.
Mhudumu huyo alisema wakati mwanamke huyo akiomba kupelekwa
chumbani, marehemu naye alipiga simu mapokezi akiomba mwanamke huyo apelekwe
chumbani kwake, agizo ambalo walilitekeleza.
Kwa mujibu wa mhudumu, baadaye kama
saa 6.00 mchana walimwona mwanamke huyo akitoka nje ya hoteli hiyo na kuondoka.
Alisema kwamba baadaye waliamua kupiga simu ya chumba alichofia
marehemu ili kujua endapo ataendelea kupanga kwani muda wa kawaida ulikuwa
umemalizika lakini simu hiyo ilikuwa ikiita bila majibu.
Mmoja wa wahudumu ambaye alikuwa akifahamiana na marehemu,
aliamua kumpigia kupitia simu yake ya mkononi lakini nayo haikupokewa.
Mhudumu huyo aliamua kupanda ngazi kwenda chumbani kwa marehemu
na katika hali isiyo ya kawaida alikuta mlango ukiwa wazi na marehemu akiwa
amelala.
"Nilijaribu kumwamsha, lakini hakuamka na ndipo alipotoa
taarifa kwa uongozi wa hoteli na baadaye waliviarifu vyombo vya usalama.
Chanzo cha kifo hiki kinakanganya maana kama
kweli ni mauaji basi yamefanyika kwa ustadi mkubwa,” alisema mhudumu huyo na
kuongeza:
“Unajua vyumba vyote vya huko juu ghorofani ukifunga mlango tu
huku chini sisi mapokezi tunasikia, sasa cha ajabu mlango tumeukuta wazi. Hapa
kuna maswali mengi," alieleza mhudumu huyo.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment